Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa kuanza na mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa anayoyafanya katika nchi yetu. Uongozi wake unalifanya Taifa letu limeendelea kuwa tulivu sana, na hata pale tunapopata changamoto kubwa hizi za mijadala ya kisiasa bado nchi yetu imetulia sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhusu Hassan kwa miradi mikubwa ambayo amatuletea katika Jimbo la Kilimbero; na hasa hasa ametuletea viongozi makini wa Mkoa wa Morogoro. Ametuletea Mkuu wetu wa Mkoa Mama Fatma Mwasa na Mkuu wa Wilaya mpya Wakili Dunstan Kiobya; kwa kweli wanafanya kazi kubwa nzuri. Tunawaombea afya ili waendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni Bunge la Bajeti tunajadili mambo ya bajeti, na katika bajeti ni mipango na matumizi. Kama nilivyosema awali, ni kwamba kuna aina nyingi za bajeti lakini katika nchi yetu tuna bajeti ambayo tunapanga matumizi mengi halafu baadaye tunatafuta vyanzo vya fedha. Sasa katika Hotuba ya Mheshimiwa Rais juzi akipokea taarifa ya CAG ametuonesha njia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwambakuna sehemu tukiwekeza, tukiacha uoga tutapata takriban 50% ya bajeti ya nchi yetu. Mheshimiwa Rais anasema tuache uoga katika uwekezaji wa bandari; 50% anayosema Mheshimiwa Rais tuna bajeti takriban ya trilioni 40 hapo. Mheshimiwa Rais anazungumzia trilioni 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi kama Wabunge katika vitu ambavyo tulitakiwa tuvikimbize ni kuhakikisha hii trilioni 20 ya bandari tunaipata kwa wakati. Kwa sababu mambo mengi tunayozungumza hapa, tunaomba na mimi nitasema mengine ya kuomba hapa. Kwa hiyo naishauri Serikali, namshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu, leteni marekebisho kama ya Sheria ya Ununuzi ya kukaribisha hawa wawekezaji wanaotakiwa. Wabunge tumetembea hapa tumeona nchi za wenzetu wanavyowekeza katika bandari na matrilioni ya fedha wanazopata. Sasa kama una gari sasa hivi pale inatupa trilioni moja, kuna mtu anaweza akaja akatupa trilioni 10 ama 20 ni kitu cha kufanya haraka; trilioni si fedha ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda India; pale Mundra miaka 20 iliyopita ilikuwa pori, sasa hivi wana port ambayo inaongoza kwa mapato India na Asia. Sisi tuna Bagamoyo pale tunajadiliana tu, waoga, bandari isibinafsishwe. Mheshimiwa Rais amefafanua vizuri sana; tuache uoga, tuwekeze, tuwape watu wenye mifano ya kuendesha bandari duniani tupate pesa. Wabunge tunalalamika hapa kituo cha afya, mama ana-click tu unapata kituo cha afya. Mimi namshukuru sana Mheshimiwa Rais pale sasa hivi ameteua wakurugenzi wa bandari ile vijana wadogo kama mimi hivi lakini ukiwasiiliza unajua hawa ni watu wa biashara na hawataki mchezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaomba sana. Kabla sijalalamika mambo mengine huko na kuomba fedha anzeni mambo pale, sheria zije hapa kama za ununuzi zina mchakato mrefu zibadilishwe ili uwekezaji ufanyike tupate fedha; hilo la kwanza la mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nilitaka kuzungumza kuhusu maadili kama wenzangu walivyosema hapa. Kuhusu hili jambo la maadili nafikiri sidhani kama sisi Wabunge tunapata muda wa kuzungukazunguka Dar es Salaam tu peke yake. Mimi nilikuwepo wakati ule Makonda anaanza kufanya yale mambo ya kupambana na hawa watu na jambo hili. Najiuliza kwa nini Tanzania sisi hatunyooshewi vidole na nchi hizi ambazo zina-support ushoga duniani. Kuna sehemu hatujafanya vizuri, ni kama jambo hili linachekewachekewa. Mimi nina watoto wawili wa kiume nikiwaangalia watoto wangu nikisoma