Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenipa afya na nguvu kuweza kuchangia katika Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nimpongeze Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni, iliyojaa matumaini makubwa sana ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Jimbo la Lushoto tumepata fedha nyingi sana za miradi. Mradi wa maji mpaka mabilioni ya fedha, mradi wa barabara tumepata mabilioni ya fedha. Mradi wa afya tumepata mabilioni ya fedha, elimu tumepata mabilioni ya fedha na miradi chungu nzima tumepata mabilioni ya fedha. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende katika kuchangia sasa baada ya pongezi hizo. Lushoto kuna barabara kuu moja tu ambayo inaingia Lushoto. Barabara hiyo inaanzia Mombo kupanda Soni hadi Lushoto Mjini ambayo ni kilometa 32. Barabara ile ni nyembamba sana na kila wakati naiongelea barabara hiyo katika Bunge lako tukufu hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike hatua sasa maneno haya au uchangiaji wangu huu ufike mwisho. Barabara hii ni nyembamba na inapelekea hata wafanyabiashara wa Lushoto vitu vinapanda bei kwa sababu gari inayoruhusiwa kupita katika barabara ile ni tani 10 tu siyo zaidi ya hapo.

Barabara hii hata Waziri Mkuu amepita na ameiona kwa hiyo niombe sasa katika bajeti hii, barabara ile itengewe fedha angalau itengenezwe hata kwa kilometa tano tano ili Wananchi wa Lushoto waondokane na adha hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo tuna barabara yetu mbadala namshukuru Rais wetu ametupa fedha za barabara ile ambayo inaanzia Dochi kupitia Ngulwi hadi Mombo ambayo ni kilometa 36 lakini bado fedha zile hazitoshi. Inatakiwa iongezwe fedha kwa sababu barabara hii ikitengenezwa itakuwa barabara mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, barabara hii naomba iende itoke TARURA iende TANROADS kwa sababu gani? Kwa sababu TARURA hawana mafungu ya dharura. Kwa hiyo, niombe sasa barabara hii itoke mwaka huu iweze kwenda TANROADS na Wananchi Lushoto waweze kupata barabara mbadala hata ile ya Soni – Mombo ikipata dharura basi wana barabara mbadala ya kupita kupeleka mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo niishukuru Serikali inatengeneza Barabara ya kutoka Magamba kwenda Mlola. Barabara ile inatengewa kila mwaka kilometa moja ambayo inagawanywa nusu kilometa kuelekea Mlalo na nusu kilometa kuelekea Mlola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sasa Serikali yako tukufu kwenye Bunge hili la Bajeti itengewe hata angalau kilometa 10 ili barabara iweze kwisha haraka wananchi wangu wa Jimbo la Lushoto au Wilaya ya Lushoto waweze kupata manufaa na barabara ile kwa sababu barabara ile ni ya kiuchumi na ukanda ule una mazao mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye suala la afya, niendelee kuipongeza Serikali inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutupa vituo vya afya zaidi ya viwili katika Jimbo la Lushoto lakini vituo hivyo viko Tarafa ya Mlola tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali niendelee kuipongeza lakini sasa bado kuna changamoto ya vituo vitatu vya afya. Mfano Kituo cha Afya Gare, tangia mwaka 2015 naongelea kituo kile cha afya lakini mpaka leo bado hakijatengewa fedha. Sambamba na hayo kuna Kituo cha Afya Kwai bado nacho hakijatengewa fedha. Sambamba na hayo bado kuna Kituo cha Afya Makanya nacho bado hakijatengewa fedha. Niiombe Serikali sasa awamu hii vituo hivi viweze kutengewa fedha ili viweze kufanya kazi na wananchi wangu waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye suala la elimu, niendelee kuipongeza Serikali inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan kwani fedha za booster zimefika na zimefanya mambo makubwa sana lakini bado kuna changamoto, Wilaya ya Lushoto ina shule nyingi sana. Shule za msingi za Wilaya ya Lushoto ni sawa sawa na Sekondari sawa sawa na Mkoa wa Katavi tena huenda zinazidi. Kwa hiyo, niiombe sasa Serikali iangalie kwa jicho la huruma shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Lushoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo kuna shule ambazo zina hadhi hata ya kuwa na kidato cha tano na cha sita. Mfano Shule ya Sekondari Masange Juu, naomba hii ipandishwe hadhi nayo iwe na kidato cha tano na cha sita. Lakini nayo Sekondari ya Magamba nayo iwe na kidato cha tano na cha sita kwani shule hizi watoto wanakaa mbali sana kwa hiyo, zikiwa shule za bweni naamini kabisa kuwa zitasaidia watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lingine ni suala la kilimo, Lushoto wakulima wengi ni wa mboga mboga na matunda lakini Mheshimiwa Bashe sijawahi kumsikia kwamba anatoa ruzuku kwenye mboga mboga na matunda wakati mboga mboga hizi na matunda ndiyo zinachangia pato kubwa la halmashauri. Kwa hiyo, niiombe sasa nayo bajeti hii ya mboga mboga na matunda basi ziingizwe kwenye bajeti nayo ipate pembejeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo kuna suala la VETA. Namshukuru Rais ametupa fedha zaidi ya Shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya Chuo cha VETA na chuo kile kimeisha lakini wananchi wanauliza; je, ni lini chuo kile kinafunguliwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, suala la mwisho ni kumwomba Mheshimiwa Bashe, nilimwomba chakula cha bei nafuu lakini Mheshimiwa Bashe viongozi wako au wataalamu wako mpaka leo hawajaniletea chakula kile. Nikuombe Mheshimiwa Bashe hebu lione hilo sasa Lushoto tuweze kuletewa chakula cha bei nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)