Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge waliochangia katika bajeti yetu ya Wizara ya Madini. Kabla sijapitia hoja chache ambazo nitazipitia na Waziri wangu atakuja kufanya hitimisho na kujibu hoja zingine nitumie fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ya kuwa msaidizi wa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya Naibu Waziri. Pia nikushukuru wewe Mwenyekiti na uongozi mzima wa Bunge ukiongozwa na mama yetu Mheshimiwa Daktari Tulia Ackson Spika wetu na Naibu Wake na ninyi Wenyeviti wetu kwa jinsi mnavyotuongoza vizuri katika Bunge hili tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwa dakika hizi chache ambazo nimepewa pia kumshukuru Waziri wangu kwa uongozi wake madhubuti anavyotuongoza sisi katika Wizara hii ya Madini na watendaji wote wa wizara yetu ambayo sisi kauli mbiu yetu katika utendaji tunajiita familia ya madini. Kwa pamoja haya yote ambayo yanasifiwa katika Bunge hili ambayo tumeyafanya ni kazi ambayo imefanywa na sisi sote kama timu. Zaidi ya yote kwa kweli tumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye ametupa neema hii ya kuwa watendaji kazi katika Wizara hii kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia hoja zilizoletwa hapa kuna hoja katika vifungu viwili; kifungu cha kwanza ni kazi inayofanywa na Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Taarifa yao imewasilishwa hapa na maoni yao sisi kama Wizara tumeyapokea na uzuri wa Kamati hii inayoongozwa na Mheshimiwa Kitandula na dada yetu Mheshimiwa Sylvia ni kamati mahiri sana na ambayo ushauri wao, maoni yao na mapendekezo yametufikisha hapa tulipofika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wizara hii ni changa imeanza tu hata haijafikisha mwongo mmoja lakini sifa zilizomiminika hapa zinaonesha ni kwa jinsi gani wizara hii iko katika safari njema ya kulipeleka taifa hili kuwa tajiri kutokana na rasilimali madini. Safari bado ni ndefu, Wachina walisema kwamba safari ya maili mia moja huanza nah atua moja. Sisi pia tumeshapiga hiyo hatua moja, na ndiyo maana mapato yamezidi kuongezeka kutoka asilimia nne wizara ilipoanzishwa kwenye pato la taifa mpaka asilimia 9.7 tuliyonayo sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kujibu tu hoja chache za Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia kwenye Wizara hii na wale wote ambao wamechangia ambao muda hautaruhusu tuweze kutoa mrejesho hapa; Wizara yetu iko makini katika kutoa mrejesho wa maandishi pia Waziri wangu atapitia baadhi ya hoja zao. Kwa hawa wachache ambao nitawatamka waelewe tu kwamba hoja za wote zimechukuliwa kwa umakini mkubwa na zitatolewa maelezo ya kina kimaandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja moja ambayo Mheshimiwa Omary Mohamed Kigua aliileta hapa kwenye mchango wake jana, akishauri kwamba Wizara ya Madini iangaliwe kuhusu haki ya mwenye leseni na mwenye haki juu ya ardhi. Nipende tu kumjulisha kwamba katika Sheria yetu ya Madini Sura ya 123 Kifungu cha 95 mpaka 97 imeweka bayana haki za kila mmoja. Mwenye ardhi ana haki ya kutathminiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mdhamini Mkuu wa Serikali chini ya Wizara ya Ardhi na kupewa fidia apishe eneo. Pia kuna utaratibu wa maridhiano kati ya aliyepewa haki leseni ya madini na mwenye haki juu ya ardhi. Wakiridhiana kwamba atapewa fungu fulani au asilimia kidogo wanaweza wakaendelea, kwa hiyo hakuna mtu anayepoteza haki yake kwa msingi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo la utoaji wa leseni ambalo pia alikuwa anasema kwamba kuna leseni zinatolewa halafu barabara inapita mahala halafu kunakuwa na migogoro ambayo inaonekana kwamba leseni zetu zinakwaza uwekaji wa miundombinu ya barabara. Na kwa hili nipende tu kumwakikishia ya kwamba hili si tatizo, sheria zipo. Barabara inapopita sehemu yenye madini kuna utaratibu mzima na umeshatumika wa kumfidia mwenye eneo lenye madini barabara iweze kupita. Kwa hiyo hilo pia lina maelezo yanayoeleweka na sahihi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Bryceson Tumaini Magessa katika mchango wake jana aliongelea suala la asilimia ya fedha ya maendeleo iliyotolewa katika Wizara yetu mwaka huu, hasa STAMICO, kuwa imeshuka. Nipende tu kumjulisha kwamba fedha za maendeleo kwenye sekta ya madini zinatengwa kulingana na miradi iliyoainishwa. Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 kulikuwa na fedha nyingi ya miradi ya maendeleo ambayo ilikuwa bado haijatolewa, na sasa hivi zimetolewa miradi inaendelea. Hivyo ilioongezewa kwa mwaka huu wa 2024 ni hela ambayo itaenda kuendeleza miradi yote iliyokusudiwa kwa taasisi ya STAMICO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja yake nyingine alikuwa anaelezea kwamba iainishwe kwamba STAMICO inapenda kugawa mitambo ambayo inaagizwa kwa fedha hizi za maendeleo, kwamba inaenda kugawiwa kwa usawa katika nchi nzima. Nipende tu kumwakikishia Mheshimiwa Mbunge kuna mitambo mitano ambayo ilishaagizwa kwa fedha za mwaka huu na kuna mitambo ambayo imewekwa kwenye fedha tunazoomba Bunge lako Tukufu lipitishe leo hapa. Mitambo hiyo itagawiwa kwa usawa kulingana na mahitaji ya kila eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambapo mitambo hii mahususi kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo itakwenda kusaidia kufanya utafiti kwa bei nafuu na kwa masharti nafuu na ili wachimbaji wetu waache uchimbaji wa kubahatisha wa ramli bali wachimbe katika maeneo ambayo taarifa sahihi za kijiolojia zimeshapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda ni mfupi na hoja zingine Waziri wangu atakuja kuzipitia…

MWENYEKITI: Kimsingi muda wako umekwisha, lakini unaweza ukahitimisha hoja yako.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende basi kuhitimisha hoja hii kwa kuendelea tu kusisitiza kwamba, sisi kama Wizara ya Madini chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Doto Biteko, Waziri wetu tumejizatiti kuhakikisha kwamba maono ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ya kutamani kuona sekta hii ikikua na kuwa moja ya sekta zinazozalisha rasilimali fedha za kuleta maendeleo katika nchi hii, zinakwenda kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu tumepanua uwanda wa uwekezaji kutoka madini yale tunasema traditional, yale ambayo yamezoeleka kama dhahabu na vitu kama alivyosema Profesa Muhongo, kwenda kwenye madini ya kimkakati ambayo wote ni mashuhuda wameona mikataba mikubwa mitatu iliyosainiwa mwezi huu wa Nne na Wawekezaji wa Madini ya Mkakati na Madini adimu ambayo uwekezaji wake ulikuwa ni zaidi ya dola milioni 667, huo ni uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu kwenye mitandao nimalizie, walikuwa wanadhani Tanzania imepigika kwa sababu ya kukubali kuuza migodi yenye madini ya thamani kubwa kwa dola milioni 667. Ile ni gharama tu ya kuwekeza, miradi ile ambayo mingine ina miaka mpaka 18 mpaka 20 katika uwekezaji thamani yake ya mapato yatakayoingia katika Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni thamani kubwa mno ambayo hata makadirio yake bado hayajaweza kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila aina ya madini yatakayogundulika kama Profesa alikuwa anasema mnajua aina 17 za rare earth element ambazo pengine mmepewa tu leseni bila kujua kuna madini gani au mtapata nini, ndiyo tunajua. Tunajua madini hayo yote na ile Mikataba asilimia kumi na sita ya Serikali ni asilimia ambayo imetengwa na inasimamiwa kupitia kampuni tanzu ambayo Serikali na wawekezaji wanaweka. Kila aina ya madini yanayopatikana kwa sababu bodi zipo zinazosimamia, zinathaminiwa na Serikali inakwenda kupata haki yake na Watanzania wanaendelea kuneemeka kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru kwa kunipa nafasi na niahidi tu kwamba sisi tutaendelea kufanyia kazi maoni yote na ushauri uliotolewa na Bunge lako Tukufu na niwaombe kwa moyo mmoja na kwa dhati wakubali kutupitishia bajeti yetu, tuweze kupiga kazi ambayo Mama Samia ametuamini na ametupa dhamana tuifanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.