Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nishukuru sana kwanza kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mchana huu kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa namna anavyoipigania nchi yetu na kupambana ili kuweza kuiweka kwenye mstari ulionyooka, hasa kwenye kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na kutoa huduma stahiki kwa wananchi, kuboresha masuala ya afya, miundombinu ya elimu pamoja na masuala ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pia pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri pia kwa namna ambavyo anatusimamia sisi kama Wabunge na anavyotuunganisha na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hapa ndani wote tuko kama Wabunge na ukitupima kwa madaraja Wabunge sisi wote tunafanana, ni daraja moja kwa sababu tumetokea huko chini kwa wananchi. Wajibu wetu wa kwanza kabisa ni kuismamia Serikali, na wajibu wa pili ni kuishauri Serikali pale tunapoona haifanyi kile ambacho sisi kama Wabunge au wananchi wetu wametuelekeza Serikali ikifanye. Wakati tunafanya mambo haya tunatakiwa kuangalia kuhusu uzalendo wetu na uwajibikaji wetu kwa Taifa kama namba moja lakini kwa wapiga kura na sehemu ya tatu tunatakiwa kuwajibika kwa chama chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pamoja na haya yote nitahakikisha kwanza ninalilinda Taifa langu kabla ya chama changu. Nitahakikisha ninawalinda wapiga kura wangu kabla ya chama changu halafu baadaye nitakilinda chama changu dhidi ya haya yote niliyoyataja hapo juu na ndipo nitapata ustawi sahihi na kuweza kuwasimamia na kuwaongoza watu wetu. Nayasema hayo, nataka nishauri Bunge lako na ikiwezekana lishawishike kwamba, kwa kadiri mambo yanavyokwenda tuna haja ya kubadilisha kanuni ili ripoti ya CAG ifanyiwe kazi na Bunge kabla hatujapitisha bajeti nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu zangu za msingi mojawapo kubwa ni kwamba, bajeti hii tunayokwenda kuipitisha ndiyo ile ambayo inalalamikiwa kwamba hapo nyuma pamefanyika ubadhirifu na kuna watu bado wataendelea kupelekewa fedha za Serikali wakiwa bado madarakani. Simaanishi kwamba tuijadili hii bajeti kwa sasa hivi, lakini kwa nia ya kubadilisha kanuni badala ya kusubiri mpaka mwezi wa kumi na moja ambayo itakuwa ni takriban miezi sita toka pesa mpya zilipopelekwa kwenye wizara tofauti ambazo nyingi zinalalamikiwa, watendaji wanalalamikiwa. Tumemsikia Mheshimiwa Rais naye akitaja baadhi ya watu kwamba wanalalamikiwa kwenye haya mambo. Kwa hiyo kimsingi ilitakiwa watu hawa kwanza wawajibike kabla hatujawapelekea pesa zingine ambazo inawezekana wakaenda kuzitumia kwa mtindo ule ule, kwa sababu watajua kwamba itakapofika Mwezi Novemba sisi kama Bunge tutajadili tutaweza kuondoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tubadilishe kidogo mtindo wa ufanyaji wetu wa kazi hasa inapokuja ripoti nzito kama hizi, kwa sababu kuna haja ya kujadili ripoti ya CAG na kuona mapungufu kabla hatujafanya location ya pesa zingine kwenye maeneo yale yale ambayo tayari kuna matobo makubwa ya matumizi mabaya ya pesa za wananchi. Ndio wale tuliosema tunawalinda, tunalinda Taifa lakini baadaye tunajilinda sisi wenyewe na tunataka tuone chama chetu kinaendelea kuongoza nchi hii, lakini haya lazima tuyasimamie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilipata nafasi ya kuuliza swali hapa asubuhi; nilikuwa naongea kuhusu barabara