Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kufunga dimba la uchangiaji jioni hii. Awali ya yote kama ambavyo wachangiaji wenzangu waliotangulia walivyosema mimi kwa kweli naishukuru sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika utekelezaji wa majukumu haya ambayo tumemtwisha ya kuiongoza nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote hii inayotekelezwa pamoja na kazi nyingine ambazo Mheshimiwa Rais anatuongoza vizuri, uratibu wake unafanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa hiyo tuna kila sababu ya kumpongeza na hata kwenye taarifa yake tumeona jinsi ambavyo miradi hii ya SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere, ATCL, Bomba la Mafuta, madaraja makubwa na kadhalika yanavyokwenda ni chini ya uratibu wake, anaziratibu hizi Wizara anazosimamia, kwa hiyo lazima tumpongeze kwa kazi nzuri na pia tumemuona akitembea huko na huko akikerwa na kutoa maelekezo mbalimbali juu ya miradi inayosinziasinzia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa miradi hii unachangia pia katika kuongeza mzunguko wa fedha katika nchi yetu, ndiyo maana kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba miradi hii inatekelezwa mpaka ifikie mwisho ndiyo kazi kubwa iliyoko mbele sasa hivi ya kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilishwa. Pamoja na kukamilishwa vilevile tuwe mstari wa mbele katika kusimamia haya makandokando yanayojitokeza kama haya yanayotokea kwenye ripoti ya CAG yanayotusumbua sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kama basi kweli muda wa kikanuni haujafika wa kujadili lakini nadhani wakati mwingine tunaiogopa hii taarifa kwa kudhani kwamba labda taarifa ya CAG ni kitu hasi, tuichukulie positively, ni kitu chanya kwamba angalau sasa tuna mifumo ambayo inaweza ikatuambia nini kimetokea, sasa unapotuambia nini kimetokea na kinajadiliwa mitaani hatuwezi kufumba midomo kabisa. Lazima tufike mahali tutaje na zipo namna nyingi za ku-justify mjadala huu katika kipindi hiki hatuwezi kukaa jambo linajadiliwa na wananchi huko sisi tukakaa hapo kimya kana kwamba siyo sehemu ya nchi hii, hilo nadhani tuwekane huru kuligusia wakati tunachangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu Jimbo langu la Mwanga. Wananchi wa Mwanga wanaishukuru sana Serikali ya CCM chini ya Mama Samia Suluhu Hassan, miradi mingi sana imetekelezwa kuanzia miradi ile ambayo tulikubaliana kama Mwanga kwamba ni miradi ya kimkakati, kama ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambao unakwenda vizuri kabisa kwa kasi, ujenzi wa barabara bypass kilometa 13.9 tutakayoita Msuya, ujenzii wa chuo cha VETA, ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri, pamoja na ahadi ya Mheshimiwa Rais ya stendi ya kisasa ambayo hii kwa kweli haijafikia mahali pa kuridhisha na ndiyo maana nahitaji hapa kuwakumbusha wanaohusika kwamba Mheshimiwa Rais aliwaahidi wananchi wa Mwanga kwamba watapata stendi ya kisasa na utekelezaji ulianza katika maana ya kutakiwa kupeleka andiko na michoro, yote haya yalifanyika lakini kuna mahali pamekwama ambapo ningeomba sana kwamba pakwamuliwe ili mradi ule utekelezwe.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, specifically kwa mradi unaowagusa wananchi kama mradi wa hospitali ya Wilaya tunaomba sasa tupatiwe zile fedha zilizobakia Shilingi Bilioni 1.3 na Watendaji wangu, Wataalam wangu wa Halmashauri na Baraza langu la Madiwani ambao kila siku namuombea Mungu awabariki na kuwalinda, wameniahidi kabisa kwamba wakipata fedha hizo za mwisho bilioni 1.3 ukifika mwisho wa mwaka huu tutaanza kuomba vifaa ili tuweze kutoa huduma zile za msingi pale za OPD na baadhi ya huduma za kulaza. Tuko kwenye jengo la mionzi sasa hivi tunaomba Wizara husika isituangushe kwa fedha zilizobakia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vituo vya afya tumeendelea vizuri. Tuna vituo vya afya vya kimkakati vipya vitatu na vile vya zamani ni vitatu jumla vituo vya afya Sita. Vituo vyote vinakabiliwa na changamoto inayofanana ya watumishi wa afya pamoja na vifaatiba. Nilipochangia mara ya mwisho kwenye ripoti ya LAAC nilitoa takwimu ya mapungufu tuliyonayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie Kituo cha Afya cha Kata ya Lang’ata ambacho kwa kweli kimechakaa sana, tunaomba kituo hiki kikarabatiwe ili kiweze kutoa huduma katika viwango vya vituo vya afya vilivyokusudiwa kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii tulipaswa kupata vituo viwili vya afya vya kisasa, kimoja tumepata kwenye Kata ya Kirya ambacho ni Kituo cha Afya cha kisasa kabisa, kinahudumia mpaka watu wa kutoka kwa rafiki yangu Senior Brother hapa Mheshimiwa Ole-Sendeka kule Simanjiro pia kutoka Same wanapata huduma pale. Pia kile kituo kingine ambacho kilipaswa kujengwa bado hakijapata fedha tunaomba tupate fedha kwa ajili ya kituo hiki cha afya cha pili ili mpango ule na ahadi ile iweze kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi ya elimu, tuliahidiwa kupata shule mbili kwenye Kata zile mbili ambazo zilikuwa hazina shule. Bado Kata moja ya Toroha haijapata shule yake pamoja na kwamba tulifikia mahali kabisa mpaka pa kuwa requested bank account ili fedha ziingie lakini hapo palipokwama sasa tunaomba pakwamuke ili fedha ziweze kupelekwa wale wananchi wangu ambao wengi wao ni jamii ya wafugaji waweze kupata shule. Shule ambayo tumeipata moja ya Kivisini imekamilika vizuri na tumekusudia kuifanya moja kati ya shule zetu bora kama ilivyo shule ya Dkt. Asha Rose Migiro, Shule ya Kamwala na Shule ya Usangi ‘A’ ambazo ni moja ya shule bora Kimkoa na Kitaifa zinazotokea pale Wilayani kwetu Mwanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna tatizo kubwa la Walimu. Suala la ajira ya Walimu ni tatizo kubwa sana. Juma lililopita tulikuwa tunafanya tathmini ya kila Mwalimu jinsi ambavyo ame-perform na alivyofaulisha kwenye somo lake, wako Walimu wa kujitolea ambao hawalipwi chochote lakini wameongoza katika kufaulisha masomo yao. Walimu kama hawa zawadi pekee ya kuwapa ni kuwajiri kwa kweli katika shule hizi. Vinginevyo wapo ambao wamejitolea muda mrefu ninaogopa wanaweza wakafikia umri wa kustaafu kabla hawajaajiriwa halafu wakapoteza kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la maji. Ipo miradi mingi lakini kwa kweli kasi ya miradi ya maji haijaridhisha bado. Mheshimiwa Waziri wa Maji juzi alikuja nilimweleza hili jambo, kubwa kuliko yote ni shukrani kubwa sana kwa Serikali kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe ambao utalisha maji katika Wilaya ya Mwanga eneo lote la tambarare Same mpaka Korogwe, huu ni mradi mkubwa sana wa Shilingi Bilioni 262. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais mradi huu ulikwama kwa muda mrefu lakini mwezi uliopita alikuja Mheshimiwa Waziri wa Maji akakwamua mradi ule tukasaini restatement agreement na kuahidiwa kwamba ndani ya miezi 14 maji yatatoka, tunaomba ahadi hii ambayo watu wameichukua kwa thamani sana kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ikamilike kama ambavyo imeelezwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la barabara linaendelea vizuri lakini kipekee niishukuru Serikali kwa ajili ya usanifu unaoendelea wa barabara inayotoka Kisangara kwenda Nyumba ya Mungu kilometa 17 kwa kiwango cha lami. Barabara hii ni muhimu kwa sababu eneo lile lina miradi mikubwa ya Kitaifa, huku mradi wa umeme ambapo tunachangia kwenye Grid ya Taifa na miradi mingine mingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kengele imegonga niseme moja la mwisho iko barabara nyingine ya kutoka Kifaru kutokea kituo cha Ng’ombe kilometa 75, hiyo ni barabara ya mpakani. Kwa hiyo kwa ajili ya umuhimu wake, kwa ajili ya mambo ya usalama na miradi mikubwa ambayo inaendelea katika eneo hili, hii ni barabara inayounganisha Tarafa Tano tunaomba iwe upgraded kufikia kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna tatizo kubwa sana la vyanzo vya mapato, vyanzo vyetu viwili vimetelekezwa. Kimoja ni Bwawa letu la Lang’ata ambalo lilikuwa likitoa Samaki na mapato makubwa sana, tunaomba kauli ya Serikali tatizo ni Samaki wamedumaa au tatizo ni mbegu isiyofaa? Mpaka sasa hivi hakuna kauli ya Serikali juu ya bwawa lile tunaomba lifanyiwe kazi pamoja na suala la magugu maji katika Ziwa. Naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)