Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya katika kuleta maeneleo ya nchi hii. Sote tunashuhudia Rais halali, usiku na mchana anahangaika huku na huko kutafuta rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii na maendeleo ya Watanzania. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Taasisi zake kwa kuja na mipango mizuri ambayo tumeisoma kwenye bajeti hii nzuri kabisa, bajeti ya mwaka 2023/2024, kwa kweli nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali pia kwa kuanza mchakato wa kuja na Dira Mpya ya Maendeleo ya kuanzia mwaka 2025 mpaka mwaka 2050. Dira iliyopo ambayo tulianza kuitekeleza mwaka 2000 mpaka 2025 ilikuwa na vipaumbele vitano ambavyo vilikuwa ni msingi wa kujenga nchi yetu. Kwanza ilikuwa ni kuboresha hali ya maisha ya Watanzania. Sote ni mashahidi miaka 25 sasa bado hali yetu haijawa vizuri sana, maisha ya Watanzania katika maeneo mengi bado hayajaimarika na hiyo inatupa fursa sasa kwamba tuangalie mikakati gani tunaiweka ili tuweze kuboresha maisha haya.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ilikuwa ni kuwepo kwa mazingira ya amani usalama na umoja ndani ya nchi yetu. Katika hili tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana, hii ndiyo kigezo kikubwa cha kuiweka nchi yetu iwe tofauti na nchi zingine. Tatu ni kujenga utawala bora wenye uwajibikaji ufanisi na wenye tija. Nne, ilikuwa ni kujenga jamii iliyoeleimika na inayoendelea kujifunza na mwisho ni kujenga uchumi imara wenye kuweza kushindana na uchumi wa dunia yaani uwezo wa kukabiliana na ushindani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hali hiyo malengo hayo ni mazuri na ninaamini hata katika dira mpya itakayokuja itazingatia haya ambayo tumeyatekeleza yale ambayo tutakuwa hatujafanikiwa basi inaweza ikayapeleka kuyaweka katika dira inayokuja mpya ili tuweze kufikia miaka 50 Tanzania iwe ni nchi tofauti.

Mheshimiwa Spika, yapo mambo kadhaa ambayo ningependa kuchangia, lakini kwa leo nitachangia suala moja nalo ni suala la ajira kwa Watanzania. Tatizo la ajira ni kubwa katika nchi yetu, ajira ni haki ya kila mtu, na tunaposema ajira, iwe ni ajira ya kuajiriwa Serikalini pamoja na Taasisi zake, iwe ni ajira ya kuajiriwa kwenye kampuni binafsi na makampuni yao, iwe ni ajira ya kujiajiri ni haki ya kila Mtanzania kuifanya hiyo, hiyo ndiyo itakayoleta mchango mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 11(1) inasema; Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kufanya kazi, haki ya kujipatia elimu na haki ya kupata msaada kutoka kwa jamii wakati wa uzee, maradhi au hali ya ulemavu na katika hali nyingine za mtu kuwa hajiwezi na bila kuathiri haki hizo Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mtu anaishi kwa jasho lake.

