Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie bajeti hii ya madini kwa mwaka 2023/2024. Nami niungane tu Wabunge wenzangu kuwapongeza Wizara kwa kazi nzuri ambayo wanafanya ya kusimamia sekta hii nyeti ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tunajisifu kwamba tumefanikiwa sana kukusanya mapato kudhibiti wizi katika sekta ya madini bado tunalo jukumu moja kubwa la msingi ambalo hatujalitimiza la kuhakikisha maeneo au watu wanaoishi kwenye maeneo yenye madini wanafanana na thamani ya madini yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nitaliongelea kwa maeneo mawili tu kama maeno ya mfano eneo la kwanza ni eneo la fidia kwa watu ambao wanapisha wawekezaji wa maeneo ya madini. Hawa wananchi ukienda kufanya tathmini ya haraka, kabla hawajapisha maeneo yale walikuwa wana maisha mazuri wakishalipwa fidia ni kweli wanalipwa fedha nyingi lakini miaka kadhaa baada ya kulipwa fidia wale watu wanarudi kwenye ufukara na umaskini uliokithiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri Mheshimiwa Waziri atusaidie kwa sababu mwisho wa siku kumpisha Mwekezaji siyo lazima akulipe fidia peke yake, kwa nini Wizara isitengeneze mipango ya muda mrefu angalau hao watu wanaoishi kwenye maeneo ya madini waweze kupewa hisa nao wawe sehemu ya makampuni hayo ambayo yanawekeza. Jambo hili litawafanya hao watu wawe na pesa za muda mrefu, zitawafanya wawe na Maisha ya muda mrefu, itawafanya hata kama watapoteza fidia kidogo waliyopewa ile awali basi wanaweza kuendelea kuboresha uchumi wao kupitia hisa zile ambazo watakuwa wanalipwa mwaka hadi mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilisisitize ni eneo linaitwa corporate social responsibility. Watu wanaoishi kwenye maeneo ya madini hawafanani, na mimi nimetoka Shinyanga, hawafanani na madini yanayochimbwa, hawafanani na utajiri ambao Mwenyezi Mungu ametujalia. Kwa mfano, ukienda Tarime pale tulienda juzi na Kamati yetu ya TAMISEMI wale watu wamepewa Bilioni Saba hela ya corporate social responsibility ile pesa waliyopewa ukifika pale hauoni matokeo ya Bilioni Saba kuingia katika Halmashauri ya Tarime huioni! Ukiuliza wanasema sisi Halmashauri sheria iko vizuri inaonesha kwamba Halmashauri lazima uishirikishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri inashirikishwa kwa maana ya kuchagua miradi ya kutekelezwa lakini Mkandarasi anayeenda kutekeleza mradi ule anaamuriwa na mgodi, aina ya class ya Mkandarasi na ujenzi wa jengo inaamuriwa na mgodi! Kama Serikali inaweza kujenga madarasa kwa Shilingi Milioni 20 ni kwa nini tumruhusu mgodi alete Mkandarasi ambaye anakuja kujenga shule ya aina ileile kwa gharama ya zaidi ya Milioni 500 kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi…

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Waitara.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Waitara.

