Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja Iambayo iko mezani. Kwanza nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwaongoza Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kaka yangu na swahiba wangu Abdallah Bin Ulega pamoja na Naibu wake ndugu yangu David Silinde pamoja na Wizara nzima kwa ujumla kwa hotuba nzuri yenye maono, yenye uelekeo mzuri ambayo inaonekana wazi kwamba tunapata mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Uvuvi pamoja na Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu nimeipitia hii hotuba na nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri, nimesikiliza pia maoni ya Kamati ambayo mengi yameipongeza Wizara. Nasema kama haya waliyoyaandika ndani ya hii hotuba wataenda kuyatengenezea mpango kazi, Mheshimiwa Waziri tutatoka kidedea na tutaona namna ambavyo sekta hii itafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kama ambavyo wamepongeza wengine kwa uteuzi alioupata pamoja na wenzake lakini niamini kwamba kwa nguvu aliyonayo, maono aliyonayo, hamu aliyonayo, Wizara hii itaenda kubadilika na italeta matokeo chanya yaliyotarajiwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia taarifa ya Mheshimiwa Waziri na bahati nzuri sana imejieleza kwenye Kamati, kuna malengo waliyojipangia hawakuzidi asilimia 40, kwa maana kwenye mapato, kwenye maduhuli ambayo walitegemea. Pia kuna mipango mingi ilikwama katika mwaka wa fedha uliopita. Hiyo ni kwa sababu ya rasilimali fedha, lakini mipango yao inawezekana haikufika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini mwaka huu wamejifunza na wamefanya tathmini, tunaamini mwaka mmoja ujao tutakuwa na mabadiliko mengine ambayo tumeeleza. Hata hivyo, nikiangalia katika hili tunayo mifugo mingi sana, tunao ng’ombe milioni 36 kwa mujibu wa taarifa ambayo tumeiona hapa. Tunaona tuna mbuzi wa kutosha, tuna kondoo wa kutosha, lakini kama haitoshi tuna rasilimali kwenye Bahari pamoja na Maziwa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini tukitumia vizuri hii mipango tuliyoipanga, tutakuwa na matokeo makubwa na Wizara hii itachangia fedha nyingi kwenye pato la taifa. Tumeona wamesema ni asilimia saba tu inachangia kwenye pato la Taifa, bado ni ndogo. Kama walivyosema wengine ni kwamba mifugo tuliyonayo inawezekana kuna changamoto ambayo tunapaswa twende nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ambalo nimeliangalia kidogo, ni upande wa ukusanyaji maziwa. Ukiangalia Nchi za Afrika Mashariki wenzetu wa Kenya wameweza kukusanya lita 1,241,000, watu wa Uganda wamekusanya maziwa Lita 707,560, lakini sisi Tanzania tumekusanya lita 64,837. Sisi tunasema tuna ng’ombe wengi, tunasema tunayo rasilimali nyingi, tuna eneo kubwa la kufugia, lakini bado tunaweza kukusanya maziwa kiasi hiki kidogo, maana yake bado kuna kazi hatujafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Sisi tunafanya ufugaji wa kienyeji. Ng’ombe wetu si kwamba tunawaona kwa mazingira, ng’ombe wetu ni wadogo, hawana kilo nyingi, nyama zao hazivutii kuliwa. Tukienda kuchoma mnadani tukala tunaamini nyama nzuri, lakini ikienda kwenye vipimo na vipimo vinavyotakiwa nyama ile ni kama haitakiwi. Nini tunatakiwa tufanye? Lazima tupige hatua moja mbele na ndio maana nakuja na ushauri. Mheshimiwa Waziri, amefanya kazi nzuri, mipango ni mizuri, lakini nimeona nami niweke mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni eneo la Ranch za Taifa. Mheshimiwa Waziri Ranch zetu hazifanyi kazi, ni kama hazipo, yamebaki kuwa mapori tu. Ranch hizi ziliwekwa makusudi ili zisaidie mapinduzi ya ufugaji nchini. Kulikuwa na uwezo wa wafugaji wetu kwenda kujifunza, maeneo mengi leo Ranch zimebaki kuwa na walinzi tu. Mameneja wale wapo tu wanaangalia kulinda angalau wasije wakaibiwa majengo yale ambayo yako pale. Hii sio sawa. Hata ukiangalia leo Waziri ametuambia hapa Ranch ya NARCO amenunua vitu lakini vitu venyewe vilivyonunuliwa ni vichache, yaani bado hawezi kujivunia kwamba kuna hatua watapiga. Kwa hiyo, naamini kabisa kwamba Ranch zetu zingine ziko grounded kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ninayotaka kusema ni hii, huu mpango mnaokuja nao wa kuwasogeza wawekezaji ambao