Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye hoja iliyoko mbele yetu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi kabla ya kutoa mchango wangu niitumie fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuendelea kuiletea maendeleo Tanzania wananchi wa Zanzibar hawa wa Jimbo la Chakechake, tunaona jitihada na nguvu wanazozitumia kwenye kuiletea maendeleo Taifa hili. napongeza pia jinsi anavyoshirikiana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ally Hassan Mwinyi kwenye kuisaidia Zanzibar kusogea kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mchango kwenye jambo moja tu. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri alivyokuwa akisoma leo hapa, na ukisoma kwenye kishikwambi, kuna ongezeko kubwa sana la idadi ya mifugo kutoka mwaka jana hadi mwaka huu. Kwa mfano kwenye ng’ombe tumetoka milioni 35.3 mpaka milioni 36.6. Kwenye mbuzi tumetoka milioni 25.6 mpaka milioni 26.6, kwenye kondoo tumetoka milioni nane mpaka milioni tisa, kwenye kuku tumetoka miliono 92 mpaka milioni 97. Ukuaji wa sekta umeongezeka kwa asilimia tano, lakini cha kusikitisha moja katika eneo ambalo halifanyi vizuri kwenye kukua na kuongezea Pato la Taifa (GDP) ni eneo hili la sekta ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa National Bureau of Statistics of Tanzania (NBS), statistics zinaonyesha tangu mwaka 2019 GDP haijaongezeka kupitia sekta ya mifugo, yaani sekta ya mifugo haijaongeza tija katika kuongeza growth development product yatu. Kwa hiyo hili ni jambo ambalo Wizara wanatakiwa walichukue kwa uzito na kuona ni jinsi gani sekta italeta maendeleo kwenye kukuza uchumi na kukuza GDP yetu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamechangia hapa, Mheshimiwa Kamonga ametoka kusema hapa, kwamba Tanzania ni nchi ya tatu kwa idadi ya mifugo barani Afrika. Zipo nchi tunazipita kwa idadi ya mifugo, lakini hizo nchi zinafanya vizuri zaidi yetu kwenye uuzaji wa bidhaa za mifugo, hasa nyama kwenye soko la kimataifa. Kwa mfano South Africa ambao hawapo hata top tena wanauza kwa dola za Kimarekani milioni 89.2 kwa mwaka, sisi ni dola milioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sudan wenye idadi ya takriban mifugo milioni 31 tu ambao sisi tunawapita kiujumla, wanauza kwenye soko la dunia takriban Dola za Kimarekani milioni 51, kwenye idara moja tu ya nyama. Misri ambayo nayo haipo hata kwenye top ten tunalingana kwenye uuzaji wa bidhaa za mifugo kwenye soko la kimataifa, hii ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Sasa kinachosikistisha, kuna watu tunawapita kwa idadi ya mifugo lakini wanapofika kwenye soko la kimataifa wao ndio wanatuongoza na wanajipatia fedha nyingi zaidi ya sisi, tunakosea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya ambao ni majirani zetu wao wana kuku karibia milioni 21 tu tunawapita mara nne ya idadi ya kuku wetu takriban milioni 92, lakini wao pato lao wanafika Dola za Kimarekani milioni 71 zinazoingia kupitia mauzo tu ya kuku. Sasa kuna mahali tunakosea kama Taifa, kwa hiyo ndio hapo napotaka sasa Wizara watusikilize na wachukue ushauri wetu wakaufanyie kazi kwa ajili ya kutaka kuboresha sekta hii itusaidie kwenye kukuza uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi moja ya jambo lililoahidiwa kwenye sekta hii ni kwamba tutabainisha na kutenga maeneo ya ufugaji kwa kuyatambua na kuyapima, kuyasajili na kuyamilikisha ili kuongeza maeneo yaliyotengwa kutoka hekta milioni mbili na laki saba hadi hekta milioni sita. Moja kati ya mwarobaini wa kukuza pato letu kupitia sekta hii ya ufugaji ni kuwa maeneo tengefu kwa ajili ya ufugaji. Tumeshaingia kwenye migogoro mingi kwa miaka mingi, tumeona ufugaji wa kuhamahama hauna tija. Ilani imetuelekeza tuyatenge maeneo maalum, tuyaweke tuyarasimishe, tuyapime na tuwape wafugaji wetu wapime, tuwawekee miundombinu mizuri tuwape maji ili waongeze tija kwenye uzalishaji wa bidhaa za mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafeli tunapokwenda kuliendea soko la kimataifa kwenye bidhaa zetu za mifugo. Kuna kitu amekisema hapa mchangiaji aliyepita, kwamba tumeshindwa kuwa-label na kuwa-trace wanyama wetu. Soko la kimataifa linataka uwajue wanyama wako tangu walivyozaliwa, umri wao wanavyokuwa, wanachokula, ukienda uwe na hizo kanzidata za kutosha kwenye soko la kimataifa unapokwenda kuuza hizo bidhaa. Sasa zote hizo hatuna, hatuzijui, kwa hiyo inafanya quality ya bidhaa zetu iwe ndogo na hivyo kufanya competition ya kwenye soko la kimataifa pia nayo iwe ndogo. Kwa hiyo moja katika maeneo ninayoishauri Wizara ni kuongeza tija kwenye kufanya hiyo kwa ajili ya kusaidia ubora wa nyama inayotoka Tanzania ilii iwe juu na hivyo soko la kimataifa tuweze kuliendea kwa usahihi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndio mchango wangu naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)