Mhshimiwa Naibu Spika, kumbe hili suala la kufanya kazi ni haki ya Kikatiba, kila Mtanzania lazima afanye kazi. Ukisoma Ibara Ndogo ya Pili inasema kila mtu anayo haki ya kujieleimisha na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na ustahili na uwezo wake. Hii ni haki ya Kikatiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia maisha ya Watanzania sasa hivi wapo vijana wengi wamesoma katika vyuo vikuu, wamesoma katika vyuo vya kati, wana taaluma mbalimbali, wapo ambao hawajasoma lakini wote ni Watanzania. Wote wanatakiwa wapate ajira na ajira maana yake ni kufanyakazi. Sasa hivi ukienda mahali popote, ukienda huku Mijini wapo vijana wengi hawana kazi, hawafanyi kazi. Ukiienda kule vijijini vijana wengi hawafanyi kazi, TAIFA letu haliwezi kujengwa na watu kutokufanya kazi, lazima tuje na mkakati wa kuhakikisha ni wajibu wa Serikali kuratibu kwamba sasa watu wote wanafanya kazi na kila mtu tujue wewe unafanya kazi gani unachangia nini katika nchi, kila mtu lazima tujue na pale ambapo mtu hana kazi ni wajibu wa Serikali kuratibu na kumuonesha kwamba kuna fursa hizi kuna hii kuna hii, wewe unaweza kufanya kipi ili kila Mtanzania afanye kazi, kwa kufanya hivyo ndipo tutajenga uchumi imara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya umaskini wetu uliopo inatokana na Watanzania wengi kutokufanya kazi. Watanznaia wengi kutokuwa na ajira. Kutokuziona fikra, kutokuziona fursa za kufanya kazi, hii inaturudisha nyuma sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi wa Tanzania wanaofanya kazi sekta ya umma bado maslahi yao siyo mazuri sana. Nina imani Serikali itaendelea kuboresha maslahi yao hawa wafanyakazi ili waweze kufanya kazi kwa weledi, kwa tija na kuleta ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wapo wafanyakazi wa sekta binafsi ambao tunawasahau, hawa wanalipwa viwango vidogo sana. Vile viwango wanavyolipwa haviwawezeshi kuishi, haviwawezeshi kujenga uchumi, haviwawezeshi kuwekeza, wala haviwawezeshi kulipa kodi. Kwa mantiki hiyo, hatuwezi kuondokana na umasikini kama hatutaweka nguvu katika hili kundi kubwa linalofanya kwenye sekta binafsi ambao viwango vyao ni vidogo. Huu ni wajibu wa Serikali kuratibu na kuangalia tufanye nini ili wapate maslahi mazuri ili walipwe vizuri waweze kufanikiwa. Hili litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali, ili Watanzania walipe kodi, ili tujenge uchumi, ili tuwekeze; ukilipa vizuri zile hela ndiyo unawekeza na ndiyo unatoa ajira kwa watu mbalimbali. Hawa watu wote wakiwekeza kule, ndiyo ajira zitakuwa zimepatikana. Hatuwezi kuitegemea Serikali peke yake kuajiri watu wote, haitawezekana. Watanzania ni wengi, wote wanahitaji kufanya kazi. Ni wajibu wa Serikali kuratibu kwa mujibu wa Katiba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufanikisha hili, tulitangaza vita vya ukombozi wa Afrika na tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa, Tanzania ikiwa inaongoza ukombozi. Sasa ukombozi ule ulikuwa wa kuleta uhuru, sasa hivi tunahitaji ukombozi wa uchumi, na kubwa zaidi ni ukombozi wa fikra za Watanzania ili Watanzania hawa waone fursa na Serikali iwasaidie hizo fursa waweze kujenga uchumi imara.

Mheshimiwa Naibu Spika, bila sisi kufungua fikra zetu, bila sisi kufungua nchi hii yenye baraka, nchi hii ambayo ina ardhi nzuri yenye rutuba, ina madini, ina milima, ina maji, ina mbuga za Wanyama, ina kila kitu; Watanzania hatustahili kuwa masikini. Umasikini wetu lazima tukae chini tuone tunautatuaje ili nchi hii iweze kuwa ni yenye uchumi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kusema, nchi yetu sasa hivi tutangaze vita ya kuja na ukombozi wa kifikra wa Watanzania ili tujenge uchumi wetu. Nchi yetu tunahitaji maendeleo ya watu, tunahitaji maendeleo ya nchi. Nami naamini, kama tutakaa chini na kutafakari haya, Tanzania itakuwa ni nchi bora katika Afrika na duniani. Moja, ni mahali pazuri pa kuishi; pili, ni mahali pazuri pa kufanya kazi; tatu, ni mahali pazuri pa kukaa; na Tanzania ni mahali pazuri pa kuwekeza. Tukijiona hivyo, nchi yetu itafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini dhamana hii Mheshimiwa Waziri Mkuu anayo, ataweza kuifanya vizuri kwa kushirikiana na Mawaziri, kwa kushirikiana na Serikali kwa ujumla, na kwa kushirikiana na Watanzania wote wenye uwezo, wenye weledi, wenye utaalamu wa kila namna, ili nchi hii tuisukume mbele tupate maendeleo, tuondokane na umasikini, tulete miradi ya maendeleo, tuwasaidie wananchi wa Vwawa, wananchi wa Tanzania, wananchi wa Mkoa wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)