watakuja kufanya na sisi ili waweze kutumia miundombinu tuliyoiweka kama Serikali kuweza kunenepesha ng’ombe, kuweza kuongeza utaalam, uhamilishaji na vile vituo kwa sababu viko karibu na wananchi, wananchi waje wajifunze pale. Mheshimiwa Waziri hapo ndiyo atakuja kuleta mapinduzi makubwa ya ufugaji hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hili walilokuwa wanataka kulianza la kuhakikisha kwamba wanakwenda kuwakaribisha wawekezaji ambao watakwenda kusimamiwa na wataalam wetu wengi ambao wako Wizara ya Mifugo, Wizara ya Mifugo ni kama Wizara ya Kilimo ina wataalam wengi sana. Mheshimiwa Waziri awatumie hawa waweze kuleta mapinduzi ya ufugaji katika nchi yetu. Nilitaka nieleze hilo kwa upande huu wa Ranch zetu, najua mipango wameshai-set, lakini naongezea eneo hilo. Wafanye vizuri, wakaribishe wawekezaji, wawasimamie, naamini tutapata matokeo ambayo tunayatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni miundombinu. Tumekuwa tukijenga majosho, tumekuwa tukijenga mabwawa, tumekuwa tukijenga miundombinu mbalimbali inayosaidia ufugaji wetu. Hata hivyo, hizi fedha tumekuwa tukizitupa kwenye halmashauri, kule hakuna mechanism ya kuzisimamia, leo majosho mengi yamekufa, mabwawa mengi yamekufa hatuna uwezo hata wa kuyakarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumshauri Mheshimiwa Waziri kwamba tuunde kama ikiwezekana Tume maalum kama ilivyokuwa Tume ya Umwagiliaji, tuwe na Tume ambayo itaenda kuratibu rasilimali ya mifugo kule kwenye Halmashauri zetu. Kule kwenye Halmashauri unakuta Afisa Mifugo yupo mmoja tu wakiingia pale Mkurugenzi vipaumbele vinakuwa ni sekta nyingine lakini sekta ya mifugo haiangaliwi ambayo ndiyo inabeba watu wengi kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri eneo hili muone namna ambavyo mtaweza kufanya, kuundwe Tume fulani mfano kwenye maji tuliona tatizo tukaunda RUWASA tuliona kuna matatizo tukaunda TANROADS leo hii kuna barabara zinajengwa, leo hii unaona kuna ufuatiliaji na mambo kama hayo, kwa nini tusifanye kwenye mifugo inawezekana tukiamua ili fedha nyingi zinazoenda kule zikasimamiwe na tume maalumu ambayo italeta matokeo ambayo tunayatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili pia nina maombi yangu katika Wilaya yangu ya Ikungi, eneo hili kama wafugaji tunao tunahitaji majosho, tunahitaji mabwawa lakini tuna maeneo ya Kata za kimkakati ambazo tukiwekewa majosho haya yatasaidia kuleta mapinduzi. Mojawapo ni Kata ya Siuyu, Kata ya Mang’onyi, Kata ya Isuna, Kata ya Mkiwa na Kata ya Misughaa maeneo haya Mheshimiwa Waziri yanao wafugaji wengi wakiwekewa miundombinu ya mabwawa, wakiwekewa majosho utaona mabadiliko ya ng’ombe wetu na utaalam ambao unataka kutuletea wa yale madume ya mbegu ambayo yataenda kubadilisha kizazi cha mifugo ninaamini kabisa tutabadilidha ufugaji wa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nimalizie kuhusu uvuvi pamoja na kuwa sisi hatuko Pwani, pamoja na sisi tuko Kati huku Mheshimiwa Waziri lakini na sisi tuna mabwawa na tuna maziwa, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri ninalo bwawa langu linaitwa Muyanji liko pale Singida, bwawa hili limejengwa toka enzi za ukoloni, bwawa hili tumekuwa tukipata kitoweo cha samaki lakini hapa katikati tumekuwa tukipata ups and downs kwa sababu hatupati samaki wazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018 tulipeleka vifaranga 3,500 kupitia Halmashauri yetu tukapandikiza mle ndani, wananchi wameendelea kupata kitoweo pale, vijana wetu wanapata shughuli za uvuvi pale, ninakuomba sana ikikupendeza bwawa lile limepungua kina nikuombe sana tupate fedha tukatoe zile tope zilizoingia mle ndani, tuliboreshe vizuri kwa kujenga miundombinu sehemu ya kunyweshea mifugo iwekwe ili isiendelee kutifuatifua udongo utakaoingia ndani ya bwawa lile, ili bwawa lile la Muyanji liendelee kutoa Samaki, kwa sababu Wizara yako inatusaidia kwenye protini na samaki kule pia tuwapate kwenye Wilaya yetu ya Ikungi na hasa kwenye eneo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hili ukilifanyia kazi utakuwa umetufanyia vizuri, baada ya maeneo haya nakushukuru, naunga mkono hoja, nakushukuru nakutakia kila la kheri. (Makofi)