Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia nami nafasi niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 42 mpaka 43 umezungumzia suala la ardhi kama mtaji, pili kutokana na ardhi tuliyonayo kuwekuwa na migogoro mingi hali kadhalika nayo ameizungumzia kwamba sasa tunakwenda kwenye suala zima la utatuzi wa migogoro ili ardhi yetu iweze kutumika kama mtaji kwa maana kwenye sekta ya kilimo, sekta ya mifugo, sekta ya maliasili na sekta nyingine zote kwa sababu ardhi ndiyo kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya maneno mazuri yaliyoandikwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, yamekuwa yakiandikwa kila hotuba ya kwake ya Waziri Mkuu lakini pia na ya kisekta kwenye Wizara zake husika. Tumekuwa tukizungumza suala zima la migogoro ya ardhi, Serikali imekuwa bado haituelewi, sijajua changamoto ni nini haswa, wanaona raha hiyo migogoro kuendelea kuwepo hapa nchini, ama kuna kitu wananufaika nacho kutokana na hii migogoro, sijaelewa! Wakija wataniambia kwa nini Serikali haitaki kutatua migogoro ya ardhi ya kiutawala lakini na migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, migogoro ya ardhi baina ya maliasili pamoja na watumiaji wengine wa ardhi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Chemba mgogoro baina ya maliasili pamoja na wananchi. Pori la Swagaswaga tumelizungumza, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili, Waziri wa TAMISEMI, Mifugo, Maji, kadhaa Mawaziri Nane walienda kwenye Pori la Swagaswaga, wakaenda wakazungumza na wananchi wakawaeleza hali halisi iliyoko pale. Wale wananchi wameanza kuishi pale kabla ya uhuru, wameishi pale kabla ya Serikali kwenda kuanzisha hifadhi, wameishi pale kabla hata ya uanzishwaji wa vijiji miaka ya 1970 huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali hiyo hiyo imejenga shule, imejenga zahanati, ni wapiga kura wanapiga kura pale, Serikali inawatambua, leo wakigeuka upande wa pili wa shilingi wanaambiwa ni wavamizi, mmevamia eneo la hifadhi, watu wanapigwa, watu wanauawa, watu wanafanyiwa manyanyaso ya kila aina, mpaka ubakaji unafanyika kwenye Hifadhi ya Swagaswaga. Hiki kitu siyo sawa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Mawaziri Nane imekwenda imepeleka wataalam, wamepeleka wataalam pale! Wataalam wameenda wamepima, kwa nini Serikali inakuwa na kigugumizi cha kutoa tamko la suala zima la wananchi wa Pori la Swagawaga kuendelea na maeneo yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wamelima mmeenda kufyeka mahindi ya wananchi wangu, kwa sababu gani za msingi? yaani mtu mmemuacha anaenda analima, anapanda, mazao yanaota, yanakua, mnaenda mnafyeka siyo laana hiyo? Siyo laana hiyo?

MBUNGE FULANI: Ni laana!

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini mvua inyeshe? Kama Mwenyezi Mungu anatuletea mvua ya bure hatuilipii tunalima, tunapanda, mnaenda mnafyeka eti kisa hifadhi! Hivi tusipokuwepo leo hifadhi zitakuwa zina thamani gani? Tusipokuwepo binadamu hifadhi zitakuwa na thamani gani? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunti kuna taarifa kutoka kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wana muda wa kujibu wangetulia tu.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge anayeongea hivi sasa, kwamba sisi kama binadamu na hata viumbe waliopo hapa duniani tuna-balance kwa eco-system. Tusingeweza kuishi peke yetu bila kuwepo na wanyama, kuwepo na mimea, kuwepo na hifadhi, kuwepo na rasilimali zote zilizopo hapa nchini. Kwa hiyo, nataka kumpa taarifa kwamba hifadhi ni za muhimu asizione kama ni kitu ambacho hakihitajiki hapa duniani au hapa Tanzania.

Mhehsimiwa Mwenyekiti, pili nampa taarifa pia kwamba athibitishe kama kuna watu wameuawa, watu wamebaka, vinginevyo aondoe hii kauli.

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Kunti, taarifa hii unaipokea?

