Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia Sekta hizi za Mifugo pamoja na Uvuvi. Nianze kwanza kabisa kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa mambo mengi mazuri anayoyafanya kwenye sekta hii, kwa sababu tulivyoona Bajeti ya Mifugo imeongezeka, ingawa Bajeti ya Uvuvi imepungua kidogo; lakini yote ni mazuri, Wizara hii inakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni mahususi sana kwa sababu inachangia asilimia saba kwa upande wa mifugo na asilimia moja kwa upande wa uvuv; na inachangia ajira kwa wananchi, pia na pato kwa wavuvi pamoja na wafugaji. Kwa hiyo, hii ni sekta mahususi kwa sababu inainua hata lishe ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, hotuba yake aliyoisoma ni nzuri sana, imejaa vipaumbele vizuri sana, imejaa mikakati mizuri sana ya kuendeleza miradi kama ilivyopangwa. Ushauri wangu ni kuwa, mambo yote yaliyopangwa yaweze kutekelezwa kwa wakati na pia bajeti ambayo tunaomba, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuweze kuipitisha kwa sababu hii ni sekta mahususi, na ni sekta nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Mifugo ina mambo mengi. Ukitaka kupata mifugo bora lazima ufuate kanuni mbalimbali ambazo lazima mifugo iwe nazo. Kwa upande wa kwanza lazima iwe na malisho. Nimeona Mheshimiwa Waziri kwenye sekta yako una mipango mizuri sana ya kuboresha malisho. Malisho kwa upande wa sekta binafsi pamoja na malisho kwa upande wa Serikali, na malisho yanayoanzishwa tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali kuwa jambo muhimu sana hapa ni malisho. Malisho yaangaliwe kwa umakini sana. Malisho yasitengwe kwenye mikoa fulani au kwenye Halmashauri fulani. Yawepo mashamba darasa ya malisho, na ikiwezekana mashamba darasa kwenye kila Halmashauri, kwa sababu mtu akiona, anaweza akaenda aka-practice yeye mwenyewe akaweza kuwa na malisho. Kwa upande wa malisho, pia kuna suala la mbegu. Kama wanavyosema, bado kuna tatizo la mbegu, lakini naona kwenye hotuba kwamba kuna mashamba ambayo yametengwa kuzalisha mbegu pamoja na shamba la vikugwe na mashamba mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hizo mbegu ziweze kupatikana madukani kusudi wafugaji waweze kupata mbegu na kuwa na mashamba na hii itapunguza migogoro mingine ambayo inaendelea au isiyo na lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ili wafugaji waweze kufuga kwa tija lazima waangalie yale mambo ya afya ya mifugo. Hii inaenda pamoja na chanjo na maji. Hapa nasemea upande wa mabwawa na malambo. Ni jambo la muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malambo na mabwawa yanachimbwa. Tumetembelea mabwawa mbalimbali, lakini unakuta mwisho wake yanakuwa siyo bora, kwa nini?

Nilikuwa nashauri ianzishwe mamlaka kama Mheshimiwa Waziri alivyosema kwenye hotuba yako. Hiyo mamlaka shughuli zake hasa, ziwe ni ufuatiliaji wa miradi hii ambayoe ni majosho, malambo ili kusudi yaweze kuendelea vizuri. Miradi ipo, lakini ufuatiliaji wake siyo mzuri. Naamini ikianzishwa mamlaka, mambo yatakuwa mazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa madume bora ni jambo muhimu sana. Nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri; najua kuwa madume bora 366 yameshanunuliwa na kusambazwa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kuwa hata hivyo, kuna wafugaji wazuri ambao wanaweza wakazalisha na madume bora kusudi hawa wananchi wafugaji hasa waweze kupata elimu ya kutumia madume bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye madume bora, kuna uhimilishaji. Wananchi wengi hawana elimu ya uhimilishaji. Nilikuwa namshauri Mheshimiwa Waziri kuwa Maafisa Ugani tulionao ambao ni wazuri, ni wasomi, wanafanya kazi nzuri, waweze kuwafikia wakulima na wafugaji, na kuwaelimisha kuhusu mambo ya uhimilishaji. Kwa mfano nina ng’ombe mmoja na una ng’ombe mmoja; natoa mfano wa ASAS mwenye ng’ombe wengi, lakini unakuta lita kwa ng’ombe mmoja anapata lita ya maziwa 36 kwa siku. Kwa nini uwe na ng’ombe wengi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja tena kwenye upande wa Maafisa Ugani. Nashukuru kwa Serikali kuwapitia pikipiki 1,012 hivi ambazo wamewanunulia. Ni jambo zuri sana. Mmewapatia na simu za kinganjani, mkiwemo na wenyewe kama Wizara ya Kilimo. Kwa hiyo, naomba, ingawa wako TAMISEMI, lakini Wizara pamoja na Serikali waweze kuwafuatilia kuona wanawafikia wafugaji. Wakati mwingine hawafiki kwa wafugaji, mpaka uwaite wewe mwenyewe, lakini kwa sababu wamepatiwa pikipiki, naamini watafika kwa wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili twende na sayansi na teknolojia, ni lazima tuboreshe huduma za mafunzo pamoja na utafiti. Kwa hiyo, fedha za bajeti zilizotengwa kwenye mambo ya utafiti, naomba zikishatolewa zote, waweze kupata bila kukata hata senti moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wafugaji na wakulima pamoja na watumiaji wa ardhi, kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi naamini unanisikia, uweze kushirikiana pamoja na Wizara hii ya Mifugo kusudi hawa wafugaji waweze kutengewa ardhi yao waimiliki, wasibughudhiwe kusudi waweze kupata malisho yao, waweze kupanda malisho yao kwenye ardhi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru mmetatua migogoro mbalimbali kwa upande wa Morogoro na wenyewe umetatua lakini kwa upande wa Morogoro, kwenye Bonde la Kilombero kwa upande wa Kilosa, Mabwelebwele, Tindiga, Kilangali bado migogoro ipo. Mheshimiwa Waziri naomba ulifanyie kazi kusudi tuweze kulitatua hilo pamoja na sehemu nyingine ambazo sikuzitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa utambuzi wa mifugo,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nasisitiza, kwa faida yake, utambuzi wa mifugo uweze kuangaliwa, na mwisho ni uchumi wa bluu, na ufugaji wa vizimbani pamoja na malambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki wanapotea, lakini tukifuga kwenye vizimba, naamini tutapata samaki wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana.