Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanya. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi ambazo anaendelea kufanya; na wananchi na watu wema wa Jimbo la Geita Mjini wanamkumbuka na wanamshukuru kwa ziara yake ambayo aliifanya mwaka jana na wanaendelea kuitakia mema Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa taarifa yake nzuri kwenye bajeti aliyoisoma kwa utekelezaji wa shughuli mbalimbali. Wananchi wa Geita wanaishukuru Serikali kwa kukamilika kwa hospitali yao ya mkoa ambayo imeanza sasa kufanya kazi za nje, kazi za OPD, wanaomba tu ikamilike ili iweze kuingia kufanya kazi kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa mradi wa maji wa takribani bilioni 100 ambazo Mheshimiwa Rais alitupatia, na mkandarasi yuko site na anafanya kazi. Tunashukuru Serikali kwa fedha za barabara kupitia mradi wa TACTIC ambao tayari wakandarasi wametangazwa na wanaanza kufanya kazi. Wananchi wa Geita wanaishukuru sana Serikali kwa fedha za stendi ambazo taratibu za TAMISEMI zinaendelea. Wananchi wa Geita wamenituma nikuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu ombi lao la Mji wa Geita kuwa Manispaa, taratibu takriban zote zilikwishakamilika wanakuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo hili likamilike kwenye mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais kule Kagera akizungumza kuhusu kuhamasisha watu kuwekeza na kulipa kodi alitoa maelekezo kwa TRA kuachana na madeni ya zamani na kuhangaika na kuhamasisha watu katika kukusanya kodi kwenye makadirio mapya. Sasa ilikuwa ni ombi langu Mheshimiwa Waziri Mkuu; tunayo shida kidogo pale Geita. Mfanyabiashara anapofanya biashara na Mgodi wa GGM anapotoa invoice anatoa na risiti, anapotoa risiti inakuwa ina VAT lakini walipaji wanaweza kuchukua siku 30 mpaka 90 na wakati mwingine ikitokea dispute hawalipwi kabisa. Mfanyabiashara anaingia kwenye deni la TRA, inatokea mfanyabiashara anakamatwa wanawekwa ndani wanashtakiwa kwa fedha ambayo hajawahi kukusanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili likienda sambamba na maagizo ya Mheshimiwa Rais; na ndiyo maana kuna madeni mengine yana miaka miwili miaka mitatu, wako wanye kesi mahakamani lakini kimsingi watu hawa hawajawahi kulipwa na GGM. Kwa hiyo ni ombi langu agizo hili la Mheshimiwa Rais liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili limezungumzwa hapa suala la BBT. Kwanza naipongeza sana Wizara kwa kuja na huo mkakati wa hayo makundi maalum kwa ajili ya kilimo. Nimeangalia malengi mahususi, kwamba ni kutoa mafunzo, kutoa mitaji, kutoa mashamba na kutafuta masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata tabu kidogo juu ya sustainability ya zoezi hili. Kwanza, tumetenga heka 400, tumeziona pale Dodoma tunaanza. Natamani kujua kwenye mpango kila mwaka tutatenga shilingi ngapi ambazo zitakuwa zimetengwa kwa zoezi hili kwa nchi nzima? tunataka kuona katika halmashauri zote pana mashamba; kama alivyosema mchangiaji mwenzangu kutoka Itigi. Kwamba tunakuwa na mfumo ambao tutapata hao vijana katika halmashauri zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kinachofanyika ni collaboration ambayoo nina uhakika sustainability haiwezi kudumu kwa sababu tumekusanya watu waliokuwa wanatafuta ajira, tukawapa kazi lakini wamevutiwa wakiamini kwamba Serikali itaendelea kutoa pesa kwenye zoezi hili. Pale ambapo mrija huu wa Serikali utakapokatika hawa watu watarudi kwenye vijiji vyao. Nimeangalia kwenye orodha nzima watu walioko kwenye halmashauri yangu ni watatu, kule kwangu mashamba haya yako wapi? Kule kwangu mkakati wa kuja ukoje na mkakati wao umepangwa kudumu kwa muda gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano; zimeandaliwa takribani heka 47,000 lakini tatizo la ajira lipo leo, liko mwakani na liko mwaka unaofata. Kwa nini mashamba haya yasingebaki kuwa ya Serikali tukawa na vijana wanaofundishwa labda kwa program maalum kwa miaka mitatu, halafu wana-graduate wanaondoka wanakuja wengine kwenye kila halmashauri? Sasa hao uliowapa hizi ya miaka 60 au 90; kwanza sasa hivi wana miaka 30, sasa baada ya