Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii nyeti, nianze kwa kusema kabisa kwamba naunga mkono hoja hii ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nipongeze na kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo imefanya kazi kubwa, imefanya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya utoaji haki. Kwetu sisi ambao tulikaa kaa kidogo kwenye hii sekta kwa muda mrefu tunaona kabisa kama ni mapinduzi makubwa kwa sababu ni sekta ambayo ilikuwa kama imesahauliwa, majengo yalikuwa yamechakaa hata karatasi za kuandikia zilikuwa wakati mwingine ni shida unapoingia mahakamani asubuhi lakini kwa hali ilivyo sasa hivi kwa kweli tunashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Mheshimiwa Rais amegundua kabisa kwamba hapo ndiyo mahali ambapo akifanya uwekezaji hata nchi yetu itaheshimika duniani kote kwa sababu ya utoaji haki ulio katika viwango bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia viongozi wa Wizara hii, ndugu yangu na rafiki yangu Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri na Dada yangu Dada Pauline Gekul pamoja na wengine wote ambao ni wadau katika kuongoza sekta hii muhimu ya utoaji haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesisitiza juu ya suala la utoaji elimu. Nadhani hakuna jambo muhimu kama hili kwa sasa na elimu hii iende katika sehemu mbili; kwanza iende kwa wananchi lakini pia iende kwa watumishi katika sekta hii ya utoaji haki. Nikianza na mahakama kwa mfano ni vizuri watu wakaelewa sheria, wananchi wakaelewa sheria wakaelewa na jinsi ya kupata haki zao kwa kutumia sheria lakini pia watumishi wa mahakama wakapata mafunzo ili wananchi wanapokwenda mahakamani waone mahakama kama mahali rafiki, wasione mahakama kama ni mahali ambapo ni pa kuogopwa au ni mahali ambapo ni pa mabavu na kadhalika. Kwa hiyo, elimu ni muhimu katika sekta hizo zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri elimu ingetolewa sawa sawa hata malalamiko kama baadhi ya yaliyoletwa hapa juu ng’ombe waliokamatwa ambao ni suala la kukaza hukumu ya mahakama siyo suala la kuja kwa Waziri Ndumbaro tena. Nafikiri hata hayo tusingepata tabu kwa sababu hukumu ikishapatikana uko utaratibu wa kui-execute wa kuikaza kwa Kiswahili wanasema kwa hiyo hayo yote yanaashiria kwamba tuna changamoto juu ya watu ya kuelewa mfumo jinsi ya kupata haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata suala la katiba mpya for that matter lisipotanguliwa au kwenda sambamba na elimu ya kutosha halitaleta tija yoyote. Tutakuwa na katiba imekaa hapo nzuri, hata kama iliyopo na kama hii ambayo iko hapa sasa hivi ambayo ina haki karibu zote lakini iko kabatini watu hawana uwezo wa kuitumia wala kuweza kupata zile haki zao ambazo ziko ndani ya katiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri mambo machache sana. Nimeona katika ukurasa wa 36 wa ripoti ya kamati imetoa ushauri kwa Tume ya Kurekebisha Sheria juu ya kufanya mambo mbalimbali. Ningependa kuongeza yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametaja pale kwamba Tume ya Kurekebisha Sheria ishauriwe juu ya masuala ya Sheria za Ardhi. Tumejenga mahakama nzuri sana maeneo mengi ikiwa ni pamoja na Jimboni kwangu Mwanga lakini bado ukiwa na suala la ardhi utatakiwa kwenda Baraza la Kata ambalo kazi yake ni kutoa ushauri tu kusuluhisha kama vile masuala ya kusuluhisha ndoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka hapo lazima uende Mahakama ya Ardhi ambayo pale Mwanga haipo. Mahakama za Ardhi ziko chache tena haziko chini ya Judiciary, chini ya mahakama ziko chini ya Wizara ya Ardhi. Kwa hiyo hiyo inaleta changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama iliwezekana kwa Mahakama Kuu kuwa na mamlaka ya kushughulikia mashauri ya ardhi na mashauri mengine ya kawaida sioni kwanini sijapata maelezo ya kutosha kutoka kwa Wizara kwamba ni kwa nini sheria isirekebishwe, mahakama za wilaya