Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niwe miongoni mwa wachangiaji. Maana Wizara hii kubwa ya TAMISEMI ndiyo iliyobeba mabi.. na mabi. na mabi. ndani yake mkiwa na ma... (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kwamba tunampongeza sana Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia fedha kupitia Wizara hii. Hela nyingi za maendeleo, zinatisha mabi. na mabi. hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumpongeze sana Waziri, na Naibu Mawaziri wake na wataalam wake wakiongozwa na Katibu Mkuu, kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya. Moja, Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa wewe ni Waziri ambaye umekuwa akipokea simu na wenzake pamoja na Katibu Mkuu; huu ndiyo ukweli. Kwa hiyo, tunampongeza sana sisi wenzake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wenzangu wamempongeza kiongozi wa TARURA; CEO. Kwenye ukweli lazima tuseme ukweli, TARURA wanafanya kazi nzuri sana, ombi letu sisi kama Wabunge, waongezewe fedha ili kwenye majimbo yetu barabara zinapitika, lakini ziweze kupitika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie ajira. Wabunge wenzangu hapa wamezungumzia ajira; mimi naunga mkono kwa sababu majimbo yote yana wasomi, majimbo yote walimu waliomaliza vyuo wapo. Kwa hiyo, tukuombe Waziri na wataalam wako, uone kila jimbo hatutaki kwamba aajiriwe katika eneo analotoka; hapana. Lakini watolewe angalau kila jimbo ili wazazi hawa tunaowasomesha watoto wetu katika sekondari zetu ambazo hizi zimetolewa hela nyingi kujenga wapate imani ya watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; wakati anawasilisha Waziri hapa nilikuwa namsikiliza kwa makini na Wabunge wenzangu. Rais Dkt. Samia fedha za zahanati peke yake kwa miaka miwili zimeongezeka takribani 1,066; siyo kitu kidogo. Ndani yake na Makambako tumepata zahanati; tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi katika zahanati ambazo wananchi wamejenga, tunaomba zimaliziwe; ni Mkolango, imeisha, Kivavi, Mwembetogwa na Mjimwema. Zahanati hizi wananchi wamejenga kwa kushirikiana na Madiwani na Mbunge wao, tunaomba zipewe fedha ili ziweze kumalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vituo vya afya kwa kipindi hiki cha miaka mitatu – nilikuwa nakusikiliza Mheshimiwa Waziri – mama Dkt. Samia ameweza kujenga vituo vya afya 344, ndani yake kuna fedha za tozo vituo 234, kuna fedha za ndani vituo 83, jumla vituo 713; hivi vyote vimebeba maB na maB na maB. Fedha nyingi sana, kwa hiyo, tunakupongeza kwa kusimamia jambo hili ambavyo vituo vya afya viko katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu; kwenye elimu fedha nyingi vilevile wakati unawasilisha hapa zimetolewa za shule za msingi na sekondari. Niombe; kwenye Jimbo la Makambako kuna eneo Kata ya Mjimwema, kata hii ni kubwa, tumeandaa eneo na tumeanza, hatuna sekondari. Kata ya pili ni Kata ya Kitandililo, wananchi wamejenga madarasa matatu, Diwani wao na Mbunge wao nimetia nguvu hapo; tunaomba Serikali iweze kumalizia kuhakikisha Kata hii ya Kitandililo tunatapata sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya sasa nizungumzie siasa; amesema Mbunge mmoja kule, Mheshimiwa Kakunda, kwamba mama aliporuhusu mikutano sisi kama viongozi wa CCM tuliguna kidogo. Lakini imeleta tija sana kwa sababu tulifika mahali Waheshimiwa Wabunge tutakubaliana hapa, sisi sote ni Watanzania – tulianza kuogopana. Leo tumekuwa kitu kimoja, ametuunganisha mama, vyama vyetu sasa tunazungumza lugha moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tumpongeze sana mama kwa jitihada hizi. Mwezi uliopita nimekwenda Unguja, Pemba, Zanzibar, nimekwenda kule nikakutana na wa vyama vingine, tulikaa tunakula chakula pamoja, tunazungumza maendeleo vizuri pamoja, nikasema Rais Dkt. Samia na Rais Dkt. Mwinyi wanatakiwa kupongezwa sana kwa kutuunganisha Watanzania ambao sasa tunazungumza lugha moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi, Mheshimiwa wa Upinzani Mwenyekiti Mbowe, ni lazima naye tumpongeze. Kwa nini nasema tumpongeze; kwa namna maridhiano ambayo wameyafanya. Sasa Mbowe amekuwa naye tunashiriki pamoja, tunaongea pamoja bila tatizo lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Mbowe, kwa sababu anataka kuwafanyia maendeleo Watanzania na mama ameshafanya kazi kubwa dunia inamuelewa, 2025 Mbowe tulia muachie mama ili atimize ndoto ya kuwaletea Watanzania maendeleo. Mbowe 2025 shiriki na Madiwani, shiriki na Wabunge, nafasi ya Rais muachie mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile wapo Wabunge wenzetu pale, wale 19, 20 nadhani na yule wa jimbo. Naomba mnisikilize vizuri, na Mbowe anisikilize vizuri, na Mbowe nilikuwa naye kwenye Kamati ya Katiba 2014, tulikuwa Kamati moja na Mbowe, rafiki yangu. Sasa Mbowe na wenzake kwa huruma ya mama amemsamehe kutoka rohoni, mama Dkt. Samia amesema yote yaliyofanyika nafuta, na yeye wale ni wapiganaji wake walikaa mpaka ndani kipindi fulani, awasamehe. Ni wapiganaji wake, awasamehe. (Makofi/Kigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo gani ambalo mtu huwezi kusamehe kila wakati watoke, watoke; wale ni wapiganaji ambao akina Mheshimiwa Mdee wale walikaa ndani, wakipigana juu ya chama chake, sasa awasamehe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi tena kwenye jimbo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la soko, Makambako tunasubiri sana, mlishatueleza mtatujengea stendi ya kisasa, mlishatuambia mtatujengea soko la kisasa. Mheshimiwa Waziri hebu tuma timu ya wataalam, tunasubiri kwa hamu ili tuwaoneshe eneo la kujenga soko na eneo la kujenga stendi ili shughuli za maendeleo katika halmashauri yetu ziweze kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kwa kweli ni laizma tumpongeze sana mama kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akifanya, akitupenda Watanzania na dunia imemuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ahsante sana. (Makofi)