TAARIFA

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Salome Makamba kwamba anaendelea kuchangia vizuri lakini pia mimi ni Mjumbe mwenzake wa Kamati ya TAMISEMI, nadhani amechanganya maelezo Jimbo la Tarime Vijijini ambalo mimi ndiye Mbunge wake na Halmashauri tunaongoza, hizo shilingi bilioni 7.3 ambazo zimetolewa sasa hivi, ziko zinazunguka kwenye Kata 26 tunatumia Force Account siyo Mkandarasi kutoka mgodini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichofanyika fedha ambazo zilitolewa mwaka 2019/2020 wakati ule sikuwa Mbunge wala hatukuwa tunaongoza Halmashauri, shilingi bilioni 5.7 ndiyo ambazo alikuwa analipa Mkandarasi na miradi ina viporo mpaka leo, hilo ndilo ambalo lilielezwa kwa Kamati hiyo. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome Makamba unapokea taarifa?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona jamaa anadhani tunafanya kampeni hapa. Wamemsikia watu wa Tarime nashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa inayotolewa ya CSR sheria iko wazi Mheshimiwa Waziri tusaidie, Mkandarasi aamuliwe na Halmashauri na Force Account ndiyo iamue nani ajenge, nani alipwe, wakati gani na mradi gani utekelezwe ambao utaacha alama kwenye maeneo ambayo yana madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye suala la mikopo ya wachimbaji. Mheshimiwa Waziri mimi niliwahi kuchangia hapa nikakuomba sana uwasaidie wachimbaji wadogo wapate mikopo kwa sababu na wale wanafanya uwekezaji na wanachangia kwenye nchi hii. Mheshimiwa Waziri uliniahidi na kweli umeenda kuwapelekea mikopo, sasa mikopo uliyowapelekea Mheshimiwa hizo benki ulizowapelekea zinazotoa mikopo wanataka hati za nyumba, hizo benki wanaopelekewa mikopo riba zao ni za kibiashara, marejesho yao ni kwa mwezi, bado mazingira ni magumu sana kwa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Serikali inalo fungu la pesa kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji wadogo, Serikali inakusanya pesa kupitia wachimbaji wadogo, ni kwa nini Serikali isitenge ruzuku kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji ili mwisho wa siku na wao waweze kuchangia katika Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema leo tunaenda kuwatoza, hawa wachimbaji wadogo tozo nyingi wanazotozwa wanatozwa katika mitaji yao, uwekezaji katika sekta ya uchimbaji mdogomdogo mtu anaweza akawekeza mpaka mwaka mpaka miezi miaka miwili lakini kodi analazimishwa kulipa kila mwezi, na Halmashauri kila siku inatunga sheria, utasikia sijua Afisa Biashara anataka kodi, Afisa Mazingira anataka kodi, mlundikano wa kodi ni mkubwa sana. Tusiwape mikopo ya kibiashara wachimbaji wadogo hatuwasaidii, tunawanyonya ndiyo maana watu wanaishia kukwama huku wanatelekeza famila zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye masuala ya mabwawa ya matope na mabwawa ya sumu. Nchi hii ilichafuka sana kipindi cha nyuma kule kwenye Mgodi wa Barrick wa Nyamongo, bwawa lilipasuka la sumu na watu wakapata madhara, tukapelekwa Mahakamani tukashitakiwa na nini na hekaheka zikawa nyingi sana. Juzi pale Mwadui bwawa la tope limepasuka pia, tunamshukuru Mungu madhara hayakuwa makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ningeomba nipendekeze Serikali ifanye tathmini ya haya mabwawa mara kwa mara, kwa maana ya kwamba iwe angalau kila baada ya Miezi Sita Serikali ipite ifanye tathmini ili kuhakikisha kwamba mabwawa haya ni salama kwa maisha ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali inapokuja kujibu inipe majibu, maana mimi ni Mbunge ninatokea Shinyanga lakini sijaipata ripoti ya tathmini ya madhara ya kupasuka kwa bwawa la tope la Mwadui, ninataka nijue ushiriki wa Serikali katika kufanya tathmini, ushiriki wa Serikali katika kutoa fidia na kuwarejesha wale watu katika maisha yao bora kuliko walivyokuwa zamani. Kwa sababu lile bwawa lilipasuka tope lilifunika nyumba, mali zilipotea, sasa nataka nijue nini ilikuwa ushiriki wa Serikali katika kudhibiti kupasuka kwa bwawa la tope la Mwadui na compensation waliyopewa wale watu, tathmini ilifanyikaje ningetamani sana kupata majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa yote naendelea kusisitiza kwa Mheshimiwa Waziri anakusanya mapato, anachangia kwenye bajeti ya Serikali lakini na sisi wananchi kutoka kwenye maeneo ya uchimbaji, tunataka tufanane na rasilimali zilizoko katika maeneo yetu, fidia peke yake haitoshi tunataka tulipwe fidia lakini tuwe sehemu ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana leo mwekezaji anajenga shule anajenga vituo vya afya mwisho wa siku watu wana vandalize kwa sababu mtu anaona hiki ni kituo cha afya cha mwekezaji, hiki ni kituo cha afya cha mgodi, lakini kama mimi mwananchi ninayetoka Shinyanga ninayetoka Kakola ninayetoka Mwadui nitaona kwamba huu mgodi ni sehemu ya mimi na unaninufaisha lazima nilinde rasilimali zote ambazo zinajengwa na mgodi, lazima nilinde mali zote ambazo tunajenga mimi pamoja na mgodi nikiwa kama sehemu ya uwekezaji wa mwekezaji huyo. Baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)