na mahakama za mahakimu wakazi zikaweza pia kushughulikia mashauri ya ardhi kama iliwezekana High Court naamini hata huko inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo linahitaji marekebisho ni juu ya hizi Sheria za Mienendo, procedure ambazo nilipata kusema hapa kwamba zinanyima haki sana watu kutokana na procedure zenyewe kuwa mzigo. Kasuala kadogo kanatokea mtu amekamatiwa mizigo yake alikuwa anapeleka sokoni labda ni vitu vya kuharibika nyanya sijui na mihogo lakini kama imekamatwa na mamlaka ya Serikali akitaka kwenda mahakamani lazima atoe notisi ya siku 90. Nyanya zinaharibika ndani ya siku 90 na mihogo inaharibika. Kwa hiyo, analazimika tu kufuata kile anachoambiwa afanye hata kama anaona hakuna haki yake lakini afanye nini hawezi kufuata hiyo procedure ambayo ni mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu hata kwenye mizani pale, mtu amekamatwa kwenye jambo ambalo ana hakika kabisa haki yake ipo lakini saa ngapi aende mahakamani aanze kutoa notisi ya siku 90 wakati mzigo ule ameubeba na fedha ya mkopo benki ambayo mwisho wa mwezi kuna marejesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusipohangaika na hizi Sheria zetu za Mienendo zikarahisisha mienendo kwa baadhi ya mambo hata kwenye zile haki za msingi ambazo ziko ndani ya katiba. Nitoe tu mfano kwa mfano juzi hapa kule Mkoa wa Kilimanjaro wameandamana watu kupinga haya mambo ya ushoga. Nawapongeza wamefanya kitu kizuri sana lakini nafikiria tu kwamba angetokea mtu asiyejua haki za watu akawanyima kibali cha maandamano, wangefanyaje. Wangetakiwa kwenda ku-challenge ile. Sasa ku-challenge unatoa notisi ya siku 90 wakati watu wanaangamia na ushoga uko wapi na wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tufike mahali turekebishe Sheria zetu za Mienendo zirahisishe jinsi ya kupata haki mbalimbali katika maeneo ambayo ni ya muhimu. Asilimia 90 mimi nasema ya haki katika katiba yetu na katika sheria zetu, zipo zinaweza zikapatikana, tatizo ni namna ya kuzipata ule mlolongo wa kuzipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni mfupi tu kwa kumalizia tu imetamkwa hapa Bungeni kwamba Serikali imeshindwa kukusanya fedha zile za Plea Bargaining. Naheshimu sana huo mchango lakini nalazimika kutoa na maoni yangu. Wote tunafahamu kwamba mambo yale ya Plea Bargaining yalifanyika ilikuwa inafanyika na watu ambao wako ndani wako, jela. Mtu ameshakaa miaka miwili na kule hata mawakili, mimi nilikuwa wakili wakati ule, mawakili tulikuwa tunakatazwa kushiriki kwenye ule mchakato. Kwa hiyo, yalikuwa ni mambo ya kulazimisha, yalikuwa ni mambo ya kuumiza watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kipindi hiki ambacho tunataka kurekebisha mambo yaliyotokea nyuma ambayo yalitesa watu sidhani kama kuna haja ya kuanza kufikiria kuanza kuwakamata tena watu katika mambo haya ambayo katika spirit ya maridhiano tulishaona kwamba hayafai. Plea Bargaining maana yake ni bargaining, mnakaa mnapatana kwa hiari kama unaona haifai mnakubalina. Ku-bargain ni kama mnavyo-bargain bei na machinga kule ilimradi maslahi ya pande zote mbili yazingatiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile iliyokuwa inafanyika kama kuwekewa pistol hapa mtu yuko ndani miaka miwili analazimika kuchangiwa kuuza vitu kufanya nini halafu leo hii tumeshapata reliefs sasa tunaanza kuweka mambo sawasawa ili twende mbele, tunaanza kusema kwamba tuanze kukamata tena watu. Nafikiri hii siyo sahihi, ipo haja ndiyo ya kupitia baadhi ya zile kesi lakini nyingi kati ya zile kesi ile Plea Bargaining haikufanyika katika utaratibu ambao unakubalika kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sishauri hilo ambalo mwenzangu ameshauri, mimi naomba kutofautiana naye na kushauri Serikali kwamba utaratibu huo hautafaa. Yale yaliyolipwa bila utaratibu fine yamelipwa, tuangalie utaratibu mwingine lakini…

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)