Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Niwapongeze Serikali yetu ambayo iko chini ya Rais wetu Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambazo zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukiwa kwenye Kamati tulitembelea Mradi wa Ujenzi wa Meli ya Kisasa ya MV Mwanza Hapa Kazi tu. Katika maelezo tuliyopewa na Wakandarasi, tuliambiwa ujenzi wa meli unatumia chuma zaidi ya asilimia 60. Chuma chenyewe ambacho kinajenga meli yetu ya kisasa ambayo itaigharimu Serikali yetu zaidi ya shilingi bilioni 108 kinaagizwa kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia gharama ya ujenzi wa meli, bilioni 108, kama tungekuwa na mkakati wa dhati wa kuchimba chuma chetu cha Liganga na Mchuchuma ina maana zaidi ya shilingi bilioni 64 zingebaki hopa nchini, zingechochea uchumi na zingeongeza ajira. Niishauri Serikali yangu suala la kuchimba chuma cha Liganga na Mchuchuma nadhani kwa sasa hatuhitaji mjadala mpana zaidi, ni suala ambalo lazima tulifanye kama tunataka kujenga uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa kanda ya Ziwa suala la meli ni suala la siasa ni suala la uchumi. Tunaishukuru Serikali kwa meli hiyo na tunamwombea Rais wetu na Mtendaji wetu Mkuu Waziri Mkuu wetu, wasukume kuhakikisha kwamba hiyo meli imekamilika na twende kuitumia kwa ajili ya uchumi wa kanda ya ziwa na Taifa letu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Hotuba ya Waziri Mkuu ameongelea huduma kwa wazee. Kuna wachangiaji wameongelea wazee ambao ni wastaafu lakini tuna wazee ambao walitumikia Taifa hili katika nyadhifa mbalimbali. Vile vile, tuna wazee kama baba yangu ambaye alikuwa mkulima akizalisha kahawa ikiuzwa na kuchangia pato la Taifa. Hao wazee ni wengi na kusema kweli nimesoma hotuba ya Waziri Mkuu amewaongelea, lakini tatizo kubwa la wazee wetu wanahitaji na wao kutambuliwa. Kwa kutambuliwa huko hawahitaji tuwatambue kwa maneno, wanataka na wenyewe watambuliwe kwa kupewa ka- pension hata kama ni kadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewasahau sana hawa wazee wetu, wanahangaika, wanateseka, tunataka yanayotendeka Zanzibar, kama Zanzibar wanaweza wakawapa pension hawa wazee ambao hawakuwa wafanyakazi wa Serikali, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na wazee wa Tanzania Bara tuwaangalie. Ni wazee ambao wametulea, wametumikia Taifa hili katika nyanja mbalimbali kilimo, uvuvi, ufugaji naomba tuwape heshima yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza wachangiaji wengi hapa tangu hotuba ya Waziri Mkuu tuanze kuichangia wachangiaji wengi wameongelea migogoro ya ardhi kati ya Taasisi za Serikali na wanavijiji na wananchi kwa ujumla. Kama tutapata majanga mbele ya safari matatizo haya yatatokana na umiliki wa ardhi tusipochukua hatua leo. Wachangiaji leo asubuhi alianza Mheshimiwa Ezra, jana tulikuwa na Mheshimiwa hapa Ndugu yangu Mheshimiwa Kwezi anaongelea kwao Sikonge kule, kila sehemu kuna matatizo makubwa sana ya ardhi na matatizo mengi unakuta ni kati ya Taasisi ya Umma aidha Hifadhi ya Misitu au NARCO ni matatizo ambayo yanasababishwa moja kwa moja na Serikali yenyewe au Taasisi zake, matatizo ya namna hiyo lazima tuchukue hatua za haraka sana kukabiliana nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana niliongelea suala la Mwisa hapa na Kaka yangu Mheshimiwa Mwijage ameongelea Rutoro, tunaongelea vijiji ambavyo vimesajiliwa kisheria, Taasisi ya Serikali inakuja kwenye hivyo vijiji kwa mantiki hiyo NARCO wanapima vitalu kwenye ardhi ya vijiji ambavyo vimesajiliwa kisheria na wanagawa hivyo vitalu wanamwachia mtu ambae amepewa kitalu kazi ya kuhamisha wananchi, hii haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatengeneza ukaburu mwingine, mwenye pesa mpishe na ukishakuwa kwenye vile vijiji mtu anakuja anakuhamisha hakuna chochote anachoondoka nacho. Hili tatizo lazima tutafute suluhu vinginevyo tutasabaisha matatizo makubwa kwa wananchi wetu na zaidi wananchi maskini, hawa ndiyo kazi kubwa ya Serikali ni kuwatetea na kuhakikisha kwamba wanaishi na wanapewa heshima kama wananchi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwisa ambayo ipo Muleba, wakati naingia kwenye Ubunge niliambiwa ni hekta 133,000 ni eneo kubwa sana ambalo