vyombo vya habari, ni jambo la hatari; na viongozi wetu muwe makini sana kwenye harusi mnazokwenda. Mnaenda kwenye harusi mnasherekea harusi, mnacheza pale unashangaa wale watu wanakuzunguka pale picha inarekodiwa zinasambazwa huku mnaonekana na ninyi viongozi mna-support jambo hilo. Jambo la hovyo la mambo mabovu ya maadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, katika East Africa tukigawanyika katika kutetea jambo hili tumeumia. Tazameni Uganda kinatokea nini kwa Museveni. Museveni alivyoanza ku-fight jambo hili nini kinampata? East Africa sisi tumekaa tunaziangalia namna gani. sasa kuna mwanasheria mmoja ametushauri Wabunge, ameandika hapa amesema sheria yetu peke yake itakuwa ngumu sana ku-fight mambo haya ya ushoga na mambo ya jinsia moja. Akasema kifungu 154 cha sheria kinazuia kuingilia kinyume cha maumbile, hakizuii ushoga mwandishi kafafanua kwa ufupi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja nisome. Anasema kifungu cha 154 cha Kanuni za Adhabu kinazuia mwanaume kumwingilia mwanamke kinyume cha maumbile na mwanamume kumwingilia mwanamke kinyume cha maumbile. Adhabu ya kosa hili ni kifungu cha miaka 30 yamkini kifungu hiki hakiwezi kuzuia ushoga kwa sababu ili mtu apatikane na hatia ni hadi athibitishe kuingilia, anus penetration. Sasa nani atathibitisha kuingilia kati ya aliyeingiliwa na aliyeingilia wakati wote wanafanya kwa hiari. Kifungo hicho kinashindwa kuanzia hapo, hii maana yake hata ukiwaona wanafanya bado unashindwa kuthibitisha kuingilia hata hivyo utawaona wapi wakifanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uganda adhabu ya kuingilia ni hadi miaka 10 wakati kwetu ni maisha ama miaka 30. Hata hivyo Uganda wanafanikiwa kuzuia matendo haya kwa sababu sheria yao haijaishia kwenye kuingilia watu wao wanashughulikia matendo ya ushoga na usagaji kwa ujumla wake wakati huku tunashughulikia kuingilia ni maelekezo mawili tofauti. Mwanasheria anasema; na ndio hii sababu unaona sisi tuna adhabu kubwa lakini hatupingwi, hatupigiwi kelele za kimataifa na wanaotetea ushoga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, anaendelea kusema ni kwa sababu wanajua kuwa sheria ya Uganda inaweza kufuta janga hili wakati ya kwetu haiwezi. Uganda kuingilia kinyume cha maumbile ni kosa, kuonesha ama kuvaa au kufanya kiashiria chochote cha ushoga na usagaji ni kosa, kujitangaza kuwa ni shoga ama msagaji ni kosa. Mwenye nyumba, mwenye hoteli, lodge, gesti kumpangisha shoga na msagaji ni kosa. Kuvaa mavazi yanayoashiria mwanamme kuwa shoga au mwanamke kuwa msagaji ni kosa, kaka zetu wanabinukabinuka huko mtaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo chochote cha habari ama mtandao wa kijamii kumtangaza katika namna yoyote kukubali vitendo hivyo ni kosa na mengine mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uganda ushahidi wa kimazingira unaweza kukuwajibisha kuwa ni shoga. Hatuwezi kuishia kuzungumza kuwa hata wanyama hawafanyi hivyo halafu ushoga ukaisha, tunahitaji hatua za kisheria za kushughulika na watu hawa. Wako huko kwenye maharusi, wako huko mjini watoto wa kiume wanavaa blauzi, wanabinuka binuka, wawakamate, watengeneze jopo la Madaktari, wathibitishe, wawafunge. Waziri Mkuu ni Muislamu, Rais Muislamu, Dkt. Mpango Mkristo, Mwenyezi Mungu, atawauliza wakati wamepewa madaraka ya kuongoza nchi hii walichukua hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata semina moja ya Mzee Kinana anasema kuna namna nyingi, ninyi ambao mna machine tools za ku–deal na mambo hayo wanaweza wakafanya wakapotea watoto wa kiume wanaovaa magauni na kubinuka