Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Hassan Zidadu Kungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mimi kwa kunipa nafasi leo kuchangia Mpango huu wa Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoweza kuisimamia Serikali vizuri na maendeleo yanakimbia kweli kweli. Pili nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii ya Madini pamoja na Naibu wake na watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu kwanza kabisa mimi naomba uelekee kwenye eneo moja, ambalo Serikali kwa sasa imeweka zuio ama inaweka zuio la matumizi ya kemikali aina ya mercury ama zebaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaweka zuio la kutumia mercury na badala yake wanataka kuruhusu matumizi ya kemikali aina ya cyanide ndiyo itumike mbdala wa zebaki. Sasa mimi naomba niishauri Serikali kupitia Wizara ya Madini; na niliwahi kuuliza swali hapa namna ya usalama wa watumiaji wa kemikali ile ya cyanide usalama wao utakuwaje, na nilijibiwa na Wizara ya Afya badala ya kujibiwa na Wizara ya Madini. Kwa sababu, matumizi makubwa ya Mercury yanatumiwa na wachimbaji wadogo wadogo si Wizara ya Afya, si na watabibu; watabibu ni asilimia ndogo sana; lakini kwa upande wa wachimbaji wanategemea sana matumizi ya mercury, tena hasa wachimbaji wa dhahabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachomaanisha mimi ni kwamba kemikali aina ya cyanide ni hatari sana kwa matumizi ya binadamu. Kwanza kabisa namna ya upatikanaji wake ni gharama kubwa mno kuipata, kwa sababu ili uweze kuagiza lazima uwe na kibali maalum na kibali kile unalipia fedha nyingi kweli kweli ambapo mchimbaji mdogo hawezi kumudu hiyo gharama ya kulipia hicho kibali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni namna ya kuweza kuitumia ama kui-handle inahitaji utaalam wa kutosha mno. Ndipo najiuliza, je, Serikali imetoa elimu kwa kiasi gani kwa wachimbaji wadogo wadogo ili kuweza kuitumia ile kemikali hatari ili isiweze kuleta madhara? Kwa sababu ukiangalia madhara ya mercury na madhara ya cyanide, mercury ina madhara madogo sana, katika asilimia 100 labda ni asilimia 10 tu lakini cyanide madhara yake ni makubwa mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu cyanide ni hatari; kwa nini nasema hivyo? kama mtu yoyote anaweza kuweka kijiko kimoja cha cyanide kwenye maji ama kwenye mto wa maji ambayo yanatiririka basi maji yale mtu yeyote atakayeweza kuoga, akitoka hapo anakuwa ni mwekundu si mweupe tena, hata kama akiwa mweusi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama bahati mbaya tone moja la maji lenye cyanide binadamu yoyote akaliweka mdomoni basi huyo tunamzika kwa dakika mbili tu, madhara yake ni hatari kweli kweli kuliko mercury. Mercury tumeitumia kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mchimbaji, nafahamu na nimeitumia sana mercury. Mercury tumeitumia kwa muda mrefu sana, kwa miaka mingi, tunaona madhara yake ni machache na ni madogo sana kuliko cyanide. Lakini achilia mbali ya mdhara yanayopatikana ni kwamba sasa upatikanaji wa hiyo cyanide ni mgumu na ni mdogo ukilinganisha; wachimbaji wadogo wadogo wametapakaa Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiidhinisha matumizi ya cyanide maana yake watakaokuwa na uwezo wa kuleta ile cyanide na kuitumia ni kampuni kubwa tu. Yaani tunazungumiza Barrick Geita huko na maeneo mengine. Lakini Ukienda kule Tunduru, Ruangwa na maeneo mengine hawana uwezo wa kuagiza cyanide na kuitumia. Lakini hasa zaidi wachimbaji hawa hawana kabisa elimu ya hiyo kemikali ya cyanide.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: …Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili nataka kuzungumzia suala la…

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi, Mheshimiwa Matiko, taarifa.

