Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Dr. Eliezer Mbuki Feleshi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kushukuru sana kwa nafasi hii, pia nishukuru na kuwapongeza wakuu wa mihimili yetu ya dola, Mheshimiwa Rais, Spika wa Bunge letu pia Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa kusimamia misingi ya demokrasia, haki na utawala bora. Niwapongeze sana Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati, Waheshimiwa Mawaziri na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda huu pia nitumie kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge, ambao wamepata fursa kuchangia hoja, kujibu au kuongelea maeneo ambayo yamefanyiwa wasilisho na Waziri wetu wa Katiba na Sheria ambaye amefanya kazi kubwa sana kwa kushirikiana na Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji ndani ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo hoja kadhaa ambazo zimeibuliwa katika michango hiyo zikiwemo sheria zetu kupitwa na wakati. Katika hili ningeomba tu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, Watanzania wote na watumiaji wote wa sheria, kwa sasa sheria zote ambazo tungependa zitumike ni zile zilizokwishakufanyiwa rekebu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuingizwa kwenye tovuti ya Office of the Attorney General Management of Information System, ambako ukiingia tu unafikia online law catalogue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hizi tumeendelea kuzitangaza kadri tunavyofanya urekebu, na itakapofika mwezi wa sita mwaka huu ningependa kutoa taarifa kwamba Serikali yetu tutatoa toleo la sheria zilizorekebiwa la mwaka 2023, ambako sheria zote kuu 446 zitakuwepo. Ni tendo la kuipongeza Serikali yetu kwa sababu toleo hili linakuja baada ya miaka 20 kupita. Toleo la mwisho la urekebu tulilonalo ni lile la 2002, na tena ambalo Serikali yetu ilipata ufadhili. Kwa hiyo ningependa kuipongeza sana Wizara ya Katiba na Sheria na Serikali yetu kwa ujumla na Bunge hili kwa kuidhinisha fedha ambazo zimewezesha kazi hiyo kubwa sana kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kazi kubwa sasa ambayo tunaendelea nayo pamoja kwa kukamilisha urekebu ni ile ya kufanya tafasiri ya sheria kuu pamoja na sheria ndogo. Tayari tumekwishakuvuka asilimia 50, na katika zile sheria ndogo 29,700 tayari sheria ndogo 211 nazo tumesharekebu. Kwa hiyo fedha iliiyoombwa na Mheshimiwa Waziri wetu ni pamoja na mambo mengine itasukuma sana kufanya hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine vilevile tunashukuru sana maelekezo ya kiti kwa maana ya Mheshimiwa Spika, ambayo yameendana sanjari sana maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria na nina kila sababu ya kumpongeza. Matumizi ya Law Reform Commission, Tume yetu ya Kurekebisha Sheria, kwa sasa Serikali imekwishakuamua kwamba, Tume hii itemize wajibu wake wa msingi wa kufanya utafiti kabla ya sheria hazijaletwa humu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kila mmoja akisimama anasema Bunge liletewe sheria, kwa hiyo kuletewa kwa sheria nyingi tunazotamani ziletwe humu iendane na uwezeshaji mkubwa ambao tunatamani sana ufanyike kwenye Tume yetu ili iweze kutuhakikishia inafanya utafiti kwa kushirikiana na wadau wote na kutuwezesha katika hilo. Kwa hiyo Mheshimiwa Massare nikuhakikishie tu kwamba kwa sheria zile zilizokwishakufanyiwa urekebu makosa yale ya ukinzani yamekwishakufanyiwa kazi. Pia nikuhakikishie kwamba kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Serikali sheria zote zitakazofanyiwa utafiti zikaendelea kutokuwa na makosa mengi sana ya kiufundi au kiuchapishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja pia imewasilishwa kuhusu wananchi ambao wanashinda kesi lakini wanakuwa hawajapata haki yao. Mheshimiwa Mpina ameongelea hili. Ningependa tu kueleza kwamba kwa sheria zetu zinazoongoza mienendo ya madai ni Civil Procedure Act ambako Order XI inaongelea habari ya Executions. Kwa Sheria ya Jinai (Criminal Procedure Act) Kifungu cha 353 kinaongelea namna ya kurejeshwa kwa mali iliyokamatwa kwa mtu aliyekwishakushinda kesi mpaka hatua ya mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kumaliza nafuu zilizo kwenye sheria, kwa mfano kifungu cha 353, basi yule aliyeshinda na kama hajapata haki yake kuna namna ya kuwawajibisha watu wanaotatiza haki hiyo kufanyika kwa mujibu wa sheria na kama ilivyochangiwa vizuri sana na Mheshimiwa Tadayo wakati anatoa mchango wake hapa. Kwa hiyo labda, kwa sababu tuna dhamana ya kuwajibika kwa mujibu wa kazi tulizokwisha kupewa, nafikiri Mheshimiwa Mpina nitaomba kuendelea kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zetu kuona kikwazo ni kipi. Kama ni upungufu wa legal aid kwa wale wanaohusika basi ninaamini wajibu wetu ni kukwamua na kuhakikisha kwamba watu wanaohusika wanaendelea kupata haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amekwishawasilisha kwenye hotuba yake, ofisi yangu kupitia idara zake hasa uandishi wa sheria, itaendelea kutimiza yale ambayo tayari yamewekwa humo. Pia tuendelee kuwaahidi kwamba tutaendelea kuhakikisha kwamba, kile ambacho tumekuwa tukikifanya hata kwa Mbunge mmoja mmoja anapotuletea hoja, tutaendelea kutoa majibu ya haraka na tutaendelea vilevile kufanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Katiba na Sheria; na kwa mambo yote yanayohusu mikataba. Nafikiri hili ni jambo ambalo tutaendelea kulitolea maelezo kadiri ya mikataba inavyojadiliwa, inavyohitimishwa ikiendana na mashauri ambayo yako kwenye mahakama za ndani na za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukichelea wakati mwingine kuongelea kesi iliyomalizika hatua moja lakini bado inaendelea kwenye hatua zingine au kwenye majadiliano mengine ambayo bado yanaendelea kwa mujibu wa sheria. Hoja ya mwisho ya Mheshimiwa Mpina nafikiri alikuwa anaongelea standard charted; jambo hili bado kuna majadiliano ya Serikali yanayoendelea na wale walio na tuzo.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja na Waziri, nakupongeza sana. (Makofi)