Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninakushukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya hasa ukilinganisha kwenye Jimbo langu la Mtwara Mjini iko miradi ya mfano ya mabilioni ya shilingi ambayo yanaendelea sasa hivi kufanyika, ni vema nikamshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Makamu wa Rais Mheshimiwa Isdory Mpango, nimshukuru Waziri Mkuu na hapa nigande kidogo niseme kwamba, Waziri Mkuu nakushukuru sana kwa mambo mengi ambayo umekuwa unanishauri, unanisaidia kwenye Jimbo langu kwa kweli nakutakia kila la kheri Mwenyezi Mungu akubaliki sana. Pia kwenye shughuli ya Mwenge Mheshimiwa Waziri Mkuu umetutendea haki Wananchi wa Mtwara, kwa hiyo tunakupa pongezi la Wanamtwara wamenipa salamu tukuambie kwamba wanakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo zaidi ya matatu ya kuzungumza. Jambo la kwanza tunazungumza uchumi ndani ya nchi yetu, tunapozungumza uchumi ndani ya nchi yetu hatuwezi kuwa na uchumi ambao ni bora kama hatutakuwa na viwanda ndani ya nchi. Nimeona nilizungumze hili tukiangalia zone ya Mtwara na Lindi ni watu ambao tunazalisha au tuna maeneo mengi ya madini lakini madini haya yana uwezo wa kutengeneza gypsum yana uwezo wa kutengeneza zana za aina nyingi za ujenzi. Ninaishauri Serikali muda sasa umefika kwa sababu material haya tusifike mahala tukawa tunayatumia vibaya, material haya kama tungefika sehemu tukawaleta wawekezaji wakaweka viwanda, nadhani tungepiga hatua kiuchumi na hata vijana wetu wangepata ajira za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo ambalo mara nyingi sana nimekuwa nazungumza kwenye Bunge hili lako Tukufu, inawezekana ninaeleweka au nisieleweke hata hivyo Wabunge wanzangu naomba kwa hili mni-support. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara tulikuwa na mpango wa Mtwara Corridor na hii Mtwara corridor package yake tunazungumza bandari, tunazungumza airport, tunazungumza na reli ya Liganga na Mchuchuma, Mbamba Bay. Nimesikiliza taarifa hapa na ripoti ya Waziri Mkuu sijasikia masuala ya Reli ya Mtwara Mbamba Bay. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumefika eneo Serikali tumewekeza bilioni 157 kwenye Bandari ya Mtwara na ninadhani uwekezaji ule umewekezwa kwa ajili ya kufungua njia na fursa za kiuchumi, ni vyema sasa nikaishauri Serikali kwamba mpango wa kutujengea reli bado ubaki palepale na jitihada ziongezeke ili reli tupate ya Mtwara Mbamba Bay. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ujenzi wa daraja, kwanza ninaishukuru Serikali mlitujengea daraja kule Mtambaswala, tunachozungumza kuhusu daraja na Mto Ruvuma tunazungumza mileage na hasa kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara Mjini kuna kiwanda cha Dangote kiwanda hiki kinapeleka cement mpaka Katavi, lakini kiwanda hiki hakina uwezo wa kupeleka cement Pemba, Mozambique na maeneo mengine kwa sababu ya mileage. Hoja yetu Wanamtwara tunasema mtufungulie daraja pale Kilambo, kutoka Mtwara Mjini mpaka unaingia Kilambo ni kilometa 70, ukitoka Kilambo mpaka unaingia Mocimboa da Praia Wilaya ya kwanza ya Mozambique pana kilometa 56. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mmoja tu, leo Waziri wa Uchukuzi alitembelea kwenye Bandari ya Mtwara akakuta kuna bomba nyingi ambazo zinakwenda Mozambique ambazo zile bomba ni za watu ambao wanakwenda kushughulika na masuala ya gesi Mozambique, lakini bandari yao ambayo wanaona ni karibu kuitumia ni Bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bomba zile ni mwaka wa pili sasa zipo bandarini hazina uwezo wa kwenda Mozambique, kwa sababu njia ambayo ipo ambayo tungeweza kuitumia, mileage zinawakataa na gharama ni kubwa sana. Sasa naomba, leo tunaizungumzia Dangote kama Dangote, mfanyabiashara mmoja mkubwa sana. Cement mfuko mmoja TRA wanachukua zaidi ya shilingi 3,000, lakini cement ya Mozambique mfuko mmoja kwa hela ya kwetu ni shilingi 35,000 kwa hela ya Tanzania. Dangote anasema kama daraja hili litapitika, nitauza cement kwa shilingi 16,000. Tunakwenda sasa kufanya biashara kubwa na TRA ya Mtwara kiujumla itakuwa imepata mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme suala hili halihitaji kuwepo na profesa, halihitaji mtu awe na degree kwenye ufahamu wa suala hili. Tumsaidie Rais. Rais wetu sasa halali usiku na mchana anahaingaika kuona ni jinsi gani Tanzania ataifikisha pale wanapohitaji Watanzania. Tunakaa humu tunahangaika na ushuru wa PP, ushuru sijui wa mbaazi, wakati item tunazo wenyewe za kuzitengeneza tukapata fedha kwenye Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuliotembea tumekwenda India juzi juzi, tumeona kule sekta binafsi wanatengeneza madaraja, nchi inafunguka, wanatengeneza reli, nchi zinafunguka, hapa tunaogopa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu vingine kwa kweli hata kuvisema vinaleta simanzi ndani ya Bunge letu hili. Mtwara ni sehemu ya Tanzania, lakini mfano mmoja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwezi mmoja na nusu uliopita alikuwa anakwenda Lindi, wananchi wa Mtwara wamemsubiri kuanzia saa 2:00 alivyopita pale mpaka saa 10:00 wako juani, wanamsubiri Rais wao kwa mapenzi makubwa. Sasa hili siyo kwamba ni suala la Mbunge, maana leo kuna hoja zinaongelewa, suala hili ni la Mbunge. Suala hili siyo la Mbunge, ni la kitaifa. Tunapozungumzia kufungua mipaka, tunazungumzia fursa za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili mimi nilitaka nilizungumze kwa mapana na marefu sana. Tunaomba wenye mamlaka mtusaidie. Mimi nimekwenda mbali zaidi, tumewasiliana na wenzetu wa Mozambique, sisi ndio majirani, wanasema sisi tuko tayari, ni suala la Waziri wa Fedha, Waziri wa Uchukuzi, sawa bwana, tuangalie ni mpango gani tunaweza tukaenda tukamaliza hii fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya mambo ni ya msingi sana, lakini kuna suala moja la mwisho nalotaka niliseme…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mtenga, na muda wako umeisha. (Makofi)

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)