Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii. Nianze kwa kuunga hoja kwa matumaini kwamba Wizara inaenda kubadilika. Ukweli ni kwamba ukisikiliza fedha, unaelezwa mabilioni kama huna uzoefu na hii sekta utaona ni fedha nyingi sana lakini niwaeleze ukweli ni kwamba Sekta ya Madini haijachangia ipasavyo na sababu ni hizi; Sekta ya Madini ingechangia ipasavyo ukuaji wetu wa uchumi unaopaswa kuondoa umaskini lazima ukue kwa asilimia nane mpaka kumi. Narudia tena ukiwa chini ya hapo hata ukifurahiaje hautautoa umaskini. Umaskini wetu lazima upungue utoke kwenye asilimia ishirini na mpaka kumi na tano na inayoweza kutupeleka huko ni sekta ya madini, gesi na vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mwaka toka 1961, miaka 60 iliyofuata mpaka 2021 ukitaka kukubaliana nayoyasema ni kwamba Sekta ya Madini muda mwingi imejishughulisha na utawala wa Sekta ya Madini (Administration of the Mineral Sector) na ndio maana madini yanayochimbwa ni hayo hayo yaani dhahabu, almasi, na vito hasa Tanzanite na rubi. Ndio maana ya Liganga na Mchuchuma nitayaongea siku nyingine, wasingeshughulika na mambo ya utawala sana Chuma ya Liganga toka miaka ya 60 tungeshachimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa uchumi wa dunia ya leo msemaji mmoja ameongea vizuri sana sijui kama walimuelewa Profesa Mkumbo ameongea vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa leo wa dunia whether wewe ni m-socialist, m–Marxist kwanza ni vitu vimepitwa na wakati havijadiliwi sasa hivi. Uchumi wa dunia sasa hivi unaoongoza ni wa aina mbili, ni private wealth yaani capitalism ya ubinafsi ambayo ndio nchi za magharibi na uchumi mwingine ambao umekuja kuibuka kwa nguvu sana ni state capitalism, nadhani ndio Profesa Mkumbo alikua anaongelea hiyo. Hii state capitalism inafanywa China imefanikiwa, India imefanikiwa, Brazili imefanikiwa, Norway inafanikiwa. Brazili ile kampuni ya PetrolBras ni ya Serikali, Norway kampuni tunayofanya nayo gesi ni ya Serikali hiyo ndio inaitwa state capitalism. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sekta hii ya madini ni lazima itupeleke huko na ndio maana yule nilimsikiliza kwa makini ni lazima iwepo migodi inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la hivyo hatutatoka tutakuwa tunadhani hizo bilioni ni hela nyingi lakini ni ndogo sana. Sasa kuanzia 2023 na kuendelea ndio maana nimesema naunga mkono nadhani tutakuja na hybrid. Tuchanganye hizi kampuni binafsi lakini za Serikali lazima ziwepo. Sasa ina maanisha kwamba Sekta ya Madini kuanzia sasa ijihusishe na uwekezaji, development na kufanya haya tunahitaji taasisi mbili muhimu sana, ya kwanza ni geological survey. Ni ajabu kwamba Tume ya Madini inapewa umuhimu bado ni makosa yale yale ya kushughulika na mambo ya utawala wa madini badala ya kuwekeza geological survey. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa geological survey ni lazima tuwekeze ndio itatueleza tuna madini ya aina gani, kiasi gani ambayo tunataka kuendelea na utawala wa madini lakini geological survey haijawekezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Wizara ya Madini sio lazima ione kwamba hii ni Wizara ya Elimu. Huko zamani tulivyokuwa chuo kikuu sisi, tulikuwa tunafanya kazi na geological survey kwa sababu ukitaka wataalam wengi wapo UDOM, wako Chuo Kikuu Dar es Salaam. Maabara zile lazima ziwezeshwe, haya madini mapya tunayoyaingia haya ninavyoelewa hatuna maabara zinazoweza kutusaidia hapa nchini. Kwa hiyo, mtaendelea kupokea ripoti kutoka nje ambazo nyie hamuwezi kuthibitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna mapungufu makubwa sana na ndio maana tunaanzisha sheria hata hazijatumika tunakuja tunazibadili. Sheria moja ambayo ina mapungufu sana lakini mtu anaweza kushangilia akaifurahia ni hii mpya inayosema tunapata hisa asilimia 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wanaonisikiliza hili ni kosa kubwa tunalolifanya. Asilimia 16 hiyo tunaweza tusipate kitu kwa sababu moja hivi. Hatuko kwenye bodi inayofanya maamuzi, kwenye menejimenti ya juu haupo, haujui unazalisha kiasi gani, haujui unauza kiasi gani, wewe umekaa pembeni unasubiri tu uletewe fedha eti una hisa asilimia 16. Maana ya kuwa mwanahisa ni kwamba ni lazima ushirikiane na mwenzako kuwekeza, kwenye faida mshirikiane na lazima mshirikiane nae kwenye hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa cha kujifunza Watanzania na naomba hii Wizara iende pale Mwadui, mwingine alitaja Mwadui ichukue ripoti ya Marehemu Ally Nuhu Kassim. Kassim alikuwa anafanya kazi nchi za nje akaomba nafasi amepata cheo kwenye UN lakini mwalimu akamrudisha mwaka 69 akampeleka pale Mwadui. Msomi mzuri wa Uingereza akamwambia hebu tunataka kutaifisha hebu angalia Mwadui inavyokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alitoa ripoti ambayo kwa kifupi inasema kwamba hawaelewi nini kilikuwa kinaendelea pale Mwadui. Watanzania hawaelewi, kwa hiyo, Mwadui tulianza na shares 50 kwa 50. Tumekwenda De Beers ilivyokuja kuchukua, De Beers ikachukua 50 kwa 50 wakasema wanajenga plant mpya nzuri ya kisasa Tanzania, mwenzetu changia hela, sisi hatuna tutaelewana huko huko. Wewe leta tu plant wakasema sawa wakaleta plant shares zetu zikashuka kutoka 50 zikabaki 25. