Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwapongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri. Ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 21 na 22, ningependa kujikita hasa kwenye kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuboresha mazingira ya wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Mwambe aliomba Mwongozo asubuhi, lakini napenda nikazie hapo kwenye suala zima la kuboresha mazingira ya biashara na mazingira ya wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimuundo na kimfumo Serikali imejipanga vizuri sana kuhakikisha inawalinda wafanyabiashara wanaoendelea kufanya kazi na kuwakuza wafanyabiashara wadogo waweze kuingia sokoni na kushindana kiushindani. Kimuundo Serikali imeweka Tume ya Ushindani wa Kibiashara ambapo mtu yeyote anapodhani kwamba hapendezwi au hafurahishwi na mwenendo wa biashara sokoni kwa washindani wake, anaweza kwenda kupeleka malalamiko au anaweza kwenda kufanyiwa tathimini. Kama hataridhika shauri lake litapelekwa kwenye Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna jambo ambalo kidogo linaendelea ambalo linaweza kuleta shida kubwa sana ya biashara ya saruji nchini. Mwaka 2022 Kampuni ya Twiga Cement iliomba kwenda kununua hisa ya kampuni ya Tanga Cement. Baada ya kuomba Tume ya Ushindani ilikwenda kufanya tathimini kama sehemu ya majukumu yake. Kwa sababu moja kati ya sifa kubwa ya kuweza kununua hisa za kampuni nyingine ambayo mnafanya biashara inayofanana, hautakiwi kununua hisa kwa zaidi ya asilimia 34 ili usije ukalimiliki soko la biashara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tathmini ilipofanyika ya hisa za Tanga Cement kununuliwa na Twiga Cement ilionekana kuna uwezekano mkubwa baada ya kununua hisa zile, Kampuni ya Twiga Cement ingeweza kumiliki hisa zile zaidi ya asilimia 68. Pia Tume ikasema kwa hatari hiyo itaifanya Kampuni ya Twiga Cement kuwa kubwa iweze kumiliki lile soko, jambo ambalo lingeweza kuleta madhara kwenye upangaji wa bei kwa sababu yeye ndio mdau mkubwa kwenye eneo hilo. Ingeleta madhara makubwa kwenye upangaji wa bei, ingeleta madhara makubwa kwenye mfumuko wa bei lakini ingeleta gharama kubwa kwa mlaji ambao ni wanunuzi wa saruji yaani sisi wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi yale yalipotoka hawakuridhika nayo, wakaenda kwenye Mahakama. Mahakama ikakubaliana na maamuzi ya Tume wakasema Hapana, wasipewe kwa sababu watalimiliki soko la cement nchini, jambo ambalo linaweza likaleta madhara makubwa kwenye uchumi wa nchi hasa katika eneo la cement. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Tume imesema, kama Mahakama imeamua, juzi tarehe 23 Februari hapa, Tume imetangaza kwamba Twiga Cement wataendelea kununua hisa za Tanga Cement, maamuzi hayo wanayapata wapi? Nguvu hiyo wanaitoa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madhara makubwa sana. Unajua mpaka sasa hivi tunapozungumza pamoja na viwanda vya cement kuwa vingi, bidhaa ya cement ina bei ya juu sana nchini. Kuna watu wananunua cement mpaka …

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi.

MHE. ELIBARIKI KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kingu hapa.

MWENYEKITI: Haya Mheshimiwa Kingu utachangia muda si mrefu. Naomba u-reserve hiyo taarifa. Endelea Mheshimiwa Salome Makamba.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Yapo madhara makubwa sana ya mmiliki mmoja kuwa na uwezo mkubwa wa kuamua bei, kuwa na uwezo mkubwa wa kupanga manunuzi na usafirishaji wa bidhaa ya cement hasa kwa wakati huu ambao nchi ndio inakwenda kujijenga kwenye maeneo ya viwanda, biashara na pesa nyingi za Serikali zinakwenda kwenye miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo inasimamia masuala haya ya uwekezaji, wajaribu ku- kulisimamia hili suala, kwa sababu mwisho wa siku mfumuko wa bei ukitokea kwenye cement, madhara ni yale yale ambayo tuliyaona kwenye sukari, kwenye mafuta ya kula na mambo mengine. Kwa hiyo ningeiomba sana Wizara itusaidie, ilimradi maamuzi yameshatolewa na Mahakama njia pekee ambayo Twiga Cement au haya makampuni yanaweza kufanya ili kumilikishana share ni kuomba marejeo ya maamuzi ya Mahakama ya Ushindani na sio kwenda kufanya ambavyo wanafanya. Kwa hiyo, naamini Serikali makini itakwenda kulisimamia hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nirudi kwangu Mkoa wa Shinyanga. Kitakwimu Mkoa wa Shinyanga unaongoza kwenye unyanyasaji wa kijinsia, mimba za utotoni na ndoa za utotoni. Ningeomba sana Ofisi ya Waziri Mkuu waifanye Shinyanga kama kanda maalum kwa ajili ya kutekeleza jambo hili. Asilimia 59 ya watoto waliopo Shinyanga wanaolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 na sielewi ni kwa nini Serikali imeamua kutumia nguvu yake kwenda kulirudisha nyuma suala la ndoa za utotoni ambalo limekwishaamuliwa na Mahakama kwamba tuletewe humu tubadilishe sheria, eti sasa hivi wanaenda kukusanya maoni ya wadau. Hii inaonesha ni jinsi gani sisi hatuko serious. Walete Sheria hapa tubadilishe na kama wanadhani kuna utaratibu umekiukwa au umekosewa tutajadili humu Bungeni hili ndilo jumba la Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha asilimia 44 ya wanawake walioko Shinyanga wananyanyaswa ndani ya ndoa zao. Manyanyaso mengi na ukatili mwingi wa kijinsia sasa hivi uko kwenye ndoa. Mwanaume anampiga mke wake anasema yule nikimpelekea kitenge na kanga atakausha hawezi Kwenda kulalamika. Manyanyaso mengi yanatokea ndani ya ndoa, Shinyanga hali ni mbaya. Ndoa za utotoni zimekithiri, mimba za utotoni zimekithiri, unyanyasaji wa kijinsia na sio wanawake tu. Ripoti iliyotoka mwaka 2022, walioripoti unyanyasaji wa kijinsia 42,245 walikuwa ni wananwake na 5,774 walikuwa ni wanaume. Kwa hiyo unyanyasaji uko pande zote mbili, elimu inatakiwa itolewe, kuweka dawati la jinsia peke yake haitoshi. Tuweke awareness kwenye jamii, tutoe elimu na watu wachukuliwe hatua. Mila na desturi mbovu ndizo zinafanya wanawake na watoto washindwe kuripoti mambo haya ya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili wa kijinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali kama ambavyo kuna baadhi ya maeneo yamewekewa kanda maalum kwa sababu za kiusalama na Shinyanga iwekewe Kanda maalum kwa sababu ya unyanyasaji wa kijinsia. Kwa sababu ikitoka Shinyanga inafuata Tabora, ikitoka Tabora wanafuata wenzetu wa Mkoa wa Mara, unyanyasaji wa kijinsia kwa Kanda ya Ziwa hali ni mbaya sana na inachagizwa na mila potofu, utamaduni mbovu, kutokuelewa ambapo wananchi wengi bado wako kwenye hii changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)