Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji kwenye hotuba hii. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai wa kuweza kusimama kwenye Bunge lako Tukufu leo na kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya madini kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli kazi yake tumeiona akisaidiana na Naibu wake, lakini hata watumishi wengine wakiongozwa na Katibu Mkuu kwenye idara hii wanafanya vizuri, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze na hawa jamaa wanaitwa GST. Nashukuru sana Waziri aliwaleta vijana wake wakaja pale Mpigamiti, wamekaa mwezi mzima. Pamoja na kazi nzuri waliyoifanya ya utafiti wa madini pale Mpigamiti wametuachia uchumi vile vile na wajomba tunao pale. Kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba wale vijana watarudi pale kuja kusalimia wajomba zetu wale. Kwa hiyo, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jambo hili naomba niseme kidogo. Pamoja na utafiti ule, lakini matokeo yale ya utafiti yamebaki kuwa kwenye Ofisi zao. Sisi watu wa Liwale hata Madiwani kushirikishwa wakafahamu matokeo ya utafiti ule hayajaachwa pale. Kwa hiyo, nini kinachotokea? Kinachotokea kwa sababu wamekwisha ingiza kwenye mambo yao ya mitandao huko, tayari tumekwisha anza kupokea wageni kutoka kwenye mikoa mbalimbali wakija kuchukua vitalu pale kwa ajili ya uwekezaji wa madini, lakini wenyeji wa pale hatuna habari yoyote. Matokeo yake ni nini? Matokeo yake sasa sisi tutakuwa wasindikizaji badala ya kuwa sisi washiriki kwenye shughuli hiyo ya uchimbaji wa madini. Ukizingatia sisi Mkoa wa Lindi tasnia hii ya madini ni ngeni kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa ni vizuri baada ya utafiti ule kukamilika, basi wangewaacha wale vijana wakaja kutupatia matokeo, angalau kuongea na Madiwani, kuongea na Viongozi wa Vijiji kwamba jamani kwenye utafiti wetu kwenye hii wilaya yenu tumekuta hiki na hiki, ili na sisi tuweze kuwa ni miongoni mwa watu wanaoshiriki katika huu uchimbaji wa madini hasa wale wachimbaji wadogo wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, pamoja na matokeo hayo ya kuonesha kwamba Liwale kuna madini ya aina mbalimbali, sasa hivi kule kuna wachimbaji wadogo wadogo wameanza kuchimba dhahabu, lakini vile vile kuna wawekezaji wameanza kuchukua vitalu, Kuna nickel pale na graphite, madini haya yote yamekwisha onekana kwamba kwa ukanda ule wa Liwale ni mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha ni kwamba mpaka leo hii wale wachimbaji wetu wadogo wanapata shida sana kwa sababu hatuna soko. Liwale hakuna duka la uuzaji wa madini, matokeo yake vijana wale, wachimbaji wadogo wanalazimika kusafiri kutoka Liwale kwenda Tunduru ama kwenda Ruangwa, jambo ambalo linaleta usumbufu kidogo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, ili kuonekana kama kweli ile kazi waliofanya wale watu wa GST ina manufaa kwa watu wa Liwale, basi watufungulie duka ili vijana wale waendelee kufanya uchimbaji ule na kupata fedha pale pale Liwale Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hata kwenye ile Idara yenyewe ya Madini, pale hatuna Mtumishi hata mmoja. Kwa hiyo, unapopata jambo fulani linalohitaji ufafanuzi au umepata jiwe fulani huna hata mahali pa kwenda kuuliza kwamba hii ni madini ya aina gani na thamani yake ni nini? Matokeo yake watu wengine wanaibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri mwaka 2022, kuna jamaa mmoja ameokota jiwe pale amekwenda mpaka Tunduru. Alipofika Tunduru akalala, asubuhi akaonana na tajiri akampa milioni 10 akasema chukua hii milioni 10m kesho uje tufanye biashara. Yule alipopata ile milioni 10 akaishia mitini, akijua kwamba hawa jamaa wanataka kunitapeli, wataninyang’anya hii milioni 10, kumbe madini yale yalikuwa na thamani kubwa sana. Kwa hiyo alipoteza kwa sababu ya kukosa hiyo elimu. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, ahakikishe Liwale tunapata duka la uuzaji wa madini, lakini vile vile tunaomba tupate mtaalam ambaye atakaa pale Liwale kwa ajili ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukiangalia umbali kutoka Liwale kwenda Nachingwea ni zaidi ya kilomita 120 na kutoka Liwale kwenda Tunduru ni umbali wa zaidi ya kilomita 200. Kwa hiyo mara nyingi wale wachimbaji wetu wadogo wanaibiwa njiani, wanatekwa na wanafanyiwa mambo mabaya. Kwa hiyo, niombe sana jambo hili lichukuliwe kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hivyo tu ninapozungumzia kuwapa elimu Madiwani wetu ni kwa sababu nasikia kwenye hayo machimbo ya madini kuna kitu kinaitwa CSR, sisi Liwale tunachinba madini sasa hivi ni mwaka wa tano kama sio wa sita, lakini Halmashauri haijawahi kupata hata thumni na wala haijui tunapataje fedha kutokana na ule uchimbaji mdogo wa madini. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, nimeomba dakika tano hizi nizungumze ili hili jambo lifike na naomba alitilie mkazo sana na elimu kwa wachimbaji wadogo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho kabisa, kama nilivyosema baada ya kugundulika kuwa kuna madini, vitabu vimeoneshwa watu wa Liwale hawana taarifa, lakini kwenye vitalu wameandika vipo na watu tayari wanaingia kwenye tovuti wanaangalia. Sasa hivi vitalu vyote vya Liwale vimekwishachukuliwa na watu. Ukienda pale unakuta kuna madini na una mwekezaji unaambiwa kuna mtu, ukiingia kitalu hiki unaambiwa kuna mtu, lakini hao wawekezaji ambao tayari wamekwishachukua leseni kule wako wapi? Hivi kuna utaratibu gani mtu anachukua kitalu mwaka mzima hajawekeza chochote. Sasa pale kwa mfano, alikuja mwekezaji mmoja kwa wananchi, akasema kwamba yeye eneo lile amekuta kuna madini ya nickel, anataka kuchimba nickel pale, akaja akarubuni rubuni watu, ameondoka sasa hivi ana mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jamaa mwingine amekuja mwaka 2023 kuchukua leseni tukamwambia lile eneo lina mtu tayari, sasa huyu mtu anawacheleweshea wale wanakijiji maendeleo yao pale, kwa sababu yeye hajawekeza, sasa amekuja mwekezaji lakini eneo lina mtu. Kwa hiyo, nimwombe Waziri, sijui taratibu za leseni zikoje, sijui mtu mmoja anatakiwa kumiliki hilo eneo kwa muda gani? Kama kuna uwezekano ombi langu, wale watu ambao wamechukua vitalu muda mrefu na hawajaanza uwekezaji wowote, basi leseni zao zifutwe ili hawa wawekezaji wapya wakija na sisi tuweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo tu. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)