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui kama Mwadui kama Tanzania kama bado ina share kama Serikali. Kwa hiyo, hii asilimia 16 ndugu zangu Waheshimiwa nawaambia ni kosa ambalo lazima tulirekebishe kwa sababu hatuna nazo control. Huenda hata tusipate kitu, au tukipata inakuwa kidogo sana. Kingine ambacho tunahitaji umakini mkubwa na Wizara ifanye ni madini mapya na leseni wanazotoa. Nitawatolea mfano hapa, leseni zimeshatolewa za PGM (Platinum Group Metals). Je, tunajua huko wanaenda kuchimba nini? Maana yake PGM hii group ina madini kama saba na yote yana thamani ndio kuna platinum, kuna palladium kuna nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nawapa mfano mmoja hapa kwenye hii group, kuna madini yanaitwa rhodium, wakati dhahabu ilikuwa ni dola 1,850 kwa ounce, rhodium ilikuwa ni dola 10,300 kwa ounce. Je, sisi tunajua hawa tuliowapa leseni watayachimba hayo? Unakuja kwenye rare earth elements wanasema madini ya mkakati, je ni ya mkakati kwako au ni ya mkakati kwa wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii rare earth element kama mtu haielewi anaiongea tu kwa mzaha mzaha ni madini 17, element 17 ziko kwenye hii group na zote zina thamani kubwa ndio hayo Marekani wanaita ya kimkakati, Ujerumani, Japan. Sasa katika haya madini yapo matatu makubwa kabisa, lutetium, lanthanum, scandium. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue moja nieleze, lutetium inatumika kwenye X-Ray hata kwenye treatment ya kansa. Treatment ya kansa ikiwa na haya madini ambayo yanaitwa 177 PSMA, kozi moja ni dola 10,000 na treatment inataka kozi moja mpaka nne. Kwa hiyo, ni between 30 and 40 thousand US Dollars. Ndio maana wanasema haya madini ukitaka kuyanunua unaweza ukaingia kwenye mabilioni ya dola. Je, leseni tunazozitoa za rare earth elements tunajua ni madini gani tumewaambia wachimbe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana badala ya kuwekeza hela nyingi sana kwenye Tume, mimi ningewekeza geological survey na kwenye taasisi zetu za geology. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna madini mengine la mfano ni scandium inatumika kwenye aerospace, kwenye mid fighters hasa za Warusi hata wanaocheza golf wanaitumia hii. Yenyewe kilogram moja ni dola 3,912 na duniani kwa mwaka zinahitajika tani kati ya 15 na 20 tons mwaka mzima. Haya yako kweye rare earth elements. Je, tunajua leseni tunazozitoa? Je, tunajua hiyo 16% tuliyopewa ya bure tunaijua? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije topic nyingine ambayo nimeiongelea kwa muda leo naichukua kwa njia nyingine na ninashukuru Wabunge nao wameongelea suala la kuwa na reserve ya dhahabu (gold reserve). Niliongea leo sitarudia ila nachukua angle nyingine ya kuwapa taarifa wale ambao bado wanasita sita kwamba kwa nini unahitaji kuwa na gold reserve? Kwa hiyo, nimeenda kwa wale wanaotukopesha, nimeenda kwenye World Bank nikaangalia hisa za World Bank ambazo zinaendana na voting powers. Yaani unavyozidi kuwa na hisa nyingi ndivyo ambavyo kura yako inazidi kuwa nzito. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo World Bank nimechukua tatu. Marekani voting powers za Marekani ni around 17%. Japan ni around 8.55%. China ni 2.25%. Sasa angalia Marekani mwenye voting power kubwa kwenye World Bank ana dhahabu reserve tani 8,133 tons gold reserve. Huyu Japan anayo vote kwenye hii IDA (International Development Association) World Bank ina mikopo ya aina mbili. Hii IDA ndiyo yetu ya sisi masikini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko huyu Japan yeye voting powers zake 8.55% ana reserve kwenye Benki yake ya Taifa tani 846. China ana voting power ya 2.25% ana reserve ya dhahabu tani 1,948. Wewe Tanzania kwa nini bado una sita? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Madini na Benki Kuu kwa nini bado mnasita? (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Professor.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia sasa. Nimalizie kwa kusema kwamba lazima tuwe na hiyo na kuwa na hiyo ni lazima refineries zetu mbili zifanye kazi. Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba refinery mbili za dhahabu tulizonazo ya Geita inaweza ika- process kilogram 600 kwa siku ya Mwanza 480 kwa siku. Lakini Waheshimiwa Wabunge hizi refineries hazina dhahabu na huenda zitafungwa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)