Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwanza napenda kuipongeza Wizari yetu hii ya Mifugo na Uvuvi; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wake wote wa Wizara. Kwa kweli wametuletea bajeti ambayo imegusa kila sekta na matarajio yetu wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiona Sekta hii ya Uvuvi na Mifugo kwamba hii ni sehemu ambayo Serikali yetu itainua kipato cha mwananchi mmoja mmoja, kitaongeza ajira, na lakini pia kitaleta uchumi mkubwa ndani ya Nchi yetu. Tunafahamu kwamba kuna baadhi ya nchi hapa duniani zinaendeshwa kwa uvuvi tu na nyingine kwa mifugo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza na pia nampongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar kwa sababu kwenye uvuvi wa Bahari Kuu ni chombo cha Muungano na ndiyo maana Mawaziri wetu wote wawili wako hapa na kila mwaka tunawaona. Nawapongeza sana kwamba na kule Zanzibar sasa kuna mikakati madhubuti ya kuhakikisha Zanzibar nayo kwa kushirikiana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia chombo hiki cha uvuvi wa Bahari Kuu kinataka kuwekeza kwenye Sekta hii ya Uvuvi wa Bahari Kuu. Nawapaongeza sana Serikali zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, naipongeza Wizara kwa kusamehe na kuondoa tozo mbalimbali katika Sekta zote; za Uvuvi, Mifugo na mambo yanayohusiana na mazao hayo, ikiwemo Sekta ya Maziwa. Sekta ya Maziwa ilikuwa ina changamoto nyingi sana huko nyuma kutokana na tozo mbalimbali ambazo zinakwamisha ukuaji wa sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo nane zimesamehewa au zimeondolewa katika Sekta ya Maziwa. Ninachokiomba sasa, tuendelee kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya maziwa kwa maziwa yanayodumu kwa muda mrefu ili kuokoa maziwa ya wafugaji wetu yasiharibike na sisi kuepuka kuingiziwa maziwa ambayo virutubisho vyake vimeongezwa baadhi ya mambo ili kuathiri afya zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa chakula pia unapatikana kwenye Sekta hizi mbili; Mifugo na Uvuvi. Naipongeza sana Serikali kwa kutaka kuwekeza katika Sekta hizi. Nikiendelea, Serikali inawekeza fedha nyingi sana kwenye Sekta ya Ufugaji kwa kuwajengea mabwawa wafugaji wetu huko waliko. Cha kusikitisha, uwekezaji ule unatuvunja moyo kwa maana haufikii viwango vile ambavyo vinatarajiwa. Ninachokiomba kwa Wizara, pamoja na kwamba maeneo ya wafugaji yako ndani sana, wawe na ufuatiliaji wa mara kwa mara kuhakikisha malambo na mabwawa hayo yanajengwa kwa viwango vinavyostahili ili kuzuia kupoteza fedha za Serikali, na walipa kodi ambao ni wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Sekta hii ya Mifugo, bado mfugaji hafaidiki na soko au fedha kutokana na bidhaa yake ya ufugaji. Tumepata masoko kutoka nje ya nchi, majirani zetu tunao, lakini kiunganishi hapa kinakuwa kikwazo, kwa sababu wanakutana na madalali. Madalali ndio wanaokwenda kwa wafugaji, wanawachukua ng’ombe mpaka Dar es Salaam, wanawakabidhi wale wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hii ni Sekta binafsi lakini kuwe na kiungo, kama kituo kuhakikisha mnunuzi anajua afike wapi ili aweze kuwapata hawa ng’ombe kupitia kwa mkulima au mfugaji mwenyewe ili afaidike zaidi yule mkulima na mfugaji, sio dalali. Kuna udalali mkubwa hapo unaofanyika kwenye Sekta hii ya Mifugo. Kwa hiyo, tuendelee kuimarisha sekta zetu au tasnia zetu za utafiti kwenye uvuvi na kwenye mifugo. Hapo ndiyo tutapata malisho bora, tutapata mbegu bora, na mazao bora kwa ajili ya sekta zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie uvuvi wa Bahari Kuu. Muda mwingi tulikuwa tunapiga kelele kuhusu sekta hii kuwekeza katika uvuvi wa Bahari Kuu. Naipongeza kwa dhati Serikali, sasa imejikita kuingia kwenye Sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu, kwa maana ya kwamba imeagiza meli mbili za uvuvi kwenye ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kule Kilwa, tumeona mambo yameanza. Tunachoomba sasa, Serikali iwekeze fedha kwa haraka ili bandari ile imalizike, meli hizo zinunuliwe, na vifaa vyake vingine vijengwe ili tuingie kwenye Sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu, nasi tuweze kufaidi rasilimali alizotupa Mwenyezi Mungu kwa kupitia bahari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye uvuvi wa Bahari Kuu, izungumzie Shirika la TAFICO. Nimeona mipango mingi ambayo imepangwa kwa ajili ya kulifufua hili Shirika ili lianze kazi. Shirika hili linahitaji uwekezaji mkubwa, linahitaji fedha nyingi kwa sababu miundombinu yake inatumia gharama kubwa. Tusione shida kuwekeza, kwa sababu tukiwekeza leo tutafaidika kesho. Tunapowekeza zaidi kwenye Shirika la TAFICO tutavuna zaidi mabilioni kwa mabilioni ya fedha na tutaongeza ajira, tutaongeza ukuaji wa uchumi na pato la Taifa. Shirika hili ni muhimu, litatukomboa kwenye sekta ya uvuvi, tutakapoingia kwenye uvuvi wa Bahari Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanye hili Shirika lianze kazi haraka, liungane na bandari ya uvuvi tuingie kwenye uvuvi wa Bahari Kuu, tufaidi. Tusiwe kila siku tu tunapiga kelele, Bahari Kuu, Bahari Kuu! Bahari imejaa Samaki, nchi za nje wanakuja na meli zao wanavua, sisi tumekaa. Mwenyezi Mungu katuruzuku hii rasilimali, tuitumie, tuwekeze, tukavuna zaidi ya tunachowekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, nimeona kwenye Wizara, Serikali ina mipango ya kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo kwa zana za uvuvi. Tuendelee kuwasaidia wavuvi wetu kwa mikopo nafuu ili waingie kwenye Sekta ya Uvuvi na wao wafaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi ni kazi ngumu. Unapotoka kwenda kuvua, unajua kwenda, hujui kurudi. Ikikukuta dhoruba huko, unaweza ukapotea baharini na usirudi, au kwenye visiwa usirudi, au ukapotelea nchi jirani baada ya miezi mitatu ndiyo unaokotwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi una hali ngumu, tuwawezeshe wavuvi wetu wavue kisasa na kwa tija. ikiwepo kuzifanyia marekebisho sheria na sera mbalimbali za uvuvi, iwe ni yenye manufaa kwetu na wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, kuna mfumo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kusema, tuendelea kuvua na kufuga kwa kuhifadhi mazingira ya nchi, ili kunusuru nchi yetu isije ikawa jangwa na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)