Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kujadili bajeti na hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inaakisi sawasawa hali halisi ilivyo nchini au tulikotoka. Mahususi kwangu, aya ya 62, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametamka kazi nzuri ya mpango wa Serikali kujenga Soko la Kimataifa la samaki katika bandari ndogo ya Kyamkwikwi. Napenda nichukue fursa hii kushukuru. Namwomba Waziri wa Mifugo asimamie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo suala lingine dogo la kitaifa linalohusu pension za watu waliowahi kuitumikia Serikali. Wako watu walitumikia Serikali, leo wana miaka 70, 90 na wengine 100, lakini ukiangalia pension wanayopewa na ukatumia ile time value of money, naishauri Serikali tuwaangalie watu hawa. Hawa watu kwa sababu ya umri, wana magonjwa yanayoendana na umri, lakini mfumo wetu wa Bima ya Afya kama NHIF, hawa watu wakienda hospitali bima za afya haziwasaidii. Serikali tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msiwe na wasiwasi, hesabu za haraka, hawa watu ni wachache. Mnaweza kuwaongezea. Msiwe na wasiwasi, kwa idadi hawa watu ni wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia uchumi wa dunia na uchumi wa Taifa. Nina hofu muda hautatosha, lakini naipongeza Serikali namna inavyodhibiti uchumi wa Taifa letu. Ukiangalia kwa jirani kunavyofukuta, ukaona nyumbani mmetulia, unaweza kujua kwamba aliyeko jikoni anahangaika kusudi mle. Nitarudi hapo muda ukiniruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze mambo matatu. Mkoa wa Kagera tumepata mapigo matatu. Nasimama hapa kuwaeleza mila za kiafrika. Unapopatwa na shida au kama una shughuli, watu wakija kwako kukuona, inakupa faraja. Ilipoanguka ndege ya Precision Serikali kwa nguvu zote ilifika Kagera, Mheshimiwa Waziri Mkuu ulikuja Kagera; hilo jambo liliwafurahisha watu wa Kagera na Watanzania wote. Tunachoomba, Waziri wa Uchukuzi, imeanguka ndege ni historia, lakini lazima tujenge uwanja wa ndege Kagera, Bukoba, utakaoweza kusaidia Soko la Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kagera tuna soko la ndege, economically ni viable, lakini uwanja wa ndege Kagera ni suala la kiusalama. Kwa hiyo, mnaweza mkaangalia Omukajunguti, na Kashaba. Naomba pamoja na pole mliyotupa, tuliangalie na hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni ugonjwa uliotukumba juzi, Marburg. Napenda niwahakikishie, mimi nimezungumza na wahusika, nimezungumza na Mbunge mwenye Jimbo, Mheshimiwa Advocate Captain Pilot Rweikiza, Marukuni shwari, Kanyangereko ni shwari. Eneo lote liko shwari, lakini jambo la muhimu kwa wananchi wa Kagera, response ya Wizara ndiyo iliwafurahisha. Ujio wa Naibu Waziri na kufuatiwa na Mheshimiwa Ummy, ndiyo jambo liliwafurahisha, lakini zaidi namna Serikali ilivyoweza kudhibiti ugonjwa ule. Nchi nyingine bado ugonjwa unaendelea na limekuwa dondandugu. Katika mambo ya kujivunia tujivunie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zaidi ya hayo, tunaiomba Wizara: Moja, mjenge hospitali kubwa ya rufaa Kagera ya kudhibiti milipuko. Hii milipuko nimemwambia Waziri, ilikuja Juliana ikaua watu, ni mlipuko; ukaja ugonjwa wa Covid, ukaua watu, kwa hiyo, umekuja na huu Marburg umeua watu, ijengwe hospitali ya kimkakati, special yenye eneo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza na Waziri, sisi tunapakana na ziwa. Karibu 1/3 ya Ziwa Viktoria liko kwetu na tunapakana na nchi nyingi, kuna mwingiliano. Kuna namna ya kutuangalia