Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Sina shida na hotuba, imeandikwa vizuri tu, kama kuandika, Mheshimiwa Waziri umeandika. Tatizo linakuja kwenye utekelezaji wa yale ambayo anayaandika. Yaani kama kwenye kuandika, kupangilia hoja, aah uko vizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia dhima ya Sekta ya Uvuvi inasema, “kuhamasisha, kuwezesha na kusimamia uvuvi endelevu, ukuzwaji viumbe kwenye maji, uzalishaji bora wa viumbe wakuzwao kwenye maji pamoja na mazao yake.” Tatizo linaanza hapo. Kule Mtwara na sehemu nyingine za nchi yetu wananchi wamehamasika kufuga viumbe wa majini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kule kwetu Mtwara, watu wako tayari kulima mwani, na kufuga majongoo bahari. Kasheshe inayowakumba, ndiyo hayo ninayokwambia kwamba kuandika siyo hoja, hoja ni kutekeleza. Watu wamehamasishwa, Mheshimiwa Silinde tuliongea, ulienda kuzindua. Hivi tangu umeenda kuzindua, umewauliza hata wanaendeleaje? Tangu umeenda kuzindua mpaka leo, hivi vifaranga vya majongoo havijapatikana na hawajui hatima yao. Ukumbuke wale watu wamewekeza fedha zao. Huko huko tunapohamasisha kwamba watu wakuze viumbe vya majini, walime mwani na kadhalika, lakini wameweka vile vizimba vizuri, wanawalipa walinzi, wanafanya uangalizi mbalimbali; majongoo, vifaranga vitoke Bagamoyo, vikifika Mtwara vimekufa, lakini mnawaambia wafanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasubiri watakuja; watakuja lini? Kwa hiyo, unapokuja kuhitimisha Mheshimiwa Waziri wafugaji wale wa majongoo Mtwara wanataka wapate jibu la uhakika, suala lile linafikia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kuhusu mwani, pia wamehamasika sana, tatizo linakuja kwenye masoko ya uhakika. Suala siyo kuuza kwa sababu hata ukiuza shilingi 200 si umeuza? Tunataka wauze kwa bei yenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko kwenye mazao ya bahari kuna fedha nyingi ambazo Serikali inazipoteza. Kuna fursa nyingi ambazo Serikali ingewekeza ingeweza kupunguza baadhi ya matatizo ya ukosefu wa ajira kwa sababu watu wamehamasika na watu wanatamani wafanye, wanachoshindwa ni uwezeshaji na uwezeshaji huu ndiyo huo ninaosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Hotuba ya Mheshimiwa Ulega, utaona sisi tunaenda kuwa matajiri lakini mwaka jana hapa niliongea vizuri sana nikasema issue siyo kutenga, issue kutekeleza. Sasa nataka nikupe mifano michache kama kawaida, nasoma yule ambaye hakupitia aone hali halisi ya Sekta ya Uvuvi. Sisi tunatoka kwenye bahari tunajua umuhimu wa Sekta ya Uvuvi! Kwa nini Serikali hii haioni umuhimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya Maendeleo, hiyo bajeti hiyo tulitegemea iende ikajenge Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko. Hiyo bajeti tulitegemea hiyo ya maendeleo tulitegemea itoe mafunzo itafute masoko, ijenge majengo ya utawala kwa ajili ya Sekta ya Uvuvi kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kushangaza humu ndani kila siku tunaimba, uchumi wa buluu na uchumi wa buluu ni mtambuka kwa sababu unahusu vitu vingi. Kuna utalii ndani yake, kuna ufugaji wa samaki na uvuvi wake na mazao yote yanayoendana humo. Kuna mambo mengi. Bajeti ya maendeleo, Mradi wa Uchumi wa Buluu. Kwanza fedha zenyewe zinazotegemewa za nje. Walitenga shilingi ngapi? Shilingi bilioni 13, mpaka hapa ninapoongea hakuna hata shilingi kumi iliyotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukikaa humu tunaimba