Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo ili niweze kuchangia kidogo. Mwaka 2022/2023, Bunge letu Tukufu liliidhinisha kiasi cha shilingi bilioni tano milioni mia moja na arobaini na nane ikiwa ni mpango wa kuboresha elimu ya sekondari katika shule zilizojengwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka ilipofika Februari, haikupelekwa hata shilingi mia. Ipo desturi ya Bunge lako Tukufu kuidhinisha fedha kuelekea kwenye miradi ya maendeleo na fedha hizi haziendi, umekuwa kama ni ugonjwa sugu, lakini pia tunafifisha maendeleo yetu. Katika hili kuna shida kwa sababu fedha hizi zilikuwa zinatakiwa ziende kwenye kununua vifaa vya maabara, lakini zikanunue kemikali ili watoto wetu ambao wanasoma shule za sekondari waweze kusoma kwa ufanisi na kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wetu walikosa fursa hii mwaka jana. Kuna tatizo ambalo linatokea baada ya watoto wetu hawa kukosa vifaa vya sayansi. Kuna athari kubwa 2021 wanafunzi 158,185 walipata daraja la sifuri na daraja la nne katika shule za sekondari. Huu ni ukosefu wa vifaa, tumemwona Mama yetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, siwezi kubeza jitihada zake, huyu Mama amejitolea kwa kiwango kikubwa kuilinda na kuitetea Tanzania kwa wivu mkubwa. Kwa sababu tu Rais Samia, aliidhinisha ujenzi wa majengo ya shule za msingi na sekondari kila Mbunge akisimama anajinasibu katika hilo na nitakuwa ni mchoyo wa fadhila kama sitamshukuru katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanafunzi asilimia 66 mwaka 2021, walipata madaraja haya zaidi ya nusu ya watahiniwa. Maana yake nini? Tunakwenda nje ya malengo ya ushindani wa kielimu, kwa nia njema na thabiti kabisa ya Taifa langu naomba nishauri, zipo shule za private ambazo zinafanya vizuri. Zikifanya vizuri siyo kuzifichia matokeo twende tuka–compete nao tuwe partners nao tusi–compete nao, tuwasaidie ili wasaidie Serikali kuweza kufanya vizuri katika matokeo ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na shule nyingi za private zinazofanya vizuri, siyo uchawi ni jitihada katika miundombinu ya elimu, Walimu wanalipwa vizuri, wanalipwa mafao vizuri, ndiyo wanafanya vizuri. Kujenga majengo pekee haitoshi katika elimu. Katika shule za private kumekuwa na mlolongo wa tozo na kodi hii ni kuwarudisha nyuma, tuna–compete nao hawa tunawaweza tuungane nao, tuboreshe elimu ya Tanzania, tuondoe tozo na kodi, ziko zaidi ya 15, akija mtu anawekeza kwenye elimu anaanza kuogopa, tuige kwa wenzetu Uganda na Kenya waliwaleta karibu, wakaungana nao, elimu imeboreshwa. Tuungane na private sector twende tukadumishe elimu kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna shida kwenye elimu. Watu wengi wameitika elimu bila ada, wameitika siyo siri. Hata hivyo, wanaokwenda kumaliza shule elimu ya msingi na sekondari wanakuwa ni nusu ya wale walioanza. Katika Ripoti ya CAG inaeleza katika halmashauri 11 za shule ya msingi tayari wanafunzi zaidi ya nusu…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Njau, Ripoti ya CAG ya mwaka gani?

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ya mwaka 2021. Halmashauri ya Kwimba wanafunzi waliandikishwa 6,950, waliomaliza shule ya msingi ni 3,783 sawa na asilimia 49, ndiyo iliyoongoza kwa wanafunzi kuacha shule. Huenda ni miundombinu lakini sisi kama Taifa tuboreshe miundombinu yetu ili tuweze ku–compete na elimu yetu. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Nataka kumpa taarifa muongeaji kwamba Wilaya ya Kwimba wanafunzi ambao hawakwenda kumaliza elimu yao ya msingi ni kwa sababu ya fisi walikuwa wametanda maeneo hayo kwa muda mrefu, lakini siyo kwamba labda eti watoto wale wameshindwa kumaliza elimu ya msingi kwa sababu wamekwenda kuchunga ng’ombe, Hapana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Njau, unapokea taarifa?

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, amenibeza. Inayofuata ni Halmashauri ya Kinondoni Mjini, ambayo wanafunzi walioandikishwa kuanza shule walikuwa 15,000, waliomaliza ni 4,652. Tayari tumeshuka sawa na asilimia 46. Kwa hiyo tunaweza kusema ni kijijini lakini pia mijini lipo hili tatizo, kuna nini? Ni lazima tufuatilie kwa ukaribu ili tujue kwa nini watoto wetu hawamalizi shule? Kwa nini wanakuwa na ari ya kwenda shule lakini hawamalizi shule. Kwa hiyo kuna tatizo ambalo liko hapa katikati, tutakapoacha tutaliacha Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea. Katika shule za sekondari walioanza katika Halmashauri ya Newala, kati ya wanafunzi 7,950, waliomaliza ni elfu nne na kitu. Hii idadi bado inazidi kupungua. Kwa hiyo ushauri wangu tuungane na sekta binafsi, tuboreshe elimu yetu, tuangalie changamoto iko wapi, twende tuka–solve changamoto, lakini tusisahau maslahi kwa Walimu. Walimu wana wakati mgumu japo hawatoshi, lakini wale waliopo wanalia ukata. Mishahara midogo, pesa zao za malimbikizo ya kupandishwa vyeo hawana, miundombinu ni mibovu. Tukienda kuboresha hapa nafikiri tunaweza tukapata kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye asilimia kumi ya mikopo. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla, jana walitoa kauli thabiti ambayo akinamama waliokuwa wanategemea wa waliyokuwa wanayategemea walisikia ile kauli wakawa na wasiwasi. Nasema leo nawaondoa wasiwasi, kauli ya Serikali ni thabiti kwa sababu kulikuwa na mianya ya rushwa, pesa zilikuwa zinapewa watu, si wahusika, kwa hiyo kimsingi ni lazima ufuatiliaji upatikane na watu waanze kufanya utafiti, ndipo pesa hizi zitolewe tena. Naiungana mkono Serikali katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)