miaka 30 watakuwa wazee kuliko karibu watu wote tulioko humu ndani, halafu maeneo ya mashamba ya kuwapa vijana wengine itakuwa hayapo. Huo mpango uliopo wa kuwapa lease ya kudumu unawapa na hati halafu baadaye watakuwa na miaka 100 itakuwa shamba moja linamilikiwa na wajukuu 200 na hao wajukuu 200 wametoka Tanzania nzima kwa sababu bahati mbaya tunawachanganya kutoka mikoa yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni maoni yangu kwamba jambo hili ni zuri lakini liandaliwe katika mfumo ambapo litapelekwa kwenye kila halmashauri na halmashauri zile zitumiwe kama mashamba darasa lakini kuwe na mpango endelevu. Naitazama hii kama tulipoanza na ile kilimo kwanza ikaja big result. Vilikuja na presha sana halafu baadaye ikapita kwa sababu hatukuangalia sustainability.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiri jambo hili ni la msingi sana na liangaliwe vizuri. Kwenye ajira; ukiingia kwenye mfumo wa usajili wa ajira.com ukijaza zile credential zako zile za kwamba wewe una bachelor, ukirudi siku nyingine na umesema degree nyingine ule mfumo hakukubalii. Ukiwa umesoma diploma ule mfumo hakukubalii. Kwa hiyo siku ukijaza ule mfumo kwa mara ya kwanza ule mfumo kila unapotaka kuingia kurekebisha zile taarifa ulizonazo wewe mfumo unakataa. Vijana wengi kwenye soko la ajira ni mult- professional. Wanachokifanya, akisoma procurement, akasoma ualimu, akasoma project management akakosa anaamua kusoma profession nyingi. Sasa, ukishaingia mara moja ukajisajili ukirudi mara ya pili mfumo unakataa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo ombi langu ni kwamba mfumo huu uruhusu mtu kuingiza credentials zake hata kama ziko saba; kama amesoma certificate, diploma au amesoma digrii tatu aweze kuingia mle ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu VETA. Pale Geita Mjini tumejenga VETA, naishukuru sana Serikali. Mradi huu ulianza mwaka 2017/2018, leo ni 2023 Mheshimiwa Waziri Mkuu VETA haijakamilika. Majengo yapo, nyasi zimejaa na hakuna mwanafunzi. Tulio-target mwaka 2018 alipokuwa anamaliza form four, darasa la saba; sasa mwingine amemaliza chuo kuu, na kama yuko uraiani amekwishakata tamaa. Hivi mpango gani huu wa Serikali ambao hauna timeframe? Yaani mnataka tu kujenga tu ilimradi tu mnajenga haijulikani itafunguliwa lini, haijulikani vifaa vitakwenda lini, haijulikani training itaanza lini; ilimradi tuna taarifa tumejenga VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali; tulikuwa tunajenga mwanzo kwa mkopo wa African Development Bank hela ikarudi, tukachukua hela za Uviko tukapeleka fine, tumebadilisha design na mambo mengine. Naomba bajeti hii ije na bajeti ya vifaa ili chuo kile kianze. Kuna vijana wengi sana pale ambao wanatafuta kazi, wanakosa kazi kwenye migodi mbalimbali kwa sababu tuliazimia kuwa na VETA tuweze kufundisha zile skills ambazo zinatakiwa na mgodi pale na migodi mingine inayozunguka maeneo yale. Sasa leo mwaka wa sita tunazungumzia chuo ambacho hakikamiliki. Naomba sana jambo hili liweze kukamilika, lakini isiwe tu kukamilika iweze kukamilika kwa design iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne; juzi nilikuwepo kwenye uzinduzi wa upandaji miti ambao umeratibiwa na watu wa STAMICO, nawapongeza sana. Siku ile pia walikuwa wana-advocate makaa yao ya mawe ya Rafiki Briquettes. Kwanza napongeza sana juhudi hizo za watu wa COSTECH ambazo zimeendelea, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, shida yangu ni moja Rafiki Briquettes ni inatokana na mawe ambayo ni Wizara ya Nishati, watu wa STAMICO wanayo; lakini wanafanya kazi hiyo kwa ajili ya kusaidia kuongeza nishati, watu wa nishati wamo, wanasaidia kupunguza ukataji miti; watu wa misitu wapo kwa ajili ya kuokoa mazingira. Kwa hiyo jambo hilo linahusisha wizara nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ombi langu, hizi wizara nne zingetafuta namna ya kuli-coordinate hili jambo kusudi likapata mtu mmoja wa kulisimamia. Namna lilivyo sasa litapotea hewani halafu utabaki kuwa mtaa wa maonesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana ahsante sana. (Makofi)