Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote nipende kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri, hotuba ambayo inaonesha ni kwa jinsi gani Serikali yetu imepiga hatua katika kuleta maendeleo lakini vile vile kuweza kuwasaidia wananchi wake kupata uhuru wa kutosha wa kiuchumi na masuala mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na vile vile nisimame hapa kwa niaba ya Jimbo la Kinondoni na wananchi wa Jimbo la Kinondoni niweze kumshukuru sana na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa yale ambayo ametufanyia sisi wananchi wa Kinondoni. Kinondoni tumepata maendeleo makubwa sana ndani ya kipindi cha miaka miwili. Naamini wengi mlioko humu ndani katika Bunge hili mnaishi au mna ndugu pale Kinondoni; na kwa hali hiyo mnapita na mnaona ni jinsi gani Kinondoni imechangamka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano maeneo mawili au matatu. Kwa mfano kwenye Kata ya Kinondoni ambapo ndiyo kata iliyochukua jina la Jimbo na jina la Wilaya; kata ile katika miaka 60 ya uhuru wetu haijawahi kuwa na secondary school ya Serikali lakini safari hii tumepata secondary school ya Serikali ya kisasa na watoto wameshaanza kusoma. Vilevile pale hatujawahi kuwa na kituo cha afya wala dispensary. Kinondoni sasa hivi ina kituo cha afya cha kisasa ambacho kimejengwa na Serikali na kinapendeza na kina huduma zote, nipende kuishukuru Serikali kwa ajili hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna barabara nyingi ambazo zimejengwa katika kata ile ikiwemo barabara ya Best Bite ambayo kwa miaka nenda miaka rudi ilikuwa ni kero sana. Pia nishukuru Serikali kwenye zile Bilioni moja ambazo Mheshimiwa Rais alizitoa kwa kila Mbunge kwa minajili ya kujenga barabara katika majimbo yetu mimi nimeipeleka kwenye kata moja ambayo ilikuwa haina barabara za lami hasa kata ya Ndugundi tumepata barabara mbili, Mkalamo moja na Mkalamo mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti,vile vile nishukuru Serikali kwa kuangalia suala la mafuriko katika Jimbo la Kinondoni. Mto Ng’ombe umekamilika, na hata mvua za juzi tulikuwa salama sana. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye tulikuwa naye kule kwenda kuangalia, na maelekezo aliyoyatoa yametekelezwa, hivyo hongera sana kwa Serikali kwa kutufanyia jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna suala la Mto Msimbazi, tumelizungumza sana. Napenda nitoe pongezi nyingine kwa Serikali kwamba sasa mradi ule wa kuboresha eneo lile la Bonde la Mto Msimbazi unakwenda kufanya kazi; na tayari tathmini zimefanyika na hivi ninavyozungumza jumla ya nyumba 2,592 zilifanyiwa tathimi na katika nyumba hizo 2,217 wamekubaliana tathmini zile. Isipokuwa nyumba 163 wenye hizo hawajakubaliana na tathmini.

Nilikuwa naiomba Serikali kwa utaratibu uliopo wa Kiserikali uendelee kufanya mazungumzo na wananchi hawa ili nyumba zao ziweze kufanyiwa upya marejeo ya tathmini ili waweze kupata tathmini ambayo inakubaliana na thamani ya nyumba zao ili mradi ule uweze ukaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio yote haya kuna matatizo kidogo ambayo ningependa niyaseme. Kwa mfano kwenye Kata ya Kigogo tuna kituo cha afya kikubwa sana ambacho kina hudumia wananchi wa Ubungo na wananchi wa Ilala. Kituo kile kilipelekewa jokofu la kutunza maiti mwaka 2020; na jana wakati nazungumza kuuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya TAMISEMI nilikuwa naiomba Serikali iweze kufanya haraka kulipa fidia ili jingo la kuhifadhi mashine ile ya jokofu la maiti iweze kujengwa na Serikali ikasema na ikaagiza halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni waweze kutenga fedha za kujenga jengo la kuhifadhi jokofu la kutunzia maiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajabu ni kwamba kumbe wakati mimi namaliza kuzungumza lile jokofu limekwenda kuondolewa limepelekwa kwenye Hospitali ya Wilaya Mabwepande. Hiyo hali sikuipenda sana kwa sababu kumbe Waziri ana taarifa nyingine, TAMISEMI kwa maana ya watendaji wana taarifa nyingine, hili jambo si zuri na halioneshi kwamba Serikali ni moja na inafanya kazi kwa pamoja. Huyu anafanya maamuzi yake na huyu mwingine anafanya maamuzi yake, hawaambizani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili si jambo jema kwa utendaji wa Serikali ambayo ina sifa nzuri ya kuweza kuwatumikia wananchi wake. Nitaomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI au Naibu wake niende naye kwenye Kata ya Kigogo ili aweze kuona jinsi gani hali ile ambayo imefanyika sasa hivi inakwenda kuathiri wananchi. Hii ni hatari kwa sababu maelekezo mengi ambayo yanatolewa hapa Bungeni wananchi wanayachukulia kwa ukubwa wake lakini sasa kama Waziri anasema fedha zitengwe na wakati huo huo mamlaka nyingine zinakwenda kuondoa jokofu maana yake kama vile kuna crush kati ya Serikali kuu na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba na mimi nigusie suala hili ambalo linatula vichwa vyetu. Sisi Wabunge ili uwe Mbunge lazima ule kiapo; na katika kula kiapo lazima utashika ima Biblia takatifu ama Quran takatifu. Asubuhi kila tunapoanza shughuli za Bunge tunaomba dua na tunamtaja Mwenyezi Mungu hapa na tunamwomba atupe hekima kufanya maamuzi na kufanya mambo mengine. Lakini Mungu huyu tunamchukiza. Mungu huyo huyo ambaye tunamsema kwamba ndiye kiongozi ambaye anatuongoza sisi katika maisha yetu tunamchukiza. Tunamchukiza kivipi? Matendo tunayoyazungumza ya kiushoga ni matendo yanayo mchukuza Mungu. Tumesema kama Bunge; na wananchi huko nje na viongozi wa kidini wanalalamika. Leo asubuhi kwa Waziri wa Elimu kulikuwa na swali ambalo lilikuwa linahusiana na masuala haya ya watoto kuharibika wakiwa boarding school, na Mheshimiwa mbunge mmoja alisimama akaomba kwamba je, Serikali haioni uharaka na umuhimu wa kuleta sheria mahsusi? Waziri anajiuma uma anasema watalichukua hilo wazo watakwenda kulifanyia kazi, alah! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unachukua wazo ambalo vitu vinaumiza vichwa vya watu. Jambo hili si la leo, mwaka 1998 kulikuwepo na sheria ambayo ilitungwa inasema Sexual Offenses (Special Provisions) Act, 1998 maana yake mambo haya yalikuwepo miaka mingi yanasumbua, yalikuwa ni madogo madogo. Hata hivyo Sheria ile haikuja explicitly, haiko kwa uwazi kabisa jinsi gani ya kuweza kupiga vita vitendo hivi, ingawa muda…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE.TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie maana yake hoja itakuwa ina-hang. Naomba kama haiwezekani kuleta sheria mpya hapa basi ifumuliwe Sheria ya SOSPA ya 1998 ili iweze ikakidhi mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.