kipekee. Katika kata tano za Wilaya ya Muleba kututengenezea vituo vya afya vya kuweza kukabili mapigo haya. Nimeomba na ninadhani Serikali mmenielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende suala la tatu. Desemba tarehe 17, timu ya Mawaziri ilifika Wilaya ya Muleba. Katika timu hiyo Waziri mwenye dhamana ya mifugo wakati ule na wenzake alioambatananao, namwona Mheshimiwa Silinde, Mheshimiwa Mavunde, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, walikuwepo; wakatamka kwamba, uliokuwa mgogoro wa Rutoro umekwisha kwa sababu, mgogoro ulikuwa kati ya NARCO na wananchi, umekwisha. Serikali itakuja kupima, lakini wakaenda mbele wakasema watu wakae bila kuhasimiana, tukamaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali yangu, msisubiri kuja kunipimia, mtupimie leo ikiwezekana kesho. Iddi yangu ninayoweza kuipokea, futari yangu inayoweza kunishibisha ni kwenda kuwapimia watu wangu leo. Watu wangu wanateseka, wana-Kagera wanateseka. Aliyozungumza Mheshimiwa Ezra pale, amezungumza kidogo; kuitendea haki sekta ya mifugo, sekta ya ardhi, sekta ya uhamiaji Kagera, ni kuunda tume huru iende ikaangalie watu wanapigwa katika nchi yao, watu wanabakwa katika nchi yao, mashamba yao yanaharibiwa. Mimi nitakuwa mgeni wa nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile clip mliyoiona ya kuuaa kwa Aspro, Katibu wa Chama cha Mapinduzi, ilikuwa edited. Ukiuona mkanda mzima unaweza ukakubaliana nami kwamba, Mheshimiwa Mwijage tukapime Rutoro kesho, tukamalize mgogoro wa Rotoro keshokutwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema Mwijage mimi vile ni vijiji na hati za Serikali ninazo hizi. Anatoka mtu, eti ni mteule, anasema pale sehemu ya kuchunga ng’ombe, ndipo hapo tunapoachana. Na kwa umri huu siwezi kuogopa kutofautiana na mtu mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema ile ni sehemu ya Serikali na Waziri anasema kwamba pale watu wakae, anatoka mtu anasema mimi sijapewa barua; upewe barua zaidi ya hii? Serikali imeandika yenyewe kwamba hapa watu wanapaswa kukaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba – hayo Mungu atatulipia mbinguni – ninachomba, wale watu ni maskini, nendeni muwapimie ardhi yao. Mtu aende aseme communal land. What does communal land mean? Wale ndiyo nchi yao, hawana kwao kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inauma, mtu yuko kwao anapigwa na mtoto wa jirani, unasikia mtoto wa jirani anampia mtoto wako kweli utalala? Watu wanasema Mwijage ni kichaa. Itakuaje wewe umelala na mkeo, mtoto anapigwa na anayempiga anazungumza lugha ya mwezini; unalala baba usingizi unakuja? Na mnaamshana na mkeo wakati watoto wanaumia, haiwezekani. Mtoto wa mjomba nenda kalelewe ujombani, lakini ukifanya shari ujombani watakwambia wewe siyo mtoto wa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtusaidie. Na zaidi katika hayo, nimesikia watu wanazungumzia kufuga, kufuga kuna tija. Ninaomba muitumie Kagera kama model ya kufuga, siyo kuchunga. Mwenyekiti ni dhamana yako, uje unite nikueleze. Tuanzie Kagera, hii biashara tunayofanya tunapoteza muda. Anza kufuga kuanzia Kagera mkiiga mfano wa Mbarara. Hatuwezi kuchunga tukaweza kuingia kwenye soko la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo futari yangu na Eid al-Fitr naomba tuandamane twende kwenye vijiji vyangu vinne mkavipime, wananchi watajijua. Nilikuwa nimewaombea chakula, sasa naomba muwapimie wakajilimie wenyewe watavuna wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)