Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa kuchangia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza, nianze kwa kukupongeza wewe binafsi kwa kuendelea kukalia Kiti na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niipongeze sana Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Mawaziri wote, kwa kazi inayoendelea kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Pwani napenda kushukuru sana kwa miradi mbalimbali iliyotekelezwa ndani ya Mkoa wetu wa Pwani kwa kipindi hiki cha miaka miwili tangu Mheshimiwa Rais Samia ameingia madarakani. Tumeshudia mwaka ulioishia Juni, 2022, Mkoa wetu ulipokea fedha za ziada zaidi ya bilioni 20 kwa ajili ya miradi mbalimbali ukiwemo ujenzi wa madarasa, ujenzi wa vituo vya afya, miradi ya maji n.k. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mwaka huu wa fedha unaoendelea mpaka sasa licha ya kwamba tumeshapokea bajeti ya zaidi ya asilimia 75 ya pesa za miradi ya maendeleo. Lakini tumepokea pia nje ya bajeti zaidi ya bilioni 10.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo ujenzi wa madarasa 341. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuja na pesa za kumalizia miradi iliyokuwa inatekelezwa na Mradi wa EP4R ambapo jana nilipita Bagamoyo nikakuta pesa, milioni 100, Shule ya Sekondari Kingani kwa ajili ya kumalizia bwalo, na miradi hiyo ilikuwa mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pesa hizo, niombe Serikali inapopanga miradi hii ya maendeleo, hususan ujenzi wa madarasa na vituo vya afya ambako unatoa pesa za kiwango cha aina moja, niishauri Serikali iangalie maeneo kwa mfano ya visiwa, hayafanani. Kwa hiyo, unatoa pesa kwa maeneo yanayolingana kwa kiwango kimoja lakini yapo maeneo ambayo miundombinu siyo rahisi kufikika, na hapa narejea Visiwa vya Mafia, Mkuranga na Kibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa Mkuu wa Wilaya pale Rufiji anajua mazingira. Leo ukitenga pesa inayofanana na Kata za Mbuchi, Kiongoroni, Salale na maeneo mengine kwa kweli pesa hizi zinakuwa hazitoshi na inasababisha halmashauri zetu kutumia pesa ya ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, niseme pia nina ushauri. Nimeisoma Hotuba ya Waziri Mkuu katika ukurasa wa 66, masuala mazima ya uwezeshaji wa wananchi. Hapa niombe kuishauri Serikali, ina mifuko zaidi ya 63 ya kuwezesha wananchi ambayo ipo katika Wizara mbalimbali, ifike wakati sasa ile mifuko iunganishe. Pengine iwe chini ya Waziri Mkuu au moja kwa moja Ofisi ya Mheshimiwa Rais ili wananchi wengi, hususan wanawake, wapate kuelewa fursa zinazotokana na mifuko hii ili waweze kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ushauri huo, napenda kuipongeza Serikali, katika Mkoa wetu wa Pwani kwa mara ya kwanza wamekuja na Mji wa Viwanda, eneo la viwanda, Kongani ya Viwanda Kwala. Na uwekezaji mkubwa uliofanyika pale na namna ambavyo imeweza kuweka mpango mkakati mzuri mji ule utakuwa wa mfano wa kuigwa na utazalisha ajira 100,000 ambazo ni rasmi na nyingine zaidi ya 300,000 zisizokuwa rasmi; kwa hiyo, naishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa pia naomba niikumbushe Serikali pia eneo la ujenzi wa viwanda Bagamoyo na eneo la ujenzi wa bandari Serikali bahati nzuri imekuja na mpango mzuri tu wa kutumia sekta binafsi na Serikali yenyewe kujenga bandari na hili eneo la viwanda lakini naomba niikumbushe ulipaji wa fidia wa maeneo hayo, wananchi wetu wa Bagamoyo wamesubiri muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa tumeona Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki, ametangaza nafasi za kazi. Niishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutoa ajira kwa vijana wetu; nafasi zaidi ya 20,000. Na naishukuru kwa sababu imekuwa na kawaida tangu Rais Dkt. Samia ameingia madarakani kila mwaka amekuwa akitoa kibali kwa ajili ya nafasi za kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri; kuna vijana wengi wanajitolea, walimu na sekta ya afya, na imewahi kusemwa hapa Bungeni kwamba zikitokea hizi ajira vijana wale hawafikiriwi kabisa. Kama sasa hivi anakubalika kujitolea kwa nini inapotangazwa ajira rasmi aonekane