Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, uongozi mpya siku zote ni fursa na sisi tuna fursa hapa ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na fursa imejitokeza. Nakumbuka maono yake yameshatolewa katika maeneo makubwa mawili, kwanza katika hotuba ambayo ilitolewa hapa Bungeni mwaka 2021, ya pili ni kwenye Makala ambayo aliiandika tarehe 01, Julai, 2022. Makala ambayo alikuwa anaakisi miaka 30 ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini ambapo aliibuka, nataka kunukuu hapa, alieleza kuwa: - "Ndiyo sababu kwenye uongozi wangu ninaamini katika kile kinachojulikana kama 4R – ikiwa ni ufupisho wa maneno manne ya Lugha ya Kiingereza; Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahamilivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujenga Upya)" mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu kwamba wenzetu Serikalini, Mawaziri, watakapoleta bajeti zao hapa tutaona jinsi ambavyo wametafsiri ndoto hii ya Mheshimiwa Rais kupitia mipango na bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa leo nataka nizungumzie eneo moja katika hizo 4R, R ya tatu ambayo ni reforms (mabadiliko). Na Mheshimiwa Rais alisema kuwa nimedhamiria kwamba kwenye kuenzi miaka yetu ya demokrasia ya vyama vingi, Serikali yangu itajitahidi kufanya mabadiliko katika mifumo ya kisiasa, kiuchumi na katika sheria. Lengo ni kwamba Tanzania yetu iende na wakati” mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba yetu Ibara ya 6 inatambua Serikali tatu, aina tatu za Serikali katika nchi hii; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali za Mitaa. Hizi ndizo aina tatu za Serikali. Na zote zina Rais wake; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo, Rais wa SMZ yupo na Rais wa Serikali za Mitaa bahati nzuri ni huyohuyo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumeweka sheria mbalimbali kwenye kutafsiri maono haya ya Katiba; Sheria ya Serikali za Mitaa tunafahamu Sura Na. 287 na 288 kwa maana ya wilaya na miji. Tumeweka sera ya ugatuaji, na sera hii tumekuwa tukiitekeleza tangu mwaka 1998. Ililenga kuhamisha na kupeleka madaraka katika maeneo makubwa mawili, kutoka Serikali kuu kwenda ngazi ya halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji. Pili, kutoka ngazi ya halmashauri kwenda kwenye ngazi za msingi za kata, mitaa, vijiji na vitongoji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hii inazungumzia vertical decentralization, haizungumzii horizontal decentralization. Lakini sisi kwenye tafsiri yetu, tulichofanya tuka-decentralize kutoka Wizara ya Maji, kutoka Wizara ya Elimu kwenda Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambayo bado ni central. Kwa kutumia falsafa ya Mheshimiwa Rais ya reform lazima tuliangalie upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, decentralization ilikwamia sehemu haijafika mwisho, na ndiyo maana wakurugenzi kila kukicha safari zao kutoka Ubungo, kutoka Songea kuja Dodoma. Wako wapi; kwenye kikao Dodoma, kwa sababu Mamlaka za Serikali za Mitaa hazifanyi kazi yake sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sheria tumeweka vyombo vitatu vya kutekeleza hili. Cha kwanza tumesema Baraza la Madiwani ndicho chombo cha juu cha maamuzi katika halmashaui. Sasa Waheshimiwa Madiwani wenzangu mliopo hapa niwaulize; hivi kweli Baraza la Madiwani katika halmashauri zetu ndicho chombo cha juu cha maamuzi? Ndivyo ilivyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema ya pili Kamati ya Maendeleo ya Kata (Ward Development Committee) ndicho chombo cha maamuzi katika ngazi ya kata ambapo Mwenyekiti wake ni Diwani. Na mwisho tumesema Mwenyekiti wa Kijiji/Mtaa ndiye kiongozi na Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, sheria na sera zipo vizuri sana, tunahitaji reform kuhakikisha kwamba sera hizi zinafanya kazi sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nipendekeze maeneo matatu ya reform; kwanza tuna changamoto ya kwanza kati ya viongozi wachaguliwa, wateule na waajiriwa. Tukienda kwenye uchaguzi tunachagua viongozi watatu; tunamchagua Rais, Mbunge na Diwani. Inapokuja kwenye utekelezaji wa majukumu, Rais ni msimamizi wa shughuli za Serikali katika Serikali Kuu na kwa vitendo anaonekana hivyo, lakini Diwani ambaye ni msimamizi katika kata yuko wapi? Hili ni eneo la reform ambalo lazima tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili; Madiwani kisheria tumewapa jukumu la usimamizi wa programu za maendeleo katika ngazi ya kata. Kisheria ndio wakuu katika shughuli zetu za maendeleo. Tukawaongezea pia jukumu la kusimamia ukusanyaji wa mapato katika kata zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Madiwani ni part time workers. Umewahi kuona wapi duniani mtu umekabidhi jukumu la usimamizi halafu ni part time? Hili ni eneo ambalo lazima tuliangalie, linahitaji reform. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyekiti wa Kijiji ambaye ndio kiongozi na mkuu wa Serikali, huyu naye ni parttime, lakini kwenye kata tukaenda tukarundika. Nilikuwa naangalia muundo wa kata moja pale Dar es Salaam, ofisi ya kata moja ina watumishi 16, watawala saba, afya wawili, elimu wawili, maendeleo ya jamii mmoja, afisa ustawi wa jamii mmoja, kilimo mmoja, mifugo mmoja, uvuvi mmoja. Dar es Salaam afisa uvuvi kwenye kata anafanya nini? Dar es Salaam afisa mifugo kwenye kata anafanya nini? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji reform, hawa watu wapunguzwe ili mshahara unaotokana na hawa tumpe Diwani awe fulltime worker. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama tupo serious na local government authority, Madiwani ni muhimu wawe wafanyakazi wa kudumu wawe salary, wapewe mishahara, kwa sababu hawa, sisi angalau kwenye Bunge ni wakutoa ushauri. Diwani sio wa kutoa ushauri ni msimamizi inakuaje msimamizi asiwe mfanyakazi wa kudumu? Tunahitaji eneo hili lifanyiwe reform...

