Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mwanakhamis Kassim Said

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Magomeni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Naibu Spika,ahsante na mimi kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia kwa jioni hii ya leo. Kama hukumshukuru binadamu mwenzio kwa analolifanya basi hata Mwenyezi Mungu huwezi kumshukuru. Katika vitabu vya Quran mwanamke ametajwa mara tatu. Nichukue nafasi hii kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya mambo makubwa sana. miaka miwili tu lakini ameitumikia nchi hii kwa nguvu zake zote kwa sababu anahofu ya Mungu, Mama Samia ni mcha Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia amefanya miradi mingi katika nchi hii kama vile barabara, skuli na miundombinu mbalimbali. Sisi hapa Wabunge tumetoka kwenye majimbo ambayo haya hatukuyaanza sisi, wapo wenzetu walipita. Sasa, kuna miradi walitengeneza Wabunge wenzetu waliopita lakini sisi hatukuiendeleza miradi ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia mtangulizi mwenziwe aliyepita amefanya miradi mingi sana na miradi ile yote haikukamilika, lakini Mama huyu alivyokuwa ni mcha Mungu na ana hofu ya Mungu miradi hii ameisimamia kikamilifu na bado anapambana nayo, na Mungu ndiye atamlipa. Kwa nini akasimamia miradi hii, ni kwa sababu ni kodi za wananchi, ni pesa za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Samia anafanya mambo makubwa sana, hata mazungumzo yake anapoyazungumza ni maneno laini yanamtoka ndani ya mdomo wake. Ni mama mmoja mwenye sura ya tabasamu muda wote, hata akikasirishwa basi yeye bado ametabasamu, huyu ni mcha Mungu wa kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge hususani wanawake Rais wetu ni mwanamke. Tulikuwa tuna nyimbo tunaimba mwanamke kuwezeshwa, lakini sasa mwanamke hawezeshwi mwanamke anafanya mwenyewe. Mama Samia anakwenda kila pembe kila na kwenye kila kichochoro. Mama huyu ni mcha Mungu, hata ukimtazama kwenye kipaji chake cha uso, ni mcha Mungu. Anapokwenda popote hatoki mtupu lazima atakuja na kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia Miradi aliyoiacha Mheshimiwa Magufuli ameiendeleza. Sisi Wabunge humu tuseme Wabunge wangapi miradi tuliyoikuta ya wale Wabunge wetu watangulizi waliopita tumeiendeleza? Tukifika tunaanza miradi mingine mipya lakini ile tumeiacha. Mcha Mungu huyu ameendelea kufanya kazi, kuwatumikia Watanzania. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wanawake tusimame na Mama Samia Suluhu Hassan, tumuimbe Mama Samia Suluhu Hassan, tumpigie makofi Mama Samia Suluhu Hassan, tumwombee dua Mama Samia Suluhu Hassan. Vile vijineno vijineno tuachane navyo, tuvipuuze, hususani wanawake Mama Samia ametubeba, ametupa uhuru, muda huu mwanamke tulikuwa tunaidai asilimia 50 sasa imetimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba wanawake tumsafishie njia Mama Samia Miaka mitano, miaka miwili amefanya mambo haya miaka mitano ijayo atafanyaje? Nakuombeni Watanzania maneno yanayozungumzwa mengine yapuuzeni, Mama anapambana, ni mwanamke, amezaliwa na mwanamke, lazima tumuunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia anapokwenda kuzunguka anachokileta anakileta kwa maendeleo ya Watanzania sote. Hawaletei watu wachache kama wakitumie wao peke yao, ni cha kwetu sote, lazima tumuunge mkono, tumpe nguvu Mama yetu, tumpe nguvu Rais wetu, tumpe nguvu Shujaa wetu hususan wanawake. Wanawake huu ni muda wetu, huu ni wakati wetu, wanawake lazima twende kifua mbele. Mama ni shujaa, Mama ametuwezesha, anaposafiri kwenda nje haendi kuzungumza na makapuku, anazungumza na wanaume, walioshiba, anazungumza nao na wanamwelewa akirudi anarudi na chochote. Nawaomba Watanzania Mama Samia amefanya mambo makubwa, ni mwanamke lakini anapambana, anaitetea nchi na kumtetea mwanamke. Mama Samia anamtetea mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze suala lingine kuhusu mwanamke. Mwanamke ni nguvu kazi ya Taifa letu, leo mwanamke huyu tunayesema ni nguvu kazi ananyanyasika, anadhalilika, wanawake wamekuwa wanauliwa kiholela, Ofisi ya Waziri Mkuu walisimamie suala hili. Wanawake wanauliwa sana. Hivi karibuni tuliona mwanamke, mumewe ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, baba ametoka nyumbani, anarudi mke wake ameuliwa. Juzi mwanamke ni Mhasibu amepigwa mpaka amechomwa moto. Kwa kweli inasikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke ni Taifa kubwa, mwanamke ni kila kitu, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu ilisimamie suala la haki za mwanamke. Mama yetu anatutetea sana wanawake, lakini bado mwanamke hatujamsimamia. Waheshimiwa asilimia kubwa Wabunge humu waliopita walikuwa ndugu zetu albino wanateseka, wananyanyasika, lakini Serikali hii ilisimama na kuwatetea ndugu zetu wale albino na liliisha. Kwa nini lisiishe suala hili la mwanamke kunyanyaswa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini lisiishe mwanamke kuuliwa? Kwani sasa hivi wanawake wengi tunasoma kwenye mitandao wanawake wanapata matatizo, wanauliwa wengi sana. Je, wale waliokuwa hawatangazwi kwenye mitandao, ni wangapi? Naomba sana Serikali, chonde chonde tusimame na mwanamke, Rais wetu ni mwanamke na sisi wanawake ni jeshi kubwa, tumpambanie Mama Samia miaka mitano tena ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)