Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nami nampongeza Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri na watumishi wote wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaliongea kidogo suala la CAG, lakini siyo kwa tarakimu. Suala hili la CAG linatupa wakati mgumu sana na sioni kama kuna uwezekano tutakwenda labda miaka 10 wizi hautaisha. Labda tutafute namna ambayo ni nyepesi kidogo. Kwa nini CAG anakagua baada ya tukio? Kwa nini CAG asianze kabla ya mradi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yangu ni kawaida mbwa huwa anabweka wakati kuna mwizi ili mwenye mali atoke, lakini mbwa akibweka baada ya kuibiwa, kuna uwezekano kwamba mbwa hakuwepo kwenye eneo lile. Kwa hiyo, tumwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama itakupendeza, tuwe na Wizara ya Matumizi na Wizara ya Kero. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, anayetayarisha mradi ni Katibu Mkuu na watumishi wake kwenye Wizara au sisi Halmashauri. Tunashauriana kwa sababu ya pesa zilizopo, tunaamua tufanye mradi. Hapa kwenye mradi, anachoangalia CAG ni kile kilichotoka nje ya ule mradi, lakini asilimia 80 ya miradi ile haina mahitaji yoyote kwenye jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano wa masoko yetu. Ni kweli, soko la ghorofa unatarajia kweli ujenge soko la ghorofa uweke nyanya watu wakanunue na umetumia shilingi bilioni 30; haiwezekani! Yaani tubishe, yaani tuone kabisa, tunaona soko la kawaida liko mahali pale, unaweka soko la shilingi bilioni 40 kwenda kuweka nyanya na samaki, watu watafuata kweli kwenda kununua? Kama kungekuwa na Wizara ya matumizi, huu mradi ungepelekwa kwao, wakauangalia kwamba huu mradi; je, unafaa? Kama wanaona unafaa, wampelekee na CAG na TAKUKURU wauangalie ndiyo uje Bungeni. Ingekuwa muda huu tunazozana fedha hazijaenda, lakini sasa hivi tunazozana pesa zimekwenda, tena tunaidhinisha bajeti nyingine. Tutafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunaiona miradi yetu asilimia kubwa haina faida kwa wananchi, badala yake tena inakuwa kero. Leo unabebwa kutoka hapa unaambiwa huwezi kuteremka na basi hapa na mvua inanyesha, lazima uende mwisho kwenye stendi ya Nane Nane. Umetoka Bahi, ni shilingi 5,000 kuja hapa. Ukiteremshiwa Nane Nane kurudi tena huku, ni shilingi 10,000. Huyu mwananchi tunamwadhibu kwa sababu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo utatengeneza mradi; huo mradi wako ulichukua hela zetu, ukatengeneza mradi mbaya, halafu leo unatuadhibu sisi tena wenye hela. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu alifikirie kwa mapana sana. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimemuunganisha Waziri wa Matumizi na Waziri wa Kero? Nafikiri mmeona hoja hapo ya Mheshimiwa Kunti ilivyokuwa. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu, inatupa wakati mgumu sana sisi kukabiliana na Mawaziri kwenye matatizo ya hoja, lakini kama kuna Waziri wa Kero, sisi tutapeleka kero zetu kwake yeye, yeye ndio atazipeleka kwa Waziri Mkuu. Maana yeye hahusiani na kitu chochote, ni kama Waziri asiye na Wizara Maalum. Itatusaidia sana. Kuna kero nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunalia ajira. Leo daktari anamaliza University Muhimbili, anakuja hana kazi, lakini haruhusiwi hata kufungua kiosk kuchoma watu sindano, lakini Mmasai anatembeza dawa na ana kibali cha Wizara ya Afya. Sasa tunafanyaje? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu umechukua milioni yake 40, baadae ukamfunga pingu, haruhusiwi tena kuuza dawa, lakini mtu ambaye hakusoma, anatembeza dawa. Samahani ndugu zangu Wamasai kama mpo. Anatembeza dawa, tena anakwambia inatibu magonjwa 40, unakuja saa ngapi? Sasa unafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima twende upya. Mabadiliko ni makubwa sana duniani. Lazima tufungue vitu vingi sana, kero ni nyingi mno. Leo wote humu ni mashahidi. Tunapanda ndege kutoka hapa Dodoma kwenda Dar es Salaam, hapa unasachiwa, unafika Dar es Salaam unasachiwa tena. Je, ulipakia abiria huko angani? Nani alipanda angani? Sasa tutamwambia nani? Hakuna wa kumwambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda barabara yetu ya mwendokasi. Mwendokasi unaona ziko nne, upande huu kuna daladala zaidi ya 100, lakini haziruhusiwi kuhamia huku, lakini huku hakuna watu, lakini nao si wanalipa deni hilo hilo! Mvua inanyesha, wamo mle kwenye daladala wameshika mkono, kwa nini wasiruhusiwe watu wa daladala wakatumia hii kwa muda mpaka tutakapopata mabasi? Maana hawa na wenyewe si wanalipa deni. Je, ikitokea mwenye funguo za ofisi yuko kwenye daladala, wewe wa mwendokasi ukawahi, faida ya mwendokasi itakuwepo? Si utakuwa mlangoni! Haitawezekana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, najaribu sana kufafanua kwamba, akiwepo Waziri wa Kero na Waziri wa Matumizi, sasa hivi ndiyo ungekuwa muda wetu kubanana kwamba, mradi huu tumeukubali uende, mradi huu bwana kama unataka kuuza nyanya kwa shilingi bilioni 20 hatutaki. Katengeneze banda la shilingi bilioni tatu, wanunuzi wa nyanya watanunua. Kwa hiyo, tunge-save sana. Huu mvutano wote usingekuwepo. Nafikiri mnafahamu kesi ya CAG ilivyowahi kuleta matatizo mengi mno kwenye Serikali. Mengi mno!

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa hiyo, tukuombe ulifikirie kwa makini sana. Pia bado najiuliza, Serikali imeamua kurudi kwenye biashara. Kilichoifanya ikatoka miaka ya 1980 na miaka ya 1990 kimebadilika? Watu wa miaka ya 1990 na 1980, na hawa wala blue band wa leo, kama wale walishindwa waliokuwa wanakula mihogo, hawa wala blue band wataweza biashara? Kweli tumeamua kurudi kwenye biashara? Kweli tutaweza? Kwa haya matatizo tu yaliyotokea haya ya wizi, tunarudi kwenye biashara tena za gharama kweli, tutaweza kuziendesha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiwaona matajiri, asilimia 80 hakuna mzima. Mwingine ana gout, mwingine ana pressure, yaani kutwa nzima makoti yamejaa vidonge: Je, itawezekana kweli! Au kwa kuwa, Serikalini ninyi mnastaafu miaka 60, mnataka kumtelekezea nani huo mzigo? Maana mzigo huo ulishatelekezwa miaka ya 1990, tukauza na viwanda, tukasema jamani tunatoka, sisi tunarudi kwenye kodi, lakini immediate tunaenda moja kwa moja tena kwenye biashara. Kabla hatujaanza biashara, nusu ya hela imeibiwa. Sasa hiyo biashara tutaianzaje? Nani atatuletea hela? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa hiyo, tunaomba sana hili suala la CAG tubadilishe huu utaratibu ili tujadili hela kabla ya wizi wenyewe. Baada ya hapo, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)