Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri sana ambayo ameiwasilisha ndani ya Bunge letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la tathmini zinazofanywa na baadhi ya watendaji kwa vitisho kwa wananchi wetu. Hivi karibuni, mwaka jana 2022 kwenye suala hili la ujenzi wa Reli ya SGR, route tatu katika Mkoa wetu wa Tabora. Jana niliuliza hapa swali la nyongeza kuhusiana na malipo yao, lakini wakati naliuliza nilisema, pamoja na fedha kidogo ambayo wameambiwa watalipwa lakini bado fedha hii imecheleweshwa kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona leo nilizungumze jambo hili ili liweze kuwekwa sawa. Watendaji hawa walipofika kufanya tathmini ya maeneo ya wananchi wetu hususan katika Manispaa ya Tabora, Eneo la Ndevelwa, watu hawa wamepimiwa maeneo yao, square mita zilizopatikana eti kila square mita moja Shilingi 800. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia ya sasa, nchi yetu hii sasa kuna ardhi unaweza kununua square mita kwa Shilingi 800? Hawa watu wana hati, wamesajiliwa, wanajulikana, ni maeneo ambayo ni mapya, hawakukataa kupisha mradi huu kwa sababu ya uzalendo wao. Walisema mradi huu upitishwe, tunahitaji maendeleo ya Wana-Tabora lakini walipwe stahiki zao sahihi. Kwa akili ya kawaida haiwezekani, mtu mwenye square mita 500 anakwenda kulipa shilingi 400,000 wakati leo ukiigusa ardhi Tabora Mjini, huna milioni mbili hupati eneo la kujenga nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu unaenda kumlipa shilingi 400,000 aipeleke wapi? Kwa nini tunataka kuifanya Serikali ionekane haijali wananchi wake, na hasa kwa kipindi hiki ambacho Mama Samia anaongoza ambaye ni mwanamke mwenzetu? Hatutaki jambo hilo litokee, lakini naomba niliseme, tena nalisema kwa machungu makubwa na kwa ukali. Haiwezekani, na kwenye nchi hii na kwenye Taifa hili kuwalipa watu shilingi 800 kwa square mita moja, haiwezekani Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Ofisi ya Waziri Mkuu, jambo hili Mheshimiwa Waziri Jenista na watu wako, tunaomba mwasaidie wananchi wetu ni masikini. Haiwezekani, nendeni mkaone mjue. Tunaumia sisi viongozi wao. Unamlipa mtu shilingi 800! Cha kusikitisha, ninao mfano mmoja hapa, kuna mtu mmoja kalipwa shilingi 350 kwa square mita moja. Huyu mwananchi ana square mita 4,643. Huo ni ukubwa wa eneo lake. Malipo alioyoandikiwa kulipwa, bado hawajalipwa maana yake, hapa nazungumza ni zaidi ya mwaka sasa umepita bado malipo hayo hawajalipwa, atalipwa shilingi 1,639,050. Hayo ni malipo ya fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye kila square mita moja ukipiga hesabu na humu ndani kuna wanamahesabu, kila square mita moja ni Shilingi 350/=. Jamani, sisi watu wa Tabora ni wapole sana, ni wastaarabu, ni wakarimu, lakini msichukulie advantage upole wetu na ustaarabu wetu kutufanyia haya. Yanaumiza! Hivi leo maeneo haya yangekuwa ni yetu sisi viongozi, tungekubali kweli kulipwa kiasi hiki! Mtu ana hati tayari, mtu ana kila kitu tayari ameshaweka pale, anasubiri mji upangwe ili aweze kufanya maendeleo yake kwenye eneo lake! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi umepita mkubwa tumekubali, lakini leo inakuwa ni dhahama sasa! Badala ya raha ya kusema kwamba nataka mradi upite, wananchi wananung’unika, wanasikitika, tutapata wapi baraka? Hii ni dhuluma, siyo haki. Ni lazima Serikali iangalie jambo hili jamani. Hata kama haliwezekani, liangalieni jambo hili mwasaidie hawa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Mwakibete amelifuatilia jambo hili angalau hiyo amount ndogo ambayo wameandikiwa, Mheshimiwa Mwakibete ameisimamia angalau walipwe kwanza, kama kuna mambo mengine yatafuata. Waheshimiwa Waziri ninyi ni viongozi wenzetu, ni wazazi, mna ndugu, mna jamaa, na marafiki, kwa fedha hii tunaomba watusaidie tafadhali watu hawa waweze kulipwa stahiki zao kwa mujibu wa eneo na maeneo yao. Shilingi 800/= haiwezi kutosha. Yaani kwa kweli naongea kwa uchungu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusiana na hili suala zima la shule kongwe. Hili suala la shule kongwe limekuwa linazungumzwa tu juu juu. Sisi wananchi wa Tabora tunazo shule maarufu kongwe Tabora Mjini pale. Kuna Shule ya Tabora Boys, kuna Shule ya Tabora Girls. Shule hizi zimetoa watu maarufu na wengine wamo humu ndani. Wengine ni viongozi wakubwa kwenye Taifa hili, lakini kizuri zaidi, Shule ya Tabora Boys Baba wa Taifa, amesoma pale. Ukiona shule zile na hali iliyopo ni aibu hata kusema shule hii amesoma Baba wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali inatuambia tutoe fedha za mapato ya ndani kwenda kufanya ukarabati wa shule hizi, jamani mnatuonea! Hebu saidieni shule hizi za kihistoria ziweze kuwa shule bora. Unapofika pale Tabora, unasema naenda Tabora Boys, hilo geti lenyewe linavyokuitikia, aibu! Halina hata mvuto! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo kwenye Kamati ya LAAC, tumepita juzi pale. Tunashukuru wafadhili wametusaidia kutengeneza mabweni, wameyakarabati. Tumeingia mpaka chumba cha Baba wa Taifa alicholala, tumekiona, lakini nenda kwenye bwalo, nenda kwenye majengo mengine, ni aibu! Shule ya Tabora Girls kuna watoto wetu wa kike, hata fence tu haina. Wanaume wakware wanapita pale na magari yao kujionesha, kufanyaje, wanawakonyeza watoto wetu, wanawaharabia masomo yao. Wajengewe angalau fence pale kwanza ili watoto wetu waweze kusoma kwa amani na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa dakika chache ulizonipatia. (Makofi)