Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana; kipekee namshukuru Mungu kwa upendeleo wa zawadi ya pumzi ya uhai ndiyo maana tuko hapa na tunajadili jambo hili kubwa. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho lake la hotuba nzuri na iliyoeleweka; na niseme kwamba mengine ya mwaka jana pia akiwa kama Naibu Waziri yalitekelezeka, kwa hiyo naipongeza sana Wizara hii kwa ujumla, yeye na timu yake ya Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu mwaka huu tufanye zaidi Mheshimiwa Waziri kwa sababu mifugo ni afya, mifugo ni kilimo, mifugo ni lishe, mifugo ni biashara, mifugo ni utalii, mifugo ni usafiri, wakiwepo punda wanaosaidia usafiri, lakini mifugo ni ulinzi; yaani mifugo ni kila kitu, ni Wizara mtambuka. Zaidi sana ni kama walivyotuambia asubuhi, mifugo ni utajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namwambia Waziri wetu kwamba utajiri huu haujawa sasa na uwiano. Kwamba wanaofuga katika kiwango kikubwa watajirike na wale wanaofuga kidogo kule nyumbani watajirike. Mimi natoka hapa hapa kwenye ufugaji mkubwa na kwenda kwenye ile hoja yangu ya kila mtu afuge na ikiwezekana afuge angalau hata kuku wawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiamka nyumbani hata kama una hiyo saa yako ya kuweka alarm lakini kabla ya alarm haijalia jogoo ameshawika. Kwa hiyo, unaona ni jinsi gani kuku walivyo muhimu kwetu Watanzania, asubuhi tunaamshwa na jogoo. Lakini jogoo huyo wa kienyeji tunaambiwa amekuja ameboreshwa; kuna wale majogoo wa kuroiler nao sijui kama wanajua kuwika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimeleta kilio kutoka mkoani kwangu. Tangu wameniona Bunge hili wanawake wa Tanzania wananiona nikiomba vifaranga vya kuku ili kila Mtanzania afuge, lakini jambo hili halijaweza kutekelezwa kiuhakika. Mwaka jana Wizara hii ya Mifugo iliweza kupeleka Kilimanjaro kwenye vikundi saba tu na mashamba darasa mawili. Sasa ile ni kitu kidogo mno. Ninaomba kwa upendeleo mwaka huu twende tupeleke mifugo hii, kila nyumba iwe na kuku. Nilishawaomba sana, ikiwezekana hata tugawe hivi vifaranga kwenye shule za primary maana kuku wa kienyeji hawana gharama, wanachakua tu wanajilisha wenyewe. Sasa kwa nini nyie Wizara ya Mifugo msisaidie wanawake wa Kilimanjaro kufuga? Naomba nipate jibu la sivyo hatujafika kushika vifungu na baba Tulia sitaki mimi kukushikia kifungu nakuheshimu sana. Naomba wanawake wa Kilimanjaro wapelekewe vifaranga wafuge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kuna hela zile ambazo sasa hivi zimesitishwa 4:4:2. Hapa leo tunalia mifugo haikupewa fedha za kutosha, hata mimi nawaombea, na tena niseme rasmi naunga mkono hoja na nataka mpate fedha nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ikiwezekana, badala ya kuwapa wale wanawake, vijana na wenye ulemevu 4:4:2 tuwape miradi, na miradi hiyo si mingine ila miradi inayotokana kwenye Wizara ya Mifugo. Muongee na TAMISEMI mwende kwenye halmashauri, marejesho yatakuwa mazuri, kuliko sasa hivi tumesimama, hamna kinachoendelea, tunangoja sera itengenezwe ilhali hela haikusubiri inazidi kupungua thamani. Naomba sana Wizara ya Mifugo izungumze na TAMISEMI, mtakubaliana tu, hizo hela zitumike tuletewe Tanzania nzima wanawake, vijana na wenye ulemavu tupatiwe miradi, si ya kuku tu tunaweza pia tukapatiwa miradi ya ng’ombe, mbuzi wa maziwa, miradi ya kondoo mpaka ya nguruwe mmesema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nilikuwa naiomba sana wizara hii ishirikiane pia na watu binafsi. Kuna mashamba ambayo yanalelewa labda na mission. Kuna wanaozalisha vifaranga lakini pia kuna watu binafsi wanaofuga. Leo tumewaona pale, na nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri, tumepata shule kweli kweli, pale nje tumepata darasa, tukaoneshwa jinsi gani ASAS anafanya vitu vyake. Kuna shule ambazo anazilea kwa maziwa