Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi na mimi niweze kuongea machache kujaribu kuzungumzia hotuba ya Waziri Mkuu.

Kwanza napenda kuishukuru Serikali yangu kwa kazi kubwa ambayo wameifanya, na katika moja ya kazi ambazo wamefanya; nimejaribu kuangalia miradi ambayo ni miradi mikubwa sana ambayo imezungumzwa katika taarifa ya Waziri Mkuu; kwamba kuna miradi takriban saba ambayo imetumia fedha nyingi sana; na fedha hizo ni kweli nitasema kwamba ni pesa ambazo kwa kiasi fulani tujipe moyo Tanzania inasonga mbele. Kama alivyozungumza Rais wetu mpendwa mama Samia Suluhu Hassan kazi iendelee, kweli kazi inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejaribu kufanya ziara na Kamati yangu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, tumepita miradi kadhaa. Ndani ya nchi hii kuna vitu ambavyo vinafanywa ni vikubwa sana; na hii inaonesha uhalisia kwamba nchi yetu inapiga hatua na uchumi unaweza ukakua kwa kiasi fulani. Hata hivyo, kwenye miradi hii ningependa pengine kuishauri Serikali; miradi ni mikubwa lakini kitu muhimu zaidi ni kuweza kujua namna na adhma ya ile miradi yetu. Lengo ni kuhakikisha uchumi wa nchi unakua.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Serikali ilipojenga reli ya Standard gauge ilikuwa na dhima maalum. Maana yake ni kwamba tukimaliza ujenzi wa reli hiyo tujue adhma ya Serikali ni kitu gani pamoja na miradi yote ambayo ilikuwepo, ikiwemo ya meli na miradi mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nije katika mchango wangu kuhusiana na taarifa ya Bajeti ya Waziri Mkuu, nijaribu kugusia taasisi moja ambayo inahusiana na masuala ya Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA). Hii taasisi kwa kweli inafanya kazi zake kubwa sana kwa mujibu ambavyo ilivyo na objective zake zilivyo au malengo yake yalivyo, lakini shida ambayo iliyokuwepo ni kwamba TaESA ni kama ni agency; tunasema kwamba imemeza kila kitu. Tukiangalia katika hali ya sasa kwa dunia hii ya leo TaESA mimi nadhani kungelikuwa na uwezekano tukawa na kamisheni itakuwa inafanya uratibu wa shughuli hizo. Baadhi ya shughuli za TaESA tuwaachie mawakala wa ajira ili kuhakikisha kwamba tunaleta muunganiko mzuri katika masuala ya uajiri; na hii inakuja kwa sababu ya mtazamo wa kidunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtazamo wa kidunia ni mpana sana. Mtazamo wa kidunia hasa katika suala la soko la ajira limekuwa la pembe tatu. Kuna suala la mawakala wa ajira, kuna suala la muajiri pamoja na yule anayeajiriwa, sasa ili kuweza kupata ajira maana yake ni lazima uanze kwa wakala wa ajira twende kwa mwajiri pamoja na yule candidate kuweza kufikiwa katika shughuli zake. Kwa sasa hivi inakuwa kama kuna monopolize ya hili soko, maana hata hao mawakala wa ajira waliokuwepo katika Taifa letu hili la Tanzania wanafanya, kisheria, kama ni brokers kwa sababu wale sio mawakala hasa. Kwa sababu wao watafute ajira au watafute kazi kisha wazipeleke kwa TaESA ambapo TaESA ndiye atakayeweza kuhakikisha kwamba mtu yule anapatiwa ajira kwa namna gani na hususani katika ajira ambazo ni za nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili mimi pengine ningeshauri Wizara, ili kuwe na ufanisi mzuri na mkubwa zaidi katika hii taasisi ambayo inahusiana na masuala ya ajira iache baadhi ya loop hole kwa upande wa mawakala wa ajira. Hii ni kwa sababu sasa hivi kidunia tumesaini mikataba (conventions) mbalimbali ya kimataifa zinazohuaiana na labour, ambayo ni lazima tuifuate. Kuna mashirika kwa mfano kama A.I.O, I.O.M ambayo yanahusiana na masuala ya uhamiaji, wale wote wanatakiwa kuratibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri zaidi kila mhamiaji anapokuja, anapotafuta nafasi ya ajira apitie kwa wakala maalum ambaye ndiye ataweza kumpatia nafasi ya ajira. Sasa kazi ya taasisi inayoshughulika na ajira maana yake ifanye kazi ya coordinate na kuchukua data kupitia kwa wale mawakala. Nadhani kwamba inaweza ikafanyika kazi nzuri zaidi na hii inakuja hata kwenye vibali vya ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutasema tuna vibali almost 8,576 vya kazi, vibali vile ndizo kazi zenyewe za watu wetu ambazo wamepatiwa watu wa nje. Tusiseme kwamba tumepata vibali vingi, kwamba sasa vimetuongezea mapato, tujaribu kuangalia kwa upande wa pili; kwamba zile ni ajira za watu wetu kwamba sasa wamepatiwa ajira watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili suala ili kuwe na ufanisi kwa suala la ajira na kusiwe na ule ulegevu ambao; kama kuna Mbunge mwenzangu mmoja alizungumza jana; kwamba imekuwa kama TaESA haina meno, shida yenyewe ni kwamba taasisi ya TaESA ilivyozinduliwa kwa wakati ule ilikuwa kuna haja hiyo. Hata hivyo kwa wakati ambao tunao kwa sasa hivi ni wakati ambao unakwenda katika sayansi na teknolojia, hivyo lazima kuna baadhi ya mambo wajipunguzie ili kuweza kwenda katika hali ya usawa, vinginevyo siku zote ajira zitakuwa zina shida; lakini kama zitakuwa zinapitia katika mlengo wa kimawakala kwenda kwa waajiri ingekuwa ni vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na lingine ambalo naweza kulizungumza ni kwamba TaESA kama ni mawakala ni vizuri zaidi kila baada ya mwaka wakatengeneza kitu kinaitwa career fare; ambacho kitakuwa kinakusanya mawakala, waajiri pamoja na candidate kwa mujibu wa fani zao walizo nazo. Sasa kama mwajiri atakuwa anahitaji mfanya kaziā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, shukrani.