Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Kama wenzangu walivyosema nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan, kwa mambo yote ambayo Wananjombe na hasa katika Jimbo langu tumeyaona yakija katika maeneo yetu. Tumekuwa na miradi mikubwa ya maji, kero ya maji ilikuwa ni kero kubwa sana katika Halmashauri ya Njombe lakini sasa tunayo miradi mikubwa miwili inayoendelea Mkandarasi anakwenda vizuri. Afya kwa mara ya kwanza wananchi wa Njombe sasa wamepata CT scan na wanaweza wakaacha kufunga safari kwenda Mikoa ya jirani kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa barabara kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais tunayo barabara ya Itoni kwenda mpaka mpakani na Ludewa ambayo ilikuwa ni changamoto kubwa sana. Barabara hiyo sasa Mkandarasi yupo site, bilioni 95 zimekuwa allocated na ina kilometa 55. Baada ya kusema hayo niende kwenye kuchangia lakini nimshukuru sana sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na kwa hotuba yake aliyoitoa hapa Bungeni na Wasaidizi wake wote waliohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchangia mambo kama matatu ama manne kama muda utaniruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kabisa ni kilimo na mifugo. Kwenye kilimo, Jimbo la Njombe lina mazao mbalimbali lakini zao la kimkakati linalotambuliwa Kitaifa ni zao la chai, nami napenda kuliongelea zao hili kwa kuanza kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe. Kilio kikubwa kilikuwa ni bei na wananchi walikuwa wanalalamika sana kuhusiana na bei ya chai na nililiongea hapa, baada ya vikao vya wadau, Serikali ikiongozwa na Mheshimiwa Bashe, wameweza kufikia mahali ambapo hata kama siyo pale ambapo wananchi walipataka angalau sasa hivi bei ya kilo ya chai ilikuwa inauzwa shilingi 314 kwa kilo, imefika 366 kwa kilo. Walipenda sana ingefika 400 lakini uhalisia ndiyo huo, kwa hiyo tushukuru kwa hicho kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema wananchi hawa, wakulima hawa wanaweza wakapata hata hiyo shilingi 400 kwa sababu ukiweza kulima kwa ubora kuna malipo yanaitwa bonus payment, ukiweza kulima ukapata ubora ambao ni asilimia 68 unapata bonus payment ya Shilingi 90 kwa kila kilo. Ukilima ukapata ubora wa asilimia 75 unapata bonus ya karibu shilingi 112 kwa kila kilo, kwa hiyo uwezekano wa kufika 400 inawezekana, sasa ni nini ambacho kinaweza kikafanyika na Serikali na nitoe ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa hapa ni umwagiliaji, Serikali iliongeza bajeti ya kilimo hapa na sehemu kubwa ya bajeti hiyo ilikwenda kwenye maeneo ya umwagiliaji, lakini kwa masikitiko makubwa sana wakulima wa chai kwenye miradi ya umwagiliaji bado hawajaingizwa, hakuna kinachoendelea kwa wakulima wa chai kwenye upande wa umwagiliaji. Ninaomba Serikali iweze kuhakikisha kwamba hata wakulima wa chai wanaingizwa kwenye miradi. Miradi hii imeendelea kuwa kwenye scheme nyingine tu lakini kwa wakulima wa chai hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacho Kiwanda cha Chai pale kina–process chai kinaitwa Kabambe. Kiwanda kile kina capacity Kubwa lakini kinatishiwa kufungwa kwa sababu uwezo wa kuki-feed kiwanda ni mdogo. Wakulima wa chai wamejitahidi walipoweza kufika lakini bado hawawezi kufikisha na jambo linalozuia ukiacha suala la umwagiliaji ni suala la miundombinu wezeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana Serikali ilikubali kutoa fedha kutusaidia kwa upande wa barabara, lakini kwa masikitiko makubwa nipende kusema tuna tatizo kubwa sana la ujenzi wa barabara ambazo ziko chini ya TARURA. TARURA inatakiwa ijipange vizuri kuweza kusimamia Wakandarasi wajenge hizi barabara haswa za maeneo wezeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jinginje ninapenda kiliongelea kwenye mifugo ni kiwanda