yale ya ruzuku, anawapa tu; shule zile vijana wale wana afya nzuri kuliko hata wale wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumejifunza, kwamba kuna magonjwa ambayo kama maziwa hayajapitiwa kiwandani, yakafanyiwa treatment yanaleta magonjwa yanayoambukiza. Kuna ugonjwa wa brucellosis ambao sasa kama ng’ombe yule alikuwa inatupa mimba na mama pia akinywa na yeye pia anapata uharibifu wa kile kiumbe ndani yake, lakini kama maziwa hayo yamepitishwa kiwandani inakuwa salama. Ila tatizo lililo Tanzania ni asilimia tatu tu ya maziwa yanayozalishwa rasmi ambayo yanapita kiwanda, mengine yote 97 hayako rasmi. Matokeo yake unakuta hata Serikali inapoteza mapato. Sasa shida iko kwenye Wizara ya Mifugo, vile vituo vya kuokota maziwa sasa vya kukusanyia maziwa, ambavyo vimesambazwa bado ni vichache sana. Vinahitajika 770 lakini mpaka sasa hivi ni theluthi moja tu vimepatikana. Hapo mnatuambia nini Wizara ya Mifugo Tanzania nzima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wangetaka maziwa yao yafike kwenye vituo ambavyo vinaweza vika-process. Kule Kilimanjaro wafugaji wote wa ng’ombe wangependa maziwa yao yaende Nronga au yaende pale Kalali, lakini haiwezekani. Tunaomba mtujengee hivyo vituo ili maziwa hayo yaweze kupitia kwenye hiyo process, maziwa yawe salama na sisi pia tuweze kuwa na maziwa mazuri kila mahali, watoto wanywe maziwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeona sasa hivi tunazungumza tatizo la watoto kuwa na tabia zisizoeleweka ni pamoja na lishe ambayo haieleweki. Lishe ambayo haijawa katika hali nzuri haiwawezeshi kabisa vijana kuwa vizuri, watakuwa hipper tu; na tutapiga sana kelele hapa lakini mtaona kwamba haiwezekani mpaka ninyi Serikali mtusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viko viwanda vingi vya maziwa ambavyo tunatumia maziwa yake nchini, lakini pia ukienda super market unakuta kwamba maziwa mengine pia ni imported. Ukiangalia uwiano wa maziwa ambayo sisi tume- import na tulio-export mengi sisi tumeleta. Wizara hii sasa iangalie, kama tumesafirisha lita 200,000 lakini tukaleta lita milioni 1.6 hapo kuna shida. Ninaomba Wizara na wale watafiti waliofanya kazi ya utafiti waone ni jinsi gani tunakwenda kuboresha mifugo yetu ili tuweze ku-export zaidi tuweze kupata hela za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na niseme wazi mwananchi wa kawaida au mfugaji wa kawaida tu hawezi kununua mtamba wa Tanzania. Niiombe Serikali hii yenye usikivu sana, chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan afikirie kuona upendeleo kwa wafugaji ambao ni zero grazing, wao mifugo yao haitoki nje, maana yake hata haya madume yaliyoletwa, tumeambiwa yatakwenda ranch. Mengine yatakwenda kwa wale waliojengewa vituo, lakini wale wanaofuga ndani ikiwemo Mkoa wa Kilimanjaro, sijaona hiyo allocation ya haya madume bora. Hii inanikumbusha na namkumbuka Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa nasikia machozi, nasikia uchungu, alileta madume yaliyofanya cross breeding yalikuwepo madume ya Friesian, yalikuwepo madume ya Boran, yalikuwepo madume ya aina nyingi na sasa yanaishia na kila siku maswali nimeuliza hapa ndani, lakini sioni wakiitika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona wenzetu majirani wameendelea kuboresha na kuboresha vizazi vya ng’ombe na kuboresha maziwa. Tanzania tuna shida gani? Shida iko wapi? Tuna shule vijana wetu wanasoma vizuri sana. Wanasoma SUA, wanasoma shule nyingine, lakini mapokeo ni kidogo. Niombe sana hii Wizara inayoongozwa na vijana hawa, yuko Mheshimiwa Waziri, yuko Naibu Waziri, wachapakazi, wazuri, sina wasiwasi nao, timu ya Katibu Mkuu iko vizuri lakini pia… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umeisha.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Naomba niliyosema wanisikie na naunga hoja mkono. Ahsante. (Makofi)