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimwia Naibu Spika Taarifa.

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Vivyo hivyo mkuu wa Serikali ya Kijiji na mtaa. Mkuu wa Serikali ya Mtaa unamfanyaje kuwa part-time?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Huyu naye lazima tufanye rationalization ili kwamba huyu naye awe ni sehemu ya utumishi katika eneo lake.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kitila kuna taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika,naomba nimpe taarifa mazungumzaji Profesa Mkumbo; najua ni mwanafunzi mzuri sana wa decentralization na nimewahi ku-share naye kwamba decentralization…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye taarifa.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa nimpe taarifa tu kwamba kwa mfumo wa ugatuaji wa Serikali za mitaa nchini hauiondoi Serikali za mitaa kwenye unitary government. Pamoja na kuwa kuna hayo mamlaka ambayo tumewapa hawa madiwani lakini mfumo hautoi madiwani kuwa na workforce ya kumwezesha kutekeleza majukumu ambayo anajaribu kuyazungumza. Ndiyo maana kwenye ngazi hiyo wameweka wataalam wa kada mbalimbali kama ilivyo kwenye Wizara, Waziri ni mmoja, Naibu ni mmoja lakini kuna katibu mkuu na watendaji tofauti wa kumsaidia ku discharge majukumu ya Serikali kwenye ngazi ile hautegemei majukumu yale afanye mwanasiasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

NAIBU SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Mkumbo.

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, Siipokei hiyo taarifa kwa sababu inakinzana na hoja yangu, kwa hiyo sipokei hata kidogo. Lakini hoja ya msingi ameipata, mimi ni mwanafunzi wake mzuri wa local government, sasa amenifundisha mwenyewe halafu ananipinga, haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya msingi ni kwamba wale watu ambao wanafanya kazi za kila siku za kusimamia maendeleo yetu ili tuone impact kwenye government reform ni muhimu sana wakapewa majukumu yao na yaendane na hadhi yao, wapewe wafanye kazi zao za msingi ikiwemo utumishi wa kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho na mimi nichukue nafasi hii kumpongeza sana kwa mkitadha huu Mheshimiwa Rais kwa kuja na haya mambo manne (4R) na kwakweli Waheshimiwa Wabunge sisi tunajukumu la kutafsiri hizi 4R za Mheshimiwa Rais hapa ndani na katika utendaji wa Serikali. Mwisho nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi anavyomsaidia Mheshimiwa Rais kwenye kusimamia shughuli za maendeleo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili.

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naunga mkono hoja.