ya Nachingwea Masasi. Nakumbuka hapa Waziri wa Fedha alimpa taarifa Mbunge mwenzangu ambaye tunapakana kwenye eneo la mpaka wa Nachingwea. Kwamba mradi wa utekelezaji wa barabara kati ya Masasi na Nachingwea utatekelezwa hivi karibuni. Majibu ya Waziri kama umefatilia vizuri na kuyasikia hapa leo naye amesema upande wao wameshamaliza na taarifa hizi zimekwenda Wizara ya Fedha, ili sasa waweze kutengewa fedha ya utekelezaji wa mradi huu, lakini kimsingi hakuna kinachoendelea mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama watu wa Masasi, Nachingwea na huko hatujaona mobilization inafanyika pale, kwa hiyo tafsiri yake hilo jambo haliwezi kufanyika siku za karibuni. Wilaya ya Nachingwea ni wilaya ambayo inafanana karibia sawasawa kabisa na umri wa uhuru wa nchi yetu, haijawahi kupata barabara ya lami, haijawahi kuunganishwa na sehemu nyingine yoyote yenye lami. Ndiyo maana sisi tunapokaa hapa tunaongea tunashauriana tunaambiana kwamba tunataka Serikali ifanye haya mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ipo, majibu haya sisi tunayapokea na hii sio mara ya kwanza basi watueleze kama inashindikana sisi tumezoea kufanya michango kwenye baadhi ya maeneo. Tunachanga ili kujenga madarasa kuisaidia Serikali na sasa hivi nataka watuambie ili tukaweze kufanya michango sisi watu wa Mtwara, Lindi na Nachingwea tuweze kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo pamoja na barabara ya Mtwara, Mnivata-Newala, ambayo nayo ahadi zimekuwa nyingi. Newala- Masasi haijatekelezwa, hatuoni nini pale kinachoendelea pamoja na kwamba hivi karibuni wamelipa fidia lakini hii ya Nachingwea – Masasi ndio tatizo kabisa siku zote tunapewa majibu haya yanayofanana. Kwa hiyo tunaomba Serikali watuambie kama haipo kwenye bajeti yake inashindikana kwa sababu hatujui kilichofata hapo mbele basi sisi kama wananchi wa maeneo haya tuchangishane kwa kukata kwenye mazao yetu ya kilimo pamoja na korosho shilingi 20 ili tukajenge hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea kipande cha kilometa 42, Masasi-Nachingwea, lakini Wilaya ya Nachingwea ina zaidi ya umri wa miaka 60. Kwa hiyo Serikali kama hata ingeamua kujenga kilometa moja moja toka wakati huo, sasa hivi wangekuwa wameshaenda mbali zaidi ya Nachingwea na wanakaribia kufika Liwale. Kwa hiyo tutakapotoka hapa tutakwenda kuwashauri watu wetu kama inawezekana basi tuchangishane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba, Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha mpango wake alisema kwamba uchumi wetu unayumbayumba na kwamba inawezekana uchumi ukatoka kwenye asilimia 4.2 kwenda asilimia 3.9. Sababu zinazotajwa katika haya mambo ya kupanda kwa bei za vitu na mengine, ni pamoja na vita ya Ukraine pamoja na Russia pia na yale masuala ya covid. Sasa sisi kama Taifa mpango wetu ni nini? Tunayo miradi yetu mikubwa ya kimkakati tunayo suala la Liganga na Mchuchuma, suala la reli ya kusini, suala la Bandari ya Mtwara, tunayo haya mambo ya gesi ambayo hayatumiki ipasavyo tungeweza kuachana na sababu hizi ndogondogo za kiuchumi kwa sababu kama vita itaendelea kwa miaka 20 manake uchumi wetu bado utaendelea kudorora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka niombe, kwa sababu tuna taarifa za CAG, CAG akakague; na Mheshimiwa Mwenyekiti utaniongoza kuna hili suala la ETS tumelalamikia muda mwingi hapa kwamba ndiyo kati ya vitu ambavyo vinaongeza