uchumi wa buluu na kwenye hotuba yake Mheshimiwa Ulega ameandika uchumi wa buluu sehemu nyingi lakini hakuna fedha hata shilingi kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi, ilitengewa shilingi ngapi? Shilingi bilioni 50, hapa leo tunapoongea kuna shilingi ngapi ambayo imetoka? Hizo fedha za ndani. Shilingi bilioni 50 imetoka shilingi milioni 426 sawa na 0.9% hata asilimia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi nikawa naongea na wenzangu, kwa hiyo, ukijumlisha hizi fedha zote za maendeleo hizi shilingi bilioni 135 kwenye Fungu 64 Uvuvi mpaka sasa hivi fedha iliyotoka nimekwambia shilingi bilioni 135 fedha za maendeleo, mpaka sasa hivi fedha iliyotoka ni shilingi bilioni 6.47 sawa na 4.8%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa asubuhi nilikuwa nawauliza watu kama mambo ndiyo haya, kuna haja ya kukaa hapa kujadili bajeti ambayo haitekelezeki? Tungesema tu kwamba ikifika kwenye mifugo na uvuvi akamalizie kwanza hiyo ya mwaka jana. Akishamaliza ndiyo arudi hapa. Tunakuja kujadili nini kitu ambacho hakitekelezeki? Ndiyo swali langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo kwenye huo ujenzi wa bandari ya uvuvi umetenga shilingi bilioni 50 umetoa shilingi milioni 426. Leo tena kaweka shilingi bilioni 50 zingine, hizi huku hata 1% haijafika. Tunaenda kuipitisha tunaenda kukubaliana ndiyo? Ndiyo hiyo inahusu nini wakati utekelezaji wake hafifu namna hii? Ndiyo swali langu mimi hilo la msingi. Ikibidi naelewa kwamba bajeti yetu sisi ni cash basis kwamba tukusanye ndiyo tutumie, naelewa wala sina shida juu ya hilo lakini najiuliza; Serikali haijaona umuhimu wa Sekta ya Uvuvi? Ndiyo swali langu ambalo najiuliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa nyingine nayokupa, Serikali ilisema itanunua maboti 158 igawe kwa wavuvi. Kule kwetu Mtwara Mheshimiwa Ulega Manispaa ya Mtwara watu mpaka sasa hivi wako kwenye michakato tu. Kuna boti limeenda kule? Halipo, wako kwenye michakato tunapitisha bajeti nyingine ile ya mwanzo haijatekelezwa. Kwa nini Mheshimiwa tunafanyiwa hivi hasa kwenye Sekta hii? Sisi wengine hatuna madini, hatuna nini tunategemea uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu hapa, ombi langu, yale maboti ile michakato ifike mwisho. Vile vikundi wale watu binafsi wapatiwe ili waweze kufanya kazi zao za uvuvi, hiyo ndiyo hoja yangu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kila nikitamani kuongea, kila nikitamani kuongea najikuta ninahuzunika kwa sababu kuna wataalam wengi sana kwenye Sekta ya Uvuvi ambao wangekuwa wanawezeshwa imani yangu tungekuwa tunasonga mbele sana. Wakati anatoa hotuba yake Mheshimiwa hapo kawataja wengine walimu wake, wengine nini lakini wamekaa tu hawatekelezi kwa sababu hawana fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda TAFIRI hakuna fedha, FETA hakuna fedha, ukienda TAFICO hakuna fedha lakini wale watu wanalipwa mishahara, wale watu wana other charges fedha ambazo wanazitumia kwa matumizi mengine lakini hawafanyi kazi zao kwa sababu hakuna fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Serikali pamoja na kwamba keki ya Taifa inaenda kwenye mambo mengi, wangejitahidi angalau hata isipungue 20%, 30%, 40% lakini unapotoa bajeti 4.8% unategemea wafanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nakushukuru sana. Mheshimiwa Ulega wakati unaandika naomba pia uende kwenye mamlaka wakupe fedha utekeleze, kuandika bila vitendo sawa na hakuna kitu. (Makofi)