Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha, upo mwongozo wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali, mwaka 2023/2024. Mwongozo huu wenzetu wa TAMISEMI walikutana kati ya tarehe 17 mpaka 21 kuujadili na kuona namna ya kuutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengine, wamezigawa Halmashauri zetu katika makundi manne. Kundi la kwanza ni kundi ambalo ziko Halmashauri tisa. Halmashauri hizi tisa zimewekwa kwenye kundi la kupeleka asilimia 70 ya mapato yasiyolindwa kwenye maendeleo. Kundi la pili, lina Halmashauri 17. Kundi hili limepangiwa kupeleka asilimia 60 ya mapato yasiyolindwa kwenye maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kundi la tatu lina Halmashauri 102. Kundi hili limepangiwa kupeleka asilimia 40 ya mapato yasiyolindwa kwenye maendeleo na kundi la tatu ambalo ndiyo kundi la Halmashauri ya Handeni Mjini iliyopo, kundi hili lina Halmashauri 56 ikiwemo na Korogwe na Halmashauri nyingine nyingi ambazo ningekuwa na muda ningezitaja. Halmashauri 56 zenyewe zimepangiwa kupeleka asilimia 20 tu ya mapato yasiyolindwa kwenda kwenye maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri ya jambo hili ni nini? Jambo hili linapeleka umasikini kwa wananchi wote waliopo kwenye Halmashauri hizi. Jambo hili, literally, halikubaliki! Ukisema kwamba makusanyo yetu ya ndani yasiyolindwa asilimia 20 tu ndiyo iende kwenye maendeleo, tafsiri yake ni kwamba, kwanza tutawa-discourage walipa kodi. Mlipa kodi anataka akilipa kodi yake, ushuru ukikusanywa, aone haspitali pale, kituo cha afya kimejengwa, aone madarasa yanajengwa kwa fedha anayokusanya. Sasa tukiwa tunakusanya halafu asilimia 80 yote tunaenda kuinywa chai, tunaenda kuitumia kwenye mafuta kwa ajili ya usimamizi, hii haitakuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatusababishia matatizo kwa sababu, mbali na kuwa-discourage walipa kodi, wanufaika wetu wa asilimia 10 zile tunazokopesha; tulipokuwa tunatenga asilimia 40 tulikuwa tunapeleka asilimia 10 kuwakopesha wananchi, kuwakopesha akinamama, vijana na walemavu, lakini ukitenga asilimia 20 inamaanisha hata hiyo fedha ambayo unawapelekea inapungua, wanufaika watakuwa wachache. Tafsiri yake ni kwamba, tunatengeneza nchi yenye matabaka makubwa. Wale wenzetu ambao wamepangiwa kupeleka fedha nyingi kwenye maendeleo, ndiyo na fedha zao za kuwawezesha wananchi wao zitakuwa nyingi, lakini na miradi watakayoitekeleza kwenye maendeleo ni mingi kuliko ambavyo sisi tutatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kufanya hivi halafu eti wao TAMISEMI wanasema, tukishaondolewa zile asilimia 20 tukabaki kwenye 20 ya fedha za maendeleo, eti watalipa madeni ya watumishi wasiokuwa walimu. Ukimlipa madeni mtumishi, huo ni wajibu wako, na ni jambo zuri kufanya. Wanasema wataleta stahiki kwa Wakuu wa Idara; huo ni wajibu wenu na ni jambo zuri kufanya. Nasema ni wajibu wenu kwa sababu, vyanzo vyote vya mapato kwenye Halmashauri mmevichukua nyie, kwa hiyo, mna wajibu wa kufanya haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema mtaongeza OC proper, vyote hivyo unavyoviongea vinaenda tu kusaidia uendeshaji wa Halmashauri, lakini ikiwa sisi tulikuwa tunatumia mapato ya ndani kujenga zahanati pale kwenye Zando mwaka juzi, 2021; mwaka jana 2022 tukajenga zahanati Mankinda kwa fedha za ndani, na mwaka huu 2023 tumejenga pale Bangu zahanati kwa fedha za ndani; na tulikuwa tunatarajia kwenye mwaka huu wa fedha tunaopitisha bajeti tukajenge zahanati kule Kwalubaka. Sasa nyie mmechukua fedha zote, tunawaambieni sasa: Je, mtatuletea fedha ili tujenge zahanati hizi ambazo… (Makofi)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi? Haya Mheshimiwa pale.

T A A R I F A

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nataka kumwongezea taarifa Mheshimiwa anayezungumza kwamba, TAMISEMI kuzisaidia hizi Halmashauri ambazo amezipunguzia asilimia 40 kwenda asilimia 20, ni kuhakikisha wanapeleka miradi ya kimkakati ili kupandisha mapato kwenye hizi Halmashauri au kama hizo Halmashauri zilishatengewa miradi ya kimkakati, ikamilike ili kuzisaidia kupandisha Halmashauri hizo, siyo kutoa hizo asilimia 40. Tutasaidiaje wananchi wetu?

MWENYEKITI: Mheshimiwa ni taarifa au ni swali?

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni taarifa nilikuwa namwongezea Mheshimiwa anayeongea.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Reuben unaipokea Taarifa?

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa ya Mbunge aliyetoka kunipa taarifa ambaye anatokea Momba, na Halmashauri yake ni miongoni mwa Halmashauri ambazo zimetengwa ili ziingie kwenye asilimia 20 na fedha zote ziende kwenye matumizi ya kawaida badala ya kwenda kwenye matumizi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema aliyenipa taarifa, Halmashauri hizi lazima tuje na mpango wa kuzisaidia. Suala siyo kuzifanya ziwe likizo ya maendeleo. Hatuwezi kuzipa likizo ya maendeleo, eti wawe wanakusanya asilimia 80 yote wanakula, 20 ndiyo inaenda kwenye maendeleo. Hii siyo sawa! Hii haikubaliki!

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi yote ya kimkakati mmewapelekea ma-giants. Ukija kwenye mradi wa TACTIC; tier one ya TACTIC iko na ma-giants, majiji makubwa. Tier two ya TACTIC iko na ma-giants majiji makubwa, halafu tier three ndiyo tuko sisi wachovu ambao ndiyo tena mnatunyang’anya na mapato, halafu na tier three yenyewe hamuitekelezi. Hii siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu mnapanga wapi? Huu ni utafiti wa wapi mmefanya? Nataka niwakumbushe, ukisoma Five Years Development Plan tuliyonayo ukurasa wa 12, inasema: “The aim of the fifth phase Government was to increase development spending to the tune of 30 - 40 percent.” Huu mpango tuliujadili hapa, tukaupitisha hapa, nyie mnawezaje kujifungia chumbani na kubadilisha bila kuja kutuambia hapa? Yaani mnawezaje kufanya hivyo? Yaani Halmashauri zote 56 zi-paralyze tu kwa sababu nyie mmeamua? Hii siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atakapokuja kufanya hitimisho hapa atuambie, sisi wa Handeni, pamoja na Halmashauri nyingine nyingi kama ilivyo Mpumbwe, Kasulu, Handeni TC, Nyang’hwale, Nzega, Mpama, Iramba, Ikungi, Longido, Namtumbo na maeneo mengine, mta-compensate vipi kwenye hii fedha tuliyokuwa tunapeleka kwenye maendeleo? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)