Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia hii Wizara muhimu, Wizara moja ya sekta za kiuzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma sana randama ya Wizara hii. Nimesoma Hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nimesoma maandiko yake yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema, naunga mkono hoja ya Wizara hii. Nataka kusema, naunga mkono hoja Wizara hii ipite.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika randama, Ukurasa wa 17, ukurasa wa 18 na ukurasa wa 32, mara tatu, Waziri ametamka kwamba, yeye migogoro ya Rutoro na Mwisa ameshaachananayo anasubiri huruma ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, waende wapime, wananchi wa Rutoro na Mwisa waishi kwa amani. Amesema mara tatu. Naunga mkono hoja ya Waziri kwa misingi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunaingia karne ya 21, tuliandika Dira ya Taifa. Hayati Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema, aliandika dibaji, nitanukuu sehemu ya dibaji, kwamba, “Tunapokwenda kwenye ile karne ya 21 lazima tuwe na nguvukazi yenye ustadi mkubwa na hulka ya kujituma.” Nguvukazi yenye ustadi mkubwa na hulka ya kujituma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeunga mkono bajeti ambayo Waziri anakiri kabisa kwamba idadi ndogo ya Watumishi katika Sekta ya Uvuvi ikilinganishwa na mahitaji ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani alivyosema Mzee Mkapa mmemsikia; mtu ambaye nimemuunga mkono, amekiri kabisa kwamba, rasilimali watu aliyonayo, haimtoshi. Namuunga mkono Mheshimiwa Rais anaposema kwamba, mifugo na uvuvi ni utajiri mkubwa. Nikipata muda nitawaonesha. Kuwa na utajiri siyo hoja, kuchota utajiri ndiyo ngoma ilipo. Hatuna rasilimali ya kuchota rasilimali zile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali Wizara hii, nitawaonesha rasilimali zilipo, waongezewe pesa, kwani hizi pesa hazitoshi. Waongezewe pesa kwa ajili ya kutengeneza rasilimali, na zana za kuchota raslimali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilizungumze na hili ni kwa Wizara zote; sekta zote za kiuzalishaji. Mnapotuletea bajeti, mnapojinasibu mahali popote, pamoja na kazi nzuri ambazo Wizara hizi zinafanya, kuleta chakula, kutengeneza ajira, malighafi za viwanda, mtueleze clearly ni kiasi gani tunapata pesa za kigeni? In bolded font.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tuna-export na kupata pesa za kigeni dola bilioni 10 hazifiki, ni tisa na kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ukraine ana-export 68 billion dollars; sisi tunapata nini? Madini tuliwasikia lakini kwa kufichaficha, tunapenda tujue, tuige mfano ule wa Ajenda 10/30. Ajenda 10/30 anakueleza malengo yake atapata kiasi gani kwa dola ambayo na mimi sikubaliani naye, nasema amejiwekea malengo kidogo. Lakini ninapenda hii iwekwe wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi kwa kampuni ya maziwa ya Asas. Kazi mliyofanya ujombani Busokelo, Rungwe nzima ni nzuri. Waheshimiwa Wabunge, Kampuni ya Asas inaagiza ng’ombe wa maziwa kutoka Afrika Kusini, ng’ombe mmoja ukimlisha unapata kilo 25, anawakopesha watu wanafuga halafu wamrudishie. Mheshimiwa Waziri, kama unaijua Kampuni ya Asas na tunagombania mwisa, nakuomba mjomba leta Asas Company Ltd. tumpe aardhi awagawie wananchi wa kwetu wa Kagera hao ng’ombe na ajenge viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze watu, hawaelewi; hekta 600,000 za NARCO nusu yake ziko Kagera. Kwa hiyo, wananchi waliozoea kutumia ardhi ile, imetwaliwa. Sasa niko tayari kufanya kazi nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na wewe nikuombe umweleze Waziri kwamba kwenye mabanda yale wasituoneshe ila waweke na banda la watu kutoa maoni na kubadilishana uzoefu kwa sababu tuna uzoefu tofauti. Tusiende kuangalia, turuhusiwe kutoa maoni yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanafanya fujo, nilindie muda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017 Tanzania tuliuza nje samaki wenye thamani ya dola milioni 193 kwa takwimu nilizonazo. Na hizi ni takwimu za World Fish Center. Rasilimali ya maji tuliyonayo sisi Tanzania siyo wa kuuza kiasi hiki. Mahesabu yanakuonesha wewe kuuza dola milioni 800 inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nchi ya Morocco ambayo tunawazidi kwa wingi wa maji wanauza samaki duniani 2.5 billion dollars. Sisi tuna maji mengi kuliko Morocco, ndipo linapokuja suala la rasilimali. Ukiweka shilingi katika sekta hii unapata shilingi 2.5. Serikali muweke shilingi kwenye sekta hii ili tupate pesa nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kiburi cha Taifa lolote ni uwezo wa kuuza nje, na imeandikwa hata kwenye Dira ya Taifa, huwezi kujenga uchumi shindani kama huna huo uwezo wa kuuza nje. Kwa hiyo, nilikuwa nawaeleza hiki kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine kwenye sekta hii ni kwamba asilimia 97 ya wanaozalisha hawa samaki tunaowazungumza ni wafugaji wadogowadogo, wavuvi wadogowadogo. Kwa hiyo, Serikali mpeleke pesa kule kwa wafugaji hawa wadogowadogo, kwa wavuvi hawa wadogowadogo, ili hao watu sasa watusaidie kujenga uchumi jumuishi. Uvuvi wa samaki utakaoleta watu wengine wakawatoa hawa ndani ya shughuli patakuwa hapakaliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwa nini tuko hivi; moja wapo ya changamoto za Wizara hii au sekta hii ni uvuvi haramu. Lakini uvuvi haramu siyo suala la Tanzania tu, hoja hapa siyo kwamba tuna uvuvi haramu, hoja ni kuu-manage, tunau-manage namna gani. Uvuvi haramu duniani, overfishing, unasababisha mapungufu ya 83 billion US Dollars; hizo ni taarifa za World Bank.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utaona kwamba hii 193 niliyowaambia ya mwaka 2017, tungefanya kazi kwa tija, kwa kuzuia overfishing na uvuvi mwingine haramu, tungeweza kuchupa na kwenda kwenye nafasi nzuri. Nilimueleza Mheshimiwa Waziri nikiwa Goziba kwamba nitakuja nimuoneshe nilichokiona Goziba. Uvuvi haramu umezidi mipanga na Wizara hii peke yake haiwezi kuutatua, mnahitaji kupata msaada wa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nikaomba aweke banda la maonyesho pale ili nije wasionioneshe, na mimi niwaoneshe nilichokiona Goziba, Bumbire, Kelebe, Makibwa na Nyamburo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye sekta ya nyama, hesabu zangu za haraka – nisije nikakosa muda – sekta ya nyama kirahisi inaweza kutuingizia dola bilioni tano. Kama kuna mtaalam katika Wizara hii ana mashaka, tukakutane kwenye banda pale nimuoneshe kwa mahesabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuwa na ng’ombe milioni 35 halafu ukashindwa kuuza nyama inayofikia bilioni sita kwa mwaka. Hata ungewachinja wale ng’ombe kwa kipindi cha miaka kumi, chukua ng’ombe milioni 35 wagawe namna hiyo, utaona hizo figures. Nitakuwa kwenye banda la maonyesho pale, niwekeeni zulia nije niwaeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kufanya nini; mmeizungumzia NARCO kwamba itawataka wawekezaji waje na business plan; hakuna. Ninyi ndio muwape NARCO masharti watakayoyafuata, wewe ndio uandae business plan. Ndiyo maana hata watu wa estate mtu anajenga nyumba, iwe hoteli, iwe hospitali au klabu, watu waende kucheza. Huwezi kufanya klabu ukaigeuza kwamba ni hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo NARCO ianzishe business plan ili watu waje wafanye nini. Na hiyo business plan iwahusu hawa waliopewa vitalu na wale watakaokuja. Siyo unajenga kitalu cha kufuga ng’ombe mtu analeta ng’ombe analingana na mbuzi; haiwezekani. Ufugaji wa kuweza kufikia malengo niliyowaeleza inatokana na malisho, mbegu utakayoleta na utunzaji wake, ili tuweze kufuga nyama tupate nyama inayoweza kufikia hizo dola bilioni tano ambazo nakueleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, umezungumza Mheshimiwa Waziri nakuunga mkono, watu sasa wanataka nyama inayozalishwa Tanzania. Na jambo la faraja ni kwamba katika nyama wanayohitaji ni wanyama wanaofugwa kirahisi; anaongoza mbuzi, anakuja kondoo, ng’ombe ni wa tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kote nilikokwenda kujifunza – siwaambii tena mambo ya Uganda – hapahapa Tanzania, hapahapa Iringa, kuna Watanzania wamefanya maajabu, Asas anawaongoza na wengine wanafuatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema mwanzo na awali kwamba naunga mkono hoja, naendelea kuunga mkono hoja. Nimemuona Mheshimiwa Waziri wa Ardhi ananiangalia, na yule wa Ofisi ya Waziri Mkuu ananiangalia; naomba kuwasilisha. (Makofi)