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye ni Shahidi alikwenda Swagaswaga, mmefika pale mmeambiwa kwani mnachoficha ni nini? Hivi watu wale wananawake wanapoumia wewe unanufaika na nini? Lakini suala la kwamba eti tuna-balance tunahitaji, sawa tunaitaji tumepewa Mwenyezi Mungu ametupa hizi rasilimali ziweze kutusaidia na kutunufaisha watu wote sote, hawa wanyama wanufaike na sisi binadamu tuweze kunufaika. Leo kwa nini mnaona thamani ya mnyama kuliko binadamu? Kwa nini mnaweka thamani ya mnyama ni kubwa kuliko binadamu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wizara wakija kuhitimisha waniambie mgogoro wa Swagaswaga unaisha lini Wilaya ya Chemba? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la misafara ya Viongozi. Viongozi wetu tunawaheshimu na tunawapenda na tunajua changamoto kubwa wanazo kwa majukumu yao wanayoyafanya. Hivi kweli tunasema muda ni mali, wakati ni mali, kusimamisha wananchi zaidi ya masaa matatu barabarani, Kiongozi hajatoka atokako, tuna wagonjwa, tuna watu wanatakiwa kwenda kutekeleza wajibu na majukumu yao mbalimbali. Mimi ninaomba Viongozi wetu wanaosaidia hususan wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Polisi biashara ya kusimamisha wananchi mabasi sijui magari mengine na wananchi wengine watumiaji wa barabara kwa ajili ya viongozi wetu wanapopita waende kwa sababu wana mawasiliano. Wawe wanawasiliana kwa kadri muda unavyosogea wawe wanawaacha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Waziri Mkuu alikuwa natatoka nyumbani kwake kuanzia Saa Mbili na Dakika Kumi na Saba magari yamesimamishwa foleni imefika mpaka Nzuguni. Tunapandisha uchumi huo? Uchumi unapanda? Kusimamisha, sasa hiyo ni moja lakini je, fikiria hapa alikuwa anatoka hapo Mlimwa, kama Waziri Mkuu ameamua kutumia leo magari kutoka Dar es Salaam mpaka aje afike hapa Dodoma wananchi watasimama kwa muda gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana hivi vitu vingine hebu tuwe tunaenda na wakati na kwa safari ndefu niombe Viongozi wetu Wakuu watumie ndege waache kutumia magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye suala zima la maadili.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Taarifa.

MWENYEKITI: Kuna taarifa Mheshimiwa Kunti.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja.

MWENYEKITI: Kuna taarifa Mheshimiwa Kunti.

Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.

T A A R I F A

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Wewe utakuja kujibu lakini. (Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Hapana Mheshimiwa Kunti si ungekaa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge, tunafahamu wote kwamba utaratibu wa utendaji kazi wa viongozi wetu umewekwa kwa mujibu wa taratibu mbalimbali ambazo zinasimamia pia heshima ya viongozi wetu hapa nchini.

Kwa hiyo, suala la namna ya ku–control hilo ni la watendaji ambao wako chini ya mamlaka zinazohusika. Kwa hiyo, nadhani ingekuwa ni bora tu kwa Mheshimiwa Mbunge kutoa ushauri kwa mamlaka zinazohusika badala ya kuhusianisha na utendaji kazi wa Viongozi wetu ambao umewekwa kwa utaratibu unaozingatia heshima ya Viongozi wetu pia hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tukiliweka hivyo litakuwa na logic nzuri zaidi kuliko kuendelea kusema Waziri Mkuu, kiongozi fulani. Tuende katika utaratibu ambao ni wa

usimamizi wa kiusalama na mambo mengine. Pia ni practice ambayo ipo katika ulimwengu mzima, practice ambayo imekuwa ikitumika katika kutoa heshima kwa Viongozi wetu na kuzingatia utaratibu ambao unatumika katika uendeshaji wa shughuli za viongozi na Serikali katika ulimwengu mzima. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunti taarifa unaipokea.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mwongozo wa Spika.

MWONGOZO WA SPIKA

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo wako. Tunajua kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, taarifa kuna muda maalum na imekuwa tabia ya Bunge hili Mawaziri kutumia muda wa Wabunge vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko kwenye kuchangia Bajeti kama wanataka kujibu, wasubiri kwa muda wao wa Kikanuni wa kujibu watapewa nafasi. Kama taarifa hatukatai lakini waende specific kwenye hoja na watumie muda wa Kiti vizuri.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunti malizia mchango wako.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali, ndiyo tuko na wananchi kule chini, tunaona adha za wananchi, tunawashauri. Mkiona inafaa tekelezeni, mkiona haifai basi to hell haina shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu maadili katika jamii yetu. Nilikuwa najiuliza kwa sauti nawaza, nikawa nasema hivi Serikali ina kila uongozi kule chini, kwenye Mtaa tuna Viongozi, kwenye Kata tuna Viongozi, kwenye Wilaya tuna Viongozi, kwenye Mkoa mpaka Taifa, hawa watu wanaosagana, hawa watu wanao sijui mwanaume anaenda anamngonokea mwanaume mwenzie, halafu ukiangalia hivi hii inaingiaje akilini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wako kwenye mitandao tunawaona, wanajisifu, Serikali mpo. Wanadhalilisha Taifa letu, mmekaa kimya. Baraka, tukiona Wamachinga wako pale One Way, tunapeleka mgambo na polisi kwenda kuwachapa, wasagaji na wanaofanyana mambo ya ajabu ya kudhalilisha Taifa mmekaa kimya, hamsemi la heri wala la shari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Mama Massaburi anachangia, Mheshimiwa Mtemvu akasema na Wabunge tupo. Sasa nikawa nashindwa kushangaa, ndiyo maana hatuchukui hatua kwa sababu na sisi Wabunge tunafanyiwa haya maneno! Kama mimi Kunti nahusika, nafanywa na mwanamke mwenzangu; nafanywe na mwanamke mwenzangu? Inakuwaje? (Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kunti, muda wako umeisha.

MHE. KUNTI Y. MAJALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ichukuliwe hatua. Biashara ya wanawake kufanyana na wanaume kufanyana wenyewe kwa wenyewe, ikome katika Taifa letu. (Makofi)