kwa Wilaya ya Muleba na Mkoa wa Kagera lile eneo ndilo linazalisha chakula cha kulisha Wilaya ya Muleba. Watu wakaja pale kwenye ardhi ya vijiji vya wananchi wakapima vitalu, sasa wanataka waondoe wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa ukiondoa wananchi hilo eneo kutokana na ukubwa wake, linapakana na Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato na upande wa Magharibi kuna Ziwa Burigi lazima tuangalie na masuala ya ekolojia ya lile eneo, ukishawaondoa misitu itakatwa tutatengeneza jangwa lakini kikubwa zaidi lile eneo ndilo linalisha Wilaya ya Muleba na Mikoa Jirani, tutatengeneza baa la njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu na kuishauri lile eneo badala ya kupima vitalu twendeni tukalipime upya, tukatenge maeneo ya kilimo, tukatenge maeneo ya ufugaji tukatenge maeneo ya makazi ya wananchi, eneo ni kubwa hatuna haja ya kugombana gombana na watu hapa ni suala la kufanya matumizi bora ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho lile eneo ni eneo la Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, siyo suala la sijui la mifugo Hapana! hatujawahi kufanya taratibu za kisheria za kuhaulisha lile eneo kutoka kwenye miliki ya Hamlashauri ya Wilaya ya Muleba kulileta kwenye Wizara nyingine yoyote Hapana! Hapa tunavyoongea naishukuru Serikali yangu wameshatupa mpaka na Hati za Vijiji vimesajiriwa na havijawahi kufutwa huyu NARCO anatoka wapi? Mamlaka kapewa na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa tumekuwa tukicheza na namba, leo hekta 130, kesho hekta 76 leo naambiwa ni hekta 43 hizi nyingine zimeenda wapi? Ndiyo maana naishauri Serikali tukapime lile eneo upya tujue lina ukubwa kiasi gani tukapange matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho. Sasa hivi tupo kwenye mfumo wa mavuno ya kahawa Kagera, nashukuru Waziri mkuu amefanya kazi nzuri na natumaini ataendelea kutufanyia kazi nzuri na nimeongea naye juzi hapa, tunaomba sasa msimu unapoanza wakulima wapewe ili vyama vya msingi vianze kununua kahawa yetu mapema, Mheshimiwa Bashe naona ameniangalia pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukimbiana wakulima eti kahawa ni magendo, katika nchi ya Tanzania kati ya Kata na Kata naomba mwaka huu nitafurahi nisipo lisikia. Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Bashe uliniambia, ulisema kahawa ni mali mkulima siyo mali ya Serikali, inakuwa mali ya Serikali pale ambapo imenunuliwa kutoka kwa mkulima imeingizwa kwenye maghala itakuwa mali ya Serikali. Sikubaliani na magendo ya kutorosha kahawa kuipeleka nje ya nchi kwa sababu tutakuwa tunakosa kodi, lakini biashara ndogondogo za humo kwa humo kati ya Kijiji na Kijiji, Kata na Kata tuwaruhusu wakulima wakauze kahawa yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana tunaendelea na kazi ya kusafirisha abiria wetu Mkoa wa Kagera. Niliongea mwaka jana na nalirudia na litakuwa la mwisho na nitaendelea kulisema kwamba Uwanja wa Ndege wa Mkajunguti ni suala ambalo haliepukiki kwa sasa kutokana na wingi wa abiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi niliongelea suala la kiwanda cha Kahawa cha TANICA, kiwanda hiki kina miliki kati ya Serikali na Vyama vya Msingi, lakini kile kiwanda hakiwezi kuzalisha kwa uwezo wake na Kagera tunazalisha kahawa, kile kiwanda ndiyo kiwanda pekee ambacho kinaweza kutusaidia ku-process kahawa inayozalishwa Kagera ninakuomba Serikali itupatie mtaji wa kutosha ili kiwanda hiki kiweze kuzalisha at full capacity, sasa hivi kinazalisha under five percent sasa kiwanda gani hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa ipo tunakimbizana na wauza kahawa, sasa hivi wanapeleka Uganda sijui wapi? Ni kwa sababu tumeshindwa kuingiza mtaji katika kile kiwanda. Serikali inaweza ikanunua zile hisa ambazo haijanunua mpaka leo ni Bilioni 8.6 ni hela ndogo! Mheshimiwa Bashe una hela nyingi na hicho kiwanda kipo chini ya Wizara yako, hebu tupeni hiyo hela tukaiongeze mtaji, tunanunulie teknolojia mpya tuweze kuzalisha, itakusaidia wewe na itatusaidia vijana wetu ambao mnawapa mtaji ili waweze kuzalisha lakini itaajiri vijana wetu na kuongeza pesa ya kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga hoja mkono na niwatakie mfungo mwema. (Makofi)