Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. Sisi katika Jimbo letu la Manyoni Mashariki kuna kazi nyingi sana zimeshafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki tumepata fedha nyingi sana. Tumepata shilingi bilioni nne kwa ajili ya ujenzi wa shule ya wasichana ya Mkoa; tumepata shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA; tumepata shilingi bilioni 12 kwa ajili ya mradi wa maji wa Kintinku Msilile; na pia tulipata shilingi bilioni 1.7 tukajenga shule tano mpya za sekondari. Haya ni mafanikio makubwa sana. Nasi watu wa Manyoni kwa kweli hatujawahi kupata fedha nyingi hizi huko nyuma, kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais na tunamtia moyo aendelee kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Waziri Mkuu na timu yake; Mheshimiwa Prof. Ndalichako na mama yangu pale, wanafanya kazi kubwa sana. Wanaitendea haki sana Wizara ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo nachangia upande wa ajira, lakini nataka nioneshe uhusiano uliopo kati ya ajira na ile taasisi yetu ya TAESA (Tanzania Employment Service Agency). Mheshimiwa Hasunga ameeleza hapa kwamba, tatizo la ajira Tanzania bado linaendelea kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikwambie, it is a time bomb. Ni bomu! Kwa sababu gani? Kwa mwaka, takwimu zinatuonesha, tunatoa vijana takribani 800,000 hadi 1,000,000 wanaingia kwenye soko la ajira, lakini ni chini ya asilimia 20 ya vijana wanapata ajira. Hili ni tatizo kubwa sana. Mimi nimefundisha katika taasisi za elimu ya juu, nina vijana ambao wamekaa zaidi ya miaka 10 tangu wamalize hawajapata ajira, wapo mtaani. Hili ni tatizo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulianzisha TAESA 2002. Lengo la TAESA lilikuwa kuratibu ajira, lakini tujiulize, wangapi wanaijua TAESA? Je, TAESA ina capacity ya kuratibu tatizo la ajira? Vile vile tulianzisha TAESA ili iweze kuwa-connect wanaotafuta kazi na waajiri kwenye sekta binafsi na sekta ya umma. Je, haya yanafanyika?

Mheshimiwa Naibu Spika, TAESA iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mwaka 2016 walianzisha program ya mafunzo ya kazi kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu, inaitwa internship program; lakini mwaka 2017 Ofisi ya Waziri Mkuu ilianzisha Mwongozo wa Mafunzo ya Kazi kwa Vijana Wanaomaliza Vyuo Vikuu (National Internship Guideline).

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Mwongozo, lakini leo hii umewasikia Wabunge wengi wakisema, huko kwenye Halmashauri zetu kuna vijana wanachukuliwa wanajitolea, wanalipwa kiasi ambacho hakipo kwenye mwongozo. Nini maana ya kuanzisha huu Mwongozo ambao uko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo tulitegemea utasaidia kuhakikisha kwamba, unaratibu suala la kutumia hata hawa vijana kwa part time, na vilevile kuhakikisha kwamba taasisi zote za umma na sekta binafsi wanatumia huo Mwongozo kwa ajili ya kuwasaidia vijana wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, program ya kuwapa mafunzo vijana waliohitimu vyuo vikuu hadi sasa takwimu nilizonazo, imefikia vijana zaidi ya 13,000. Hao vijana wanaingia mkataba wa miezi sita hadi 12, wanalipwa 150,000/= kwa mwezi. Maana yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi takribani shilingi bilioni 18 zimetumika kwa ajili ya hii programu. Swali langu linakuja, kuna uhusiano gani kati ya TAESA na Sekretarieti ya Ajira? Kuna uhusiano gani uliopo kati ya TAESA ambayo inawatafutia vijana ajira na Sekretarieti ya Ajira? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekretarieti ya Ajira imejikita kwenye ajira za umma. Sasa swali langu linakuja? Je, wale vijana ambao TAESA imewapa mafunzo, ni jinsi gani inaratibu kuhakikisha kwamba wale vijana wanaotoka TAESA inawapeleka kwenye Sekretarieti ya Ajira ili waweze kupata ile ajira?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo. Hakuna link iliyopo kati ya TAESA na Sekretarieti ya Ajira. Hawa ni watoto wa baba mmoja na mama tofauti. Nilitegemea kwa sababu, TAESA ime-invest hela nyingi sana kuwajengea uwezo hawa vijana, nilitegemea zinapotoka ajira za Sekretarieti ya Ajira, kipaumbele kiwe kwa wale vijana waliotoka TAESA. Leo nikimwuliza Mheshimiwa Waziri aniambie ni vijana wangapi waliopata mafunzo ya TAESA, walipata ajira za Sekretarieti ya Ajira, inawezekana wakawa wachache sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo na kwa kweli, tunahitaji kulifanyia kazi. Tukiangalia katika nchi za wenzetu, kwa mfano Kenya. Kenya wana TAESA kama ya kwetu, lakini wenzetu walichofanya wameanzisha kitu kinaitwa National Employment Authority. Ukiangalia majukumu yake ni tofauti sana na ya kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, TAESA yetu haina meno. Tunategemea TAESA yenye meno ambayo itasaidia vijana wetu kupata ajira. Siyo lazima ajira ya Serikalini, lakini iweze ku-connect vijana wetu na ajira mbalimbali; iwatafutie ajira; iwajengee uwezo; na mambo mengine, lakini bado tuna tatizo kubwa sana kwenye suala la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali, kama nilivyotangulia kusema, tatizo la ajira bado ni kubwa sana. Kweli tunasema vijana wajiajiri, lakini mzazi anapopeleka mtoto shule, chuo, anategemea yule mtoto aje awe afisa; hayo ndiyo mategemeo ya kila mtu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri wangu ni nini? Kwanza, tunahitaji kupitia upya TaESA, tuipe nguvu ya kifedha, tunahitaji tufikie vijana wengi. Tuone uhusiano uliopo kati ya TaESA na Sekretarieti ya Ajira. Wale vijana ambao wamekuwa groomed na TaESA tunategemea wachukuliwe na Sekretarieti ya ajira; hilo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, hizi taarifa za hizi nafasi za internship tunahitaji ziwe za uwazi. Vijana wote wa Kitanzania wapate. Nilitegemea kusikia vijana wangu wanaotoka Manyoni vilevile wamenufaika na huu mradi wa TaESA, lakini nikiuliza inawezekana nisiwapate.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, nilitegemea kuona kuna kanzidata (database) ya kuhakikisha kwamba vijana wote wanaomaliza vyuo vikuu wanajiunga kwenye ile kanzidata ambayo itakuwa chini ya TaESA ili iwe rahisi TaESA wenyewe kuratibu masuala ya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudie kuishukuru sana Serikali, hususan Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa mnayoifanya, sisi Manyoni ametupa miradi mingi sana. baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja; ahsante sana. (Makofi)