inflation kwenye bei za bidhaa mbalimbali. CAG sasa akakague na kuona kama tender hii ya ETS bei zilizopo na athari zilizopo kwenye soko atuletee taarifa hapa sisi kama Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka pia CAG akakague na kuangalia Mfuko wa Pembejeo. Ukija Mtwara kwenye zao letu la korosho kuna Mfuko wa Pembejeo wa Pamoja. Mfuko huu umeshafanya kazi zaidi ya miaka mitatu, lakini pia haupo kisheria, ndiyo tunataka CAG akakague atuletee hapa taarifa, kama Mfuko bado unatufaa sisi au kama haufai basi uondolewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tunataka kufanyiwa review kwa export levy, kodi inayotozwa kwenye masuala ya korosho. Pafanyiwe review pia katika tozo mbalimbali ambazo zinatozwa kwenye korosho, hela ya korosho kila mara inaanguka, wakulima wanapata hasara, makampuni yanapata hasara, uchumi wa maeneo yetu unadorora kwa sababu tunategemea zaidi zao la korosho, lakini watu wanashindwa kuja kununua kwa sababu ya tozo zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata sisi ziara ya kwenda kwenye nchi wanakozalisha korosho, nchi ambako wanatumia mfumo kama wa kwetu. Sisi Tanzania peke yake ndiyo tuna hizi kodi hapa tunazozitaja. Sasa ni wakati wa kuona kama ni kweli kodi hizi zinastahili ama kodi hizi hazistahili ili tuweze kwenda sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linaumiza sana wananchi ni masuala ya fidia kwenye maeneo mbalimbali. Kwenye Jimbo la Ndanda tuna mgogoro mkubwa sana na wa siku nyingi wa eneo kati ya Jeshi la Magereza pamoja na wananchi kwenye Kata ya Namajani kwenye Vijiji vya Ngalole pamoja na Chiroro na maeneo hayo. Toka mwaka 2012 Mahakama ilitoa award kwa wananchi na kuwaambia kwamba eneo lile lirudishwe kwa wananchi, Serikali haijafanya hivyo, magereza haijafanya hivyo. Katika bajeti hizi zote sijaona popote ambapo imetengwa fedha ya kwenda kuwapa wale wananchi fidia zao ili waweze kuachia hayo maeneo. Kwa hiyo kama Serikali imeshindwa, tutakapokuwa tunamaliza Bunge na tunakwenda kwenye Wizara ya Ardhi, watueleze ili tukawambie wananchi sasa wakalime kwenye yale maeneo yao, waachane na huu mpango wa Serikali kwa sababu hautaweza kutekelezeka karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la fidia pia. Barabara inayotokaa Nanganga inakwenda Ruangwa nyumbani kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, inakwenda pia na kuunganisha na Wilaya ya Nachingwea. Palibomolewa pale majumba ya wananchi wa kawaida, palibomolewa misikiti, lakini pamoja na Ofisi yetu ya Chama cha Mapinduzi, hakuna fidia iliyolipwa mpaka sasa hivi na wananchi wanapouliza Serikalini wanasema fungu la fidia lilikuwa halijaandaliwa. Tunaka tutakapokuwa tuna wind-up haya mambo basi tuweze kupata majibu ya pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nisisitize kwenye yale niliyoyasema kwamba kwa vyovyote vile tunahitaji uchunguzi wa kina wa kuona kama Mfuko huu wa Pembejeo unaosimamia Mikoa ya Mtwara, Lindi na maeneo yote wanayolima korosho bado uko viable na kwamba CAG akaukague tupate taarifa hapa kwa sababu itakuja ndani ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kama hayo niliyoyasema, kwa hiyo, naomba nisisitize kufanyike ukaguzi ili wananchi waweze kupata majibu na sisi kama Bunge tubadilishe Kanuni, tujadili taarifa ya CAG kabla hatujatenga pesa kwa bajeti inayofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana. (Makofi)