hana sifa? Na nimeona tangazo na vigezo, Serikali iseme neno. Na Mheshimiwa Spika alitoa maelekezo kuwa Serikali iseme neno kwa vijana wanaojitolea ambao leo sasa neema imeshatangazwa, taratibu zake zikoje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masuala ya miundombinu niishukuru sana Serikali kipekee kwa ujenzi wa Daraja la Mbuchi. Daraja hili Mheshimiwa Waziri Mkuu amefika na hata wananchi wa Mbuchi wamesema waziwazi, kwa ukombozi kupitia daraja lile kwa kweli hawana namna, ni kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijitendei haki kama sitachangia suala zima la maadili. Tumeona namna gani Wabunge na hata viongozi wa dini na wananchi mbalimbali wamekuwa wakilisemea. Tumeona ongezeko la vitendo vya ubakaji na kulawiti kwa watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka jana tu, 2022, matukio zaidi ya 12,000 kulinganisha na matukio 11,000 yaliyotokea mwaka wa fedha uliopita. Pamoja na adhabu mbalimbali wanazopewa, kifungo cha miaka 30, niiombe Serikali kwa kuwa matukio yanaongezeka, iandae mdahalo wa Kitaifa tujue tatizo ni nini hasa na iangalie hii sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisoma hotuba ya Waziri Mkuu, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na mambo mazuri aliyosema juu ya ulinzi wa watoto, ningefurahi kama angegusa walau hata mapitio ya sheria, walau hata mapitio ya kufanya mdahalo kujua chanzo ni nini. Kwa nini kuna ongezeko kubwa la matukio haya; nini kimebadilika sasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tu tumesoma baba mzazi amembaka mtoto wa mwaka mmoja Iringa huko; hili siyo jambo la kawaida. Na matukio yamekuwa yakiongezeka mara kwa mara. Kwa hiyo, niiombe Serikali, na niunge mkono, inaonekana adhabu ya miaka 30 haitoshi, adhabu iwe kuhasiwa tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nimpongeze Mkuu wetu wa Wilaya ya Bagamoyo, yeye ametoa kabisa maelekezo; hakuna Mtendaji wa Kijiji wala wa Kata wa kutoa barua ya kudhamini wanaofanya matendo haya ya ubakaji. Yale makosa yanadhaminiwa lakini tukiweka msingi huo wa kutodhamini, kwa nini adhaminiwe. Mtoto ameharibika! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Bagamoyo ndani ya wiki tatu tu watoto zaidi ya watano wamebakwa na kulawitiwa na wamelazwa katika Hospitali yetu ya Bagamoyo. Na zaidi ya kesi 10 ziko mahakamani kwa kipindi kifupi tu. Kwa hiyo, napenda kusema hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa Ripoti ya CAG; na mimi naunga mkono kubadilisha kanuni. Kwa sababu kuna vikundi mbalimbali vimeshajadili, vimeshatoa hukumu, vimeshatoa maelekezo kabla Serikali haijapata nafasi na CAG kuja kwenye Kamati za Bunge. Itakapofika Novemba nachelea kusema tutakuja kufanya nini. Kwa sababu Watanzania wameshaaminishwa vya kuaminishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa Mkaguzi wa Hesabu Ofisi ya CAG na utaratibu huu wa CAG ulianza tangu 2007, hivihivi anawasilisha taarifa kwa Mheshimiwa Rais baadaye anakuja Bungeni inawasilishwa anakutana na Wenyeviti wa Kamati, wanazungumza, taarifa inakuwa public inaendelea kujadiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama tutaacha msingi wa kila mtu atakayeona inafaa anajadili na kutoa hukumu na kujumlisha hasara zilizopatikana bila utaratibu mahususi kwa kweli Mwenyekiti tutakuwa hatulitendei haki Bunge. Zinatajwa hasara mbalimbali wakati nyingine pengine siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri tupate fursa na sisi kama Wabunge, kwa sababu ndio tuliokasimiwa kwa niaba ya wananchi, tuijadili ripoti ili iwe rasmi kuliko ilivyo sasa; vyama vya siasa vimejadili, wananchi mbalimbali wamejadili, wameshatoa hukumu zao wakati pengine hali ilivyo sivyo inavyoafsiriwa kwenye taarifa za CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimalizie taarifa ile pia nayo ni ya kitaalam. Niwaombe Watanzania, siyo kila hoja ni ufisadi, tutatishana bure.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Subira.

MHE. SUBIRA K. MGALU: …lakini tuipe nafasi ili ufafanuzi utolewe. Naunga mkono bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu; nampongeza sana. Ahsante sana. (Makofi)