Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na naomba nianze kwa kutambua na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa ya kuimarisha eneo zima la haki za binadamu, demokrasia pamoja na utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na hayo napenda kufanya rejea kwenye mchango wangu katika bajeti hii ya Wizara Katiba na Sheria ambayo nilitoa mwaka jana Tarehe 28 Aprili, 2022 ambapo nilipendekeza ya kwamba Serikali ilete Bungeni Sheria ya Vyama vya Siasa pamoja na Sheria ya Uchaguzi ili zifanyiwe maboresho kwa lengo zima la kuimarisha ushiriki wa wanawake kwa maana ya usawa wa kijinsia katika siasa lakini pia kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake ndani ya vyama vya siasa na vivyo hivyo kutambua suala zima la ukatili wa kimtandao kwa wanawake wanasiasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Damasi Ndumbaro ambaye aliridhia mapendekezo hayo na akaielekeza Tume ya Kurekebisha Sheria ibebe jukumu hilo na ianze kufanya mapitio ya sheria hizo mbili, nami nilipata fursa ya kukutana na Tume hiyo na kuwasilisha maoni yangu siku ya Tarehe 11 Mei, na naipongeza sana Tume ya Kurekebisha Sheria kwa sababu natambua ya kwamba, mwezi wa Tatu mwaka huu wamewasilisha ripoti ya mapendekezo yao kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hivyo naipongeza sana Kikosi Kazi cha Mheshimiwa Rais waliopewa jukumu la kutoa maoni na mapendekezo kuhusu hali nzima ya masuala ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini, ambao na wao wameshawasilisha ripoti yao kwa Mheshimiwa Rais waliwasilisha mwishoni mwa mwaka jana, nami pia nawashukuru kwa kunipa fursa ya kuwasilisha maoni yangu mbele ya kikosi kazi hicho siku ya Tarehe 14J ulai, 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huu naomba nitumie fursa hii kuishauri na kuiomba Serikali kwamba itakapoleta maboresho ya sheria hapa Bungeni ya Sheria ya Vyama vya Siasa pamoja na Sheria ya Uchaguzi yafuatayo yazingatiwe: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi itakapoletwa iainishe bayana namna ambavyo uteuzi wa wagombea ndani ya Vyama vya Siasa utafanywa na itapendeza sana iwapo sheria hii itakamilika na kuletwa Bungeni kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka kesho 2024. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu, kwa takwimu za sasa ni asilimia 2.1 tu ya Wenyeviti wa Vijiji ambao ni wanawake asilimia 12.8 tu ya Wenyetivi wa Serikali za Mitaa ambao ni wanawake asilimia 6.7 tu ya Wenyeviti wa Vitongoji ni wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni dhahiri kwamba bado ipo haja ya kuongeza idadi ya viongozi wanawake katika hizi nafasi za kisiasa. Kwa muktadha huo, lazima Sheria ya Vyama za Siasa pamoja na Sheria ya Uchaguzi zije Bungeni kabla ya mchakato mzima wa kuteua wagombea kwa ajili ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili; katika mchakato wa Katiba mpya, naiomba sana Serikali ihakikishe kwamba asasi za kiraia kwa maana ya CSOs na NGOs zishirikishwe ipasavyo. Moja, zishirikishwe katika kutoa elimu kwa umma kuhusu Katiba; pili, zishirikishwe katika kutoa mchango na maoni katika namna bora ya kuboresha Katiba mpya. Hapa nitilie mkazo, ni muhimu sana kuhakikisha asasi za kiraia kwa maana ya CSOs na NGOs za mikoa ya pembezoni nazo zinashiriki ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa tatu ni kuhusiana na Samia Legal Aid Campaign. Naipongeza sana Serikali kwa kuja na Samia Legal Aid Campaing, lakini nitumie fursa hii kusisitiza kwamba Samia Legal Aid Campaign ijielekeze zaidi katika changamoto ambazo zinawakumba wanawake na watoto. Mathalani, matunzo kwa watoto, ukatili wa kijinsia, mirathi, ardhi na mengineyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo huo, asasi za kiraia kwa maana NGOs na CSOs zipate fursa ya kushiriki katika maeneo yao. Hapa kipekee na kwa upendeleo kabisa naiomba sana Serikali kupitia Wizara hii, kwamba kwa kuwa Kagera ni kati ya mikoa ambayo ina changamoto kubwa katika maeneo haya, basi katika ile mikoa mitano ya mwanzo ambapo Samia Legal Aid Campaign itakwenda kufanyika, na Mkoa wa Kagera uwe mmojawapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe kwa kusemea viongozi wa Serikali za Mitaa. Nimefanya utafiti mdogo katika majimbo yetu na Wabunge wa majimbo wapo hapa ndani ya Bunge; iko changamoto kubwa ambayo inaendelea kwamba Mwenyekiti wa Kijiji au Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa, au Mwenyekiti wa Kitongoji anaweza akaondolewa katika nafasi yake bila kufuata utaratibu unaostahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, itakapoleta hapa Bungeni Sheria ya Uchaguzi, ihakikishe Sheria hii inawalinda Viongozi wa Serikali za Mitaa waweze kumaliza muhula wao kama ambavyo sheria hii inalinda Madiwani na Wabunge. Pale ambapo kutakuwa na hitaji la kumwondoa kiongozi yule, basi kuwe na utaratibu ulio wazi, unaoeleweka ili kuondoa mianya ya hivi sasa ambayo inaweza kupelekea mtu kufanyiwa hila, mtu kutotendewa haki na kuondolewa pasipo utaratibu sahihi. Siyo hivyo tu, kuna suala zima la haki ya kuchaguliwa na haki ya kuchagua. Hivi sasa yako maeneo mengi ambayo yanaongozwa na aidha Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa maana ya Wenyeviti wa Mtaa au Wenyeviti wa Vitongoji ambao wanakaimu. Hili jambo siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali ihakikishe kwamba inaweka utaratibu wa kulinda viongozi wetu wa Serikali za Mitaa kama ambavyo Madiwani na Wabunge wanavyolindwa, na pale ambapo kutakuwa na haja ya kumwondoa, basi uwekwe utaratibu rasmi kwa maana ya kufuata vigezo ili impeachment iweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa fursa. Naunga mkono hoja. (Makofi)