Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi lakini vile vile nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata hii nafasi ya kuchangia saa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa leo ni siku ya Mwanamke wa Bunge naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Spika wetu wa Bunge ambaye ni mwanamke namba moja kwa kazi nzuri sana ambazo amekuwa akizifanya hapa Bungeni, lakini vile vile hata katika Jimbo lake hata kwa tuzo nyingi ambazo amekuwa akizipata kwa kweli anastahili. Tunampongeza sana sana sisi wanawake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pongezi zangu nyingi sana kwa Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kwa kweli Wizara hii ya ameitendea haki. Ameitendea haki kwa sababu amekumbuka hata wanawake wachimba madini. Tunamshukuru pia tumeweza kutembelea wanawake wengi sana wachimba madini, wengi wanamshukuru. Kuna fursa nyingi sana sasa hivi wana hamu hata ya kuchimba madini kwa ajili yake. Mwenyezi Mungu ambariki sana Doto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumpongeze Naibu Waziri Dkt. Kiruswa na yeye amekuwa msaada sana katika hii Wizara na kuhakikisha kwamba inakwenda vizuri. Nimpongeze pia Katibu Mkuu wa Wizara kaka yetu Heri anafanya kazi nzuri sana pamoja na watendaji wote wa Wizara hii ya Madini niombe wachukue, niwapongeze pia Kamati ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kupongeza Wizara hii kwanza kwa kuweza kuongeza pato la Taifa kutoka walikuwa wana 7.8% mwaka 1921 na sasa hivi wamefikisha point tisa point saba mwaka 2022. Mheshimiwa Rais wetu aliwawekea lengo kwamba wafikishe angalau 10% na unaona sasa hivi wana 0.3% tu na ninaimani kabisa kutokana na kazi yao nzuri watavuka lengo kwa hiyo, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Iringa pia na sisi tuna Mgodi unaitwa Nyakavangala. Huu Mgodi uko katika Jimbo la Isimani nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja Nyakavangala tulipouliza maswali hapa Bungeni na ukakutana na wawekezaji wa Nyakavangala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakushukuru kwamba ulikuja kuona kulikuwa kuna changamoto nyingi sana na bado zipo vilevile. Ulikuwa umeagiza GST wawasaidie ule mgodi lakini toka ulivyotoka bado hawajaenda kufanya kitu chochote. Kwa hiyo, tunakuomba endelea kuwahimiza waende ili hawa GST wakasaidie huu mgodi na sisi tuweze kupata wawekezaji pia lakini waweze kupatiwa fedha ili nasisi tuwe kama, tupate wawekezaji kama GGM ili na sisi Wanairinga tuweze kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Iringa wapo wachimbaji wadogo wadogo. Kwa mfano Mwenyekiti kule kwake kule Mufindi wananchi wanachimba wadogo wadogo lakini hawajapimiwa wanachimba tu bila kujua kwamba wanatakiwa wafanyaje. Kwa hiyo, tunaomba sasa Wizara hii GST waje wapime katika Mkoa wetu wote wa Iringa ili wachimbaji wadogo wajue maeneo halisi ya uchimbaji ili kinamama, vijana, na Wanayalukolo wote wa Iringa waweze pia kujiajiri kupitia madini na pia tuongeze pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana STAMICO, nimpongeze Mtendaji Mkuu wa STAMICO na Bodi nzima kwa sababu STAMICO zamani tulikuwa tunajua ni shirika ambalo linaweza likafa wakati wowote lakini sasa hivi huu uongozi umefanya tunaona STAMICO sasa inafanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona wameweza kubuni miradi ya kupunguza hata uharibifu wa mazingira kwenye migodi nchini lakini pia kuna mradi ule wa kuongeza kipato mkaa wa mawe wameendelea kuingia ubia kazi ya uchorongaji pamoja na GGM na tulishuhudia siku ile tulivyokuja Geita wameingia Mkataba wa karibu shilingi bilioni 52.2 kwa hiyo, ni kazi nzuri sana ambayo wamekuwa wakiifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia STAMICO wamekuwa mara nyingi sana wakiwasaidia watu wenye ulemavu vifaa vya uchimbaji. Tunawapongeza sana. Tunaomba pia hata wako, hawa tunaona watu wenye ulemavu wanaume lakini wako pia watoto wa kike pia wako wana kikundi chao, tunaomba pia muwasaidieni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mara nyingi wamekuwa wakiwasaidia pia hata wanawake wachimbaji. Tunaomba muendelee sasa kulea wanawake wachimbaji nchini kwa sababu wameonyesha mwamko mkubwa sana na muweke kabisa jicho la kipekee ili kuwapatia sasa utaalam maana yake ndiyo vitu ambavyo wanavikosa; utaalam na vifaa vya uchimbaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunashukuru hata Mheshimiwa Waziri alikiri kuwa wanawake wengi ambao wameingia kwenye mambo ya uchimbaji wamekuwa wakilipa vizuri kodi na mapato na kwa uaminifu sana kwa hiyo tunazidi kuwapongeza wanawake wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuwapongeza wanawake wote wachimba madini nchini. Kupitia Chama chao cha TAOMA tumeweza kubaini changamoto nyingi sana baada ya kukutana na chama hiki cha wachimba madini nchini pamoja na wanawake wanaochimba madini. Kwanza kabisa hawana mitaji ya kutosha katika kuweza kuchimba haya madini lakini vilevile tunaona kwamba vifaa, hawana vifaa kabisa vya kuchimbia na uchenjuaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baya zaidi hawakopesheki kabisa kwa sababu hawana dhamana za kuweka. Kwa hiyo sasa naomba sasa mabenki wawakopeshe basi hawa wanawake wachimba madini. Tunawaomba STAMICO kwa sababu wao ni walezi basi watoe dhamana wawadhamini hawa wanawake waweze kukopesheka ili wachime kwa urahisi na waweze kufanya kazi yao vizuri kwa sababu kina mama wengi zamani walikuwa wanakuwa tu mama lishe, hawafanyi kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba tumpongeze Mwanamke mwenzetu ambaye yeye amekuwa mwekezaji wa Mgodi wa GGR pale Geita. Kwa kweli na amekubali pia kuwa mlezi wa wachimbaji wanawake wadogo wadogo nchini Dada yetu Sarah Masasi, tunampongeza sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaomba sasa Wizara iweke mkakati wa kuwasaidia Watanzania waliowekeza katika hizi refinery ili wapate malighafi kwa sababu changamoto pia wamewekeza, wameweka fedha zao nyingi wamekopa benki lakini unakuta malighafi za kwenda kwenye hizi refineries hakuna. Kwa hiyo, kuwepo na mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba malighafi inakwenda pale ili wathaminishe hizi dhahabu kabla hazijapelekwa nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nikushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwashukuru na Wabunge wenzangu wote na pia nishukuru wanawake wote kwa sababu leo ni siku yetu basi tunawashukuru pia Uongozi wa Bunge kwa kuona umuhimu na sisi wanawake tuwe na usiku wetu na Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)