cha maziwa ambacho kipo katika Mji wa Njombe. Ninaongea kwa masikitiko makubwa sana kwenye kiwanda hiki, ni kiwanda pekee ukiacha viwanda vya avocado au parachichi kiwanda pekee ambacho kinakusanya maziwa, kiwanda hiki kilipata mkopo wa Benki ya Kilimo - TADB lakini kiwanda hiki kimefungwa kimesimama, niliomba hapa msaada wa Serikali uweze kuingilia mpaka leo haijaweza! Ninasikitishwa sana na ethical behavior na integrity ya TADB kwenye kushughulikia suala la kiwanda hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba wananchi wafugaji wana-own asilimia 30 ya kiwanda hiki, ungetegemea TADB wao wana jukumu la ku-promote na kusaidia wafugaji na wakulima, kwa hiyo wangeingia katika scheme ya kuasaidia hata kama wamekopa na kwamba fedha hazijarudishwa. Wananchi hawa kwanza TADB wao wenyewe wako responsible kwa default kwa kiasi kikubwa kwa sababu hawakutoa fedha kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TADB walichofanya kwa masikitiko makubwa, wamechukua madalali kwenda kuuza kile kiwanda na siku zote wanapeleka madalali karibu na sikukuu wakati watu hawapo, wameuza eneo la shamba lakini wameuza warehouse kwa milioni 500, kwenye kiwanda ambacho thamani yake ni bilioni 2.6 hii hakiubaliki na tunaomba Serikali iingilie kunusuru maisha ya wakulima hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tu nimesikia tena hapa baada ya kuuza jingo, TADB wamekwenda tena na dalali mwingine wanataka kuuza mashine! Nadhani TADB ilianzishwa kwa minajiri ya kuwasaidia wafugaji, wakulima ili waweze kujikomboa. Wakulima na wafugaji 1,000 wa sekta hii ya maziwa watakwisha maisha yao kabisa iwapo Serikali haitasaidia, siyo kwamba hawawezi kulipa hilo deni, mkakati wa kilipa hilo deni upo lakini TADB wana-interest na ndiyo maana nimesema ethical behavior ya TADB lazima iangaliwe, nina uhakika CAG ni eneo ambalo anatakiwa akaliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine napenda niliongelee ni eneo la usafiri wa anga. Mji wa Njombe kwa kweli tuna uhitaji mkubwa sana wa kuwa na kiwanja cha ndege. Napenda kuiomba sana Serikali iweze katika bajeti inayokuja iweze kuona hata kama hatutaweza kupata ujenzi wa kiwanja cha ndege upgrade ambayo inafanyika sehemu nyingine lakini kwa kuanzia angalau fedha ziwe allocated tuweze kuona eneo hili kubwa la uchumi linapata huduma ya usafiri wa anga wa uhakika. Tuna Wawekezaji wengi kwenye maeneo mengi, wangependa kuja katika kuwekeza katika Mkoa huu wa Njombe na Mji wa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipitisha sheria hapa ya Uwekezaji. Mimi napenda kuiongelea Sheria ya Uwekezaji wa harakaharaka. Wakati tunaongea hapa tuliiomba sana Serikali na ninashukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu ameongelea kwamba Serikali itaendelea kuangalia kuboresha mazingira ya biashara, pia itaendelea kuangalia sera zake kwa nia ya kuboresha. Moja ya maeneo ambayo tuliomba na ninaomba liendelee kuangaliwa kwa haraka ni kuangalia uwezekano wa kuona ni namna gani viwanda katika nchi yetu vinaweza vikapelekwa kwenye maeneo mengine kwa kuweka incentive scheme, tunaliomba hilo na tunaomba Serikali iendelee kuliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili watu wengi hatuliangalii kwa umakini, ni lazima tufanye mambo kwa mkakati tunaagiza ndege ya mizigo, hiyo ndege ya mizigo haitakuwa economical kama itakuwa inakwenda kuchukua mizigo tu ambayo ni ya kilimo na kupeleka sokoni. Inatakiwa iwe na mizigo mingine inayopeleka maeneo hayo na mizigo hiyo ukianzisha viiwanda na shughuli nyingine za kiuchumi ndipo unaweza kuifanya hii ndege iweze ku-add value katika maeneo yetu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa sekunde 30 malizia mchango wako.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapo na naunga mkono hoja. (Makofi)