Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jambo la kwanza naomba niunge mkono hoja iliyoko mezani. Naunga mkono hoja kwa sababu ripoti inaonyesha mambo mengi yamefanyika ni mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na mambo machache sana ya kuzungumza. Jambo la kwanza ni kumpongeza Mheshimiwa Rais. Kwa niaba ya Wananchi wa Makete tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi ambazo anazifanya na hata kwa hatua ambazo anazichukua dhidi ya watu ambao wanaonyesha kabisa wakimvuta shati na kumrudisha nyuma hasa hasa haya mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye taifa letu. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwa miradi ambayo anaileta kwenye Jimbo langu la Makete. Sasa hivi tuna mradi wa Barabara ya kutoka Mbeya kuelekea Makete, barabara ya kiwango cha lami na mkandarasi alishasaini tayari barabara ile lakini niombe tu kwamba Serikali hii mikataba ambayo imeshasainiwa Serikali iweze kutoa advance payment kwa wakandarasi ili ziweze kujengwa kwa kasi kwa sababu barabara hii hadi sasa mkandarasi bado anasua sua kutokana na kwamba hajalipwa advance payment ili aweze kuanza kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali iweze kushughulikia hilo jambo ili barabara ile iweze kujengwa kwa sababu ni barabara ya kiuchumi na ni barabara ya kimkakati na ni barabara ambayo kwa Jimbo la Makete wananchi wangu wanaisubiri kwa hamu sana ili iweze kutekelezeka na shughuli za kiuchumi ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kuzungumzia nataka kuzungumzia kwenye suala moja linalohusu Kariakoo. Naizungumzia Kariakoo kwa sababu karibia 50% ya wafanyabiashara wa Kariakoo ni Wananchi wa Wilaya ya Makete na ni wananchi ambao wanafanya kazi pale lakini pia Kariakoo ni moja kati ya kitovu cha uchumi cha Taifa letu. Kwa hiyo, nazungumzia Kariakoo kwa mantiki hii hapa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimeiita hii; how TRA is trying to kill Kariakoo, yaani nimejaribu kuielezea jinsi gani TRA wanajaribu kuimeza na kuiua Kariakoo sehemu ambapo tunategemea kama Taifa tunapata mapato yetu mengi kwenye ukusanyaji wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nina mambo matatu makubwa ya kuizungumzia Kariakoo; jambo la kwanza, Kariakoo ilikuwa inafanya vizuri sana kwenye soko la vitenge. Katika ukanda wa Afrika Mashariki Kariakoo ilikuwa inaongoza kwenye soko la kitenge lakini leo ninavyozungumza soko la kitenge Kariakoo limekufa. Kwa nini limekufa? Limekufa kwa sababu ilipitishwa Sheria hapa ya Ongezeko ya mita moja ya kitenge kutoka dola 0.4 kwenda 0.8 kwa maana kwamba 100% ya ongezeko kwa minajili ya kwamba tunalinda viwanda vya ndani lakini nikuelezee tu leo hii ukienda Zambia, ukienda Congo, ukienda Malawi ndiko vitenge vinakouzwa zaidi kuliko Dar es Salaam – Kariakoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wafanyabiashara wa Kariakoo wengi wamepoteza vitenge, wamepoteza mitaji tumeua Soko la Kariakoo. Kwa hiyo, TRA kwa kulinda viwanda vya ndani ambavyo pia havitoshelezi soko wameweza kuizamisha Kariakoo kwenye soko la vitenge leo hii mapato kupitia vitenge hatuwezi kuvipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la tatu, Kariakoo inakufa, kwa nini inakufa? Ukienda leo hii kuna suala la wafanyabiashara wa kigeni. Wafanyabiashara wa kigeni wananunua sana mizigo kwenye Soko la Kariakoo, mizigo yao mingi ni whole sale. Wakinunua TRA wamekaa kuvizia, wanavizia kwa ajili ya kuwakamata, wakiwakamata wanasema mzigo wako ulionekana ni mkubwa risiti ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali ni vyema wakatafuta utaratibu mwema jinsi ya ku-deal na suala la ukusanyaji wa mapato kwenye Kariakoo. Wafanyabiashara wengi wamepungua wa kigeni wanakimbia, wako ndani, bidhaa zao zimeshikwa wanashindwa tena kurudi kufanya kazi kwenye Soko la Kariakoo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti niiombe TRA na Mheshimiwa Waziri Mkuu anatusikia, ni vyema kuweka kikosi kazi maalum cha kwanza kuangalia jinsi gani wafanyabiashara wanavyoweza kufanya kazi hasa hasa hawa wafanyabiashara wanaotoka nje kuja kununua mizigo kwenye Soko letu la Kariakoo ili Kariakoo iendelee kubaki salama iweze kuendelea kuilisha Taifa letu tubaki kwa na brand kwenye nchi yetu. Tofauti na hapo kuendelea kuvizia wafanyabiashara wa kigeni, wamenunua mizigo uwakamate tunaendelea kuiumiza taifa, tunaendelea kuiumiza Kariakoo ambacho sisi kwetu ni kitovu cha uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili niombe sana Serikali ilichukue katika uzito mpana sana. Hatuyasemi haya kwamba labda tunalengo baya na TRA, tunayasema haya tuna malengo mazuri. Ng’ombe yoyote unayemlisha lazima akutolee maziwa vizuri. Sasa hawa wanakamua tu, wanakamua tu lakini hawatengenezi mazingira mazuri ya kuiona Kariakoo inazidi kuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine juzi TRA wametoa waraka kuhusu consolidation. Utaratibu wa nyuma wote ulikuwa unaonyesha nina bidhaa naenda kununua China kwa mfano. Naungana na mwenzangu labda wawili, watatu tunaagiza mzigo kwenye container moja tunalileta Kariakoo. Watu wa cargo consolidation wanaweza kulishughulikia container na mizigo nikapata. Juzi umetoka waraka wa kwamba wafanyabiashara wote mnaoagiza mizigo China ni lazima mizigo yenu ikifika hapa kila mtu alipie kwa mzigo wake pale bandarini. Kwa maana ya kwamba mizigo ikifika inamwagwa, mfanyabiashara analipia pale mