Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nakwenda kuzungumza mambo mawili tu na mambo haya mawili nayokwenda kuzungumza yapo katika level ya kitaifa kwa lengo la kuisaidia Serikali na kuwasaidia walipakodi ambao ni Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 7 Desemba, 2020, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kiongozi wetu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa uzalendo kwa kutanguliza maslahi mapana ya Taifa alitoa maelekezo kwa kuangalia namna gani Watanzania walipita katika msuko msuko mkubwa ambao ulipelekea kupanda kwa bei kubwa ya bidhaa katika Taifa letu ikiwemo bidhaa ya cement na bidhaa zingine. Tarehe 7 Desemba Waziri Mkuu alitoa maagizo ya kufanyika kwa study ambayo ingeweza kuleta majibu katika Taifa letu kwa nini Watanzania wamepata burden kubwa katika sekta ya ujenzi kwa sababu ya kupanda kwa bei ya cement katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikupe taarifa; Fair Competition Act Na. 8 ya mwaka 2003 section 5(1) imeeleza namna gani kampuni inaweza kuwa na market share katika Taifa letu katika uwekezaji wa aina yoyote katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikupe taarifa hata ninapozungumza hapa, aliyekuwa Waziri wa wakati huo Professor Kitila Mkumbo; ninakupongeza kwa sababu wewe pia ulitanguliza mbele maslahi ya nchi na nina imani hata mwalimu wangu aliyenifundisha Mzumbe University Mwalimu Dkt. Ashatu akipewa na yeye maelezo mazuri atakwenda kuyatanguliza maslahi mbele ya nchi, wataweza kuzishauri mamlaka za nchi kuhakikisha ya kwamba maslahi ya Watanzania, maslahi ya walipakodi yanalindwa dhidi ya ma- cartel ya kijambazi yanayochukua nafasi katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie, study iliyofanywa na vijana wazalendo wa Kitanzania waliosomeshwa na kodi za walalahoi wa Kitanzania. Study imeonyesha miunganiko ambayo Twiga Cement waliokuwa wanataka kumnunua Tanga Cement jambo la kwanza. Study zinaonyesha ilikuwa inakwenda ku-violate Fair Competition Act Na. 8 ya mwaka 2003 section 5(1) iliyopitishwa na Bunge hili tukufu kwa ajili ya kumlinda mwananchi mlalahoi kule mtaani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunapozungumza study imeonyesha gharama ya kutengeneza na kuzalisha mfuko mmoja wa cement kwenye taifa hili la Tanzania it is only 5,700 Tshs. Gharama ya kuzalisha mfuko mmoja wa cement ni shilingi 5,700. Kampuni ikiachwa ikauza kwa faida, bei ya cement kwenye Taifa letu hakuna namna bei ya cement inaweza ikazidi shilingi 8,700 na shilingi 9,000 lakini nini kinafanyika? Makampuni haya ya uzalishaji wa cement study zinaonyesha yanafanya kitu kinaitwa cartels zilizozungumzwa katika Fair Competition Act ambayo imepitishwa na Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikupe taarifa, cartel hizi tunazozizungumza nataka niwaambieni na ndiyo maana Wabunge nataka niwashawishi. Mna kazi kubwa sana kumwombea Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu huyu na Mawaziri ili wawe na moyo wa kizalendo wa kufanya maamuzi ya kizalendo. Mambo haya wanapambana na watu matajiri wakubwa, watu wenye fedha, vita hii bila kumtanguliza Mungu taifa hili Watanzania watakuwa wanageuka kushoto wanapigwa, wanageuka kulia wanapigwa mamiradi ya Serikali Mheshimiwa Rais juzi amelalamika anasema Engineer estimates zinakuwa kubwa. Miongoni mwa vyanzo vinavyosababisha nchi yetu inapata hasara ni kwenye study kama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza, Umoja wa Wazalisha Cement wa Afrika Mashariki kwa study wamegundulika wanakaa vikao, wanafanya market allocation, wanapanga bei za cement na ninataka nikwambie hata Bunge hili kuna wakati tunakuja tunapitisha vitu hapa maskini ya Mungu bila kuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza, research inaonyesha ukuaji wa Sekta ya Ujenzi umekua kwa 13% lakini nenda kwenye viwanda, uzalishaji wa cement umeongezeka only kwa 3% na hiyo percent ninayoizungumza ya 3% kwa 13% ambayo sekta inakua; viwanda vimezalisha 3% lakini capacity yake vinatakiwa vizalishe 50% na tulichokifanya kibaya zaidi tumekwenda tukapandisha bei ya importation ya cement kutoka 25% mpaka 35%. Tunamlinda nani wakati wazalishaji wa ndani only wanazalisha 3% ya maximum capacity ya uzalishaji wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya yanaumiza sana kwa mtu yeyote mzalendo anaelipenda Taifa lake hawezi kunyamaza akaacha kuzungumza mambo haya yanayofanyika kwenye Taifa hili. Hapa tunapozungumza, cement inauzwa shilingi 18,000. Study zimefanywa na watoto wetu wa Kitanzania waliosoma kwa kodi zetu. Study inaonyesha zote hizi zimefanyika na ni ma-cartel. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa ukimuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu hii ripoti toka taarifa imesemekana ripoti ifanyike, hii ripoti haijawahi kuwekwa hadharani. It has never been published in the public, umma uweze kuona namna gani viwanda vya cement vimetengeneza ma-cartel kwa kushirikiana na wasambazaji, kwa kushirikiana na wafanyabiashara kuwaibia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme neno moja, kama Bwana Mungu wetu aishivyo, Wabunge wazalendo hatutanyamazishwa kusema mambo yanayowaumiza Watanzania, mambo yanayoumiza watu wetu katika sekta nzima ya uzalishaji na hii inasababisha Serikali yetu inatekeleza grand project. Miradi ya SGR, miradi ya barabara, miradi ya ujenzi, gharama za ujenzi zinakuwa kubwa, nani wa kulihurumia hili taifa na kuwa na ujasiri wa kuyasema haya na ku-risk maisha yake? Nani wa kuwa na huo ujasiri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumza hapa ninajua hayo ma-cartel kule yananisikiliza. Yataanza kutengeneza hata njama, wanafanya hata njama wakati mwingine ku-silence kila sauti itakayosimama kuwatetea Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumza hapa study imefanywa na hawa vijana na ninakuomba Waziri wangu Mkuu Kassim Majaliwa kwa uzalendo ule ule ulioufanya kaka yangu ya kuagiza study ifanyike, tumia uzalendo ule ule tena itisha ripoti hii mtakuja kuniambia Serikali tukiamua kuwa serious haifiki mwezi wa sita hapa, bei ya saruji inapaswa kuwa chini ya shilingi 9,000 kuwasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninaomba nizungumze. Tumezungumza hapa kuhusiana na mambo ya kulinda maadili ya Taifa. Nchi hii haiwezi kuwa na prosperity kama tutaacha kulinda tunu za maadili ya kitaifa hili. Hii nchi yetu ni nchi iliyopata uhuru na sababu kubwa ya Mwalimu Nyerere kupigania uhuru wa Taifa hili ilikuwa taifa liwe huru liweze kulinda misingi yake iliyopelekea Taifa hili kuheshimiwa nyakati zote toka Taifa hili limepata uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa wito, Bunge letu kama chombo cha kutunga sheria na kusimamia Serikali ninatoa wito kwa mahakama zetu za Taifa hili, ninatoa wito kwa viongozi wa dini zote. Katika Biblia katika imani yangu, neno la Mungu linasema; “Mungu wetu huwa hadhihakiwi.” Pia neno la Mungu katika kitabu kitabu kitakatifu Biblia inasema, “Mungu wetu huwa siyo Mungu wa Kujaribiwa kwa sababu yeye ni Mungu mwenye uwezo na mamlaka.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa wito kwa Serikali, kwa sababu hata haya ma-NGO tunayoyaona ambayo yanasababisha kuharibu maadili ya watoto ukiangalia yamesajiliwa na Serikali yetu hii hii ambayo tunazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawezaje tukasema tunalinda hizi haki za watoto kama tutashindwa Serikali kuhakikisha kwamba tunajenga platform na mazingira ambayo yatampa Mungu heshima na tukampa Mungu wetu utukufu ili Taifa letu liendelee kubarikiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa wito kwa Serikali, ninawaomba sana lindeni vizazi vyetu, walindeni watoto wetu wa Kitanzania kwa kuhakikisha kwamba jambo lolote ambalo litakuja ku-contravene na misingi ya Taifa hili inakwenda kudhibitiwa kwa maslahi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kama utaniruhusu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, ahsante sana kwa mchango wako.