mjini. Waende kwenye maduka Sinza watazame watoto wa kiume wanabinuka binuka hovyo, wanavaa vibatiki, sidiria, watoto wa kiume! Sasa sheria zetu haziwezi kufanya hivyo, tunapiga piga mark time hapa, walete sheria kwamba uki–post unakamatwa, tabia zako hazieleweki unakamatwa, jopo la Madaktari wanakaa wanathibitisha. Watazame sheria ya juzi Mahakamani pale, yale mambo ya Zanzibar anasemaje yule mtalam pale, anasema: “Ninachoweza kuthibitisha ni kwamba tundu la huyu mtu unaweza kuingiza vidole viwili.” kaishia pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wanavaa blauzi, kwani sisi tunakereka na ushoga kwa taarifa ya Mwakyembe na zile taasisi kwa sababu gani? Kwa sababu watu wanaonekana, sikilizeni taarifa ya Mwakyembe, sikilizeni yule dada na yule aje afanye presentation hapa mwone. Usiku kuna mzungu Masaki huko anakusanya mashoga wanafanya party. Sasa hili ni jambo ambalo kama tunakereka nalo, Serikali wana machines, watumie kwa hawa, wawapakie kwenye malori, wawapeleke kwenye magereza, sisi Idete kule, Kilombero kule magereza yetu ndiyo magereza yanayoongoza kutokuwa na watu wa kutosha, wawalete kule wawafunge na mashamba ya kulima yapo, unalima na jembe futi moja hivi, waje kule walime. Watu wanachezacheza hapa ushoga, ushoga, tunalalamika tu, wawakamate hao watu wawatie ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kwa sababu ya muda, nataka kumshukuru Mheshimiwa Rais, kwa miradi mikubwa ambayo ametuletea lakini hasa hasa niseme kuhusu Barabara yetu ya Ifakara – Kidatu, kweli Mheshimiwa Rais ametusaidia. Utakumbuka nilitaka kukaa chini kwenye kapeti hapa kuhusu Barabara yangu ya Ifakara – Kidatu, lakini tangu Mheshimiwa Rais Samia ameingia miaka miwili hii tayari nina kilomita 42 katika kilomita 66 za lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wakati huu tayari tumeshapata bilioni 42 za Mradi wa Maji wa Kiburubutu. Nimejulishwa hapa tayari tuna pesa ya VETA iliyoenda kujenga Chuo cha VETA pale Ifakara ambapo advanced milioni 45 imeenda kwa ajili ya ku–clear eneo na tumepata Mahakama mpya. Namshukuru sana Waziri wa Mambo ya Ndani alikuja Kilombero na ni imani yangu atatusaidia kupata Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali katika mikakati yake ya Kilimo, Waziri Bashe, ametuambia kwa mara ya kwanza Serikali itaanza kununua mpunga kwa bei nzuri, tunaomba mbolea iwahi, tunaomba suala la wakulima wa miwa lifanyiwe kazi, tunashukuru kwa kiwanda cha sukari kipya kinaendelea, tunaomba kikamilike kwa wakati, tunashukuru Mheshimiwa Rais, kwa sekondari nane mpya tumejenga. Tumejenga zahanati nne, tumejenga vituo vya afya viwili, juzi ametuingizia milioni 300 Ifakara za sekondari, ametupa milioni 470 za sekondari advanced, ametupa milioni 500 juzi la Jengo la Mama na Mtoto katika halmashauri yetu na ametupa bilioni 13 za Mradi wa Substations ya kukuza umeme Ifakara, ametupatia lami kilomita mbili Ifakara, ametupatia lami Mwaya na mambo mengi Mheshimiwa Rais, ametusaidia kufanya. Tangu dunia iumbwe Halmashauri ya Ifakara na Wilaya ya Kilombero haijawahi kupata fedha nyingi kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya alikuja Ifakara, akatembelea St. Francis Hospitali, ni Hospitali ya Rufaa, hospitali ambayo inasaidia halmashauri tano na wilaya tatu, Baba Askofu pale anaomba msaada kwa sababu tunashirikiana na Serikali CT–Scan, MNRI na Ultrasound za kisasa, naomba Waziri awasaidie, kama alivyofika pale ametembelea, ameona hali halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba viwanda, tuna majengo tayari ya viwanda. Kutokana na kwisha kwa muda naunga mkono hoja. (Makofi)