TAARIFA

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nataka nimpe taarifa mzungumzaji ameeleza vyema kwamba cyanide ni gharama kubwa lakini pia ina madhara. Lakini mercury ameeleza ina madhara kidogo kulinganisha na cyanide, lakini kwa sasa hivi inavyosemekana na nilishauliza swali hapa Bungeni bado wachimbaji wadogo wadogo wanaona mercury ni bei ghali zaidi. Pia inasemekana wanatumia mbolea, hizi mbolea ambazo tunatumia kwenye kilimo wanazitumia sasa hivi kusafishia madini. Nataka nimpe taarifa anavyochangia aendelee kuishauri Serikali wafanye tafiti ya kina kama kweli mbolea zinaweza kutumika na tukajua hazina madhara ziweze kutumika kwenye madini pia tuachane na cyanide.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kungu unapokea taarifa.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa lakini kwa maelezo yafuatayo. Nilipokuwa nasema zebaki kwa maana ya mercury gharama yake ni ndogo yaani mchimbaji anao uwezo wa kununua mercury kwa shilingi 10,000 tena mpaka shilingi 5,000 akaenda kukamatisha dhahabu yake na ina uwezo wa kukamata 0.1 ikashika kulikoni na cyanide. Sasa cyanide kuinunua kibali tu peke yake si chini ya milioni 30 ni kibali tu hapo, hujainunua bado. Sasa najiuliza hawa wachimbaji wadogo wadogo watawezaje kumudu gharama za cyanide? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nashauri…

MHE. HUSSEIN NASSOR AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi, Mheshimiwa Hussein Amar.

TAARIFA

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mchangiaji anapozungumzia kwamba madhara ya cyanide pamoja na mercury kwamba mercury haina madhara. Mercury ina madhara makubwa na matumizi ya mercury na cyanide ni vitu viwili tofauti. Cyanide inatumika kwenye makinikia lakini mercury kwenye unga fresh. Lazima aeleze vizuri asilete tishio la kusema kwamba cyanide ni mbaya, cyanide tunaitumia na mimi nimeshaitumia zaidi ya miaka ishirini, nipo kwenye hiyo fani.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kungu unapokea taarifa.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hii taarifa lakini nadhani mtoa taarifa hajanielewa vizuri nini namaanisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napozungumzia madhara makubwa kati ya zebaki na cyanide lazima nieleweke. Cyanide kwanza utunzaji wake ni wa hali ya gharama kubwa ukilinganisha na mercury. Mercury hata mimi leo naweza nikawa nayo hapa nikakaa nayo nikaenda nayo popote bila shida yoyote lakini cyanide siwezi hata kuigusa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wale ambao wanaitumia, wanatumia kwa vifaa maalum, tena kwa uangalizi mkubwa, watu wa usalama lazima wawepo. Sasa, je, yule mchimbaji ambaye hayuko kwenye kampuni atawezaje kutafuta dhahabu yake ya point mbili, tatu na atapataje uwezo wa kuipata hiyo cyanide. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima …

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. MWITA. M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kungu utaendelea kuchangia mpaka leo Spika atakapotoa maelekezo mengine.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba niendelee na mchango wangu. Mimi nimeona matumizi ya cyanide na mimi nimetumia mercury kwa muda mrefu sana. Leo hii unaweza kuweka mercury ndani ya ndoo ya maji ya kuoga kwa bahati mbaya ukaoga na usipate madhara, lakini leo hii ukiweka tone moja tu la cyanide kwenye ndoo ya kuoga hata ukitumbukiza tu mkono usioge mwili mzima mkono huo unakuwa sio mkono wako tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ninachomaanisha? Nachomaanisha ni kwamba kabla ya kuidhinisha matumizi haya cyanide Serikali kwanza iende ikatoe elimu ya kutosha, kwa wachimbaji wadogo wadogo waelewe namna ya kuitumia, waelewe madhara yake, pia waelewe namna ya kujikinga na madhara yatakayotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara ya cyanide ni hatari tena kwa muda mfupi sana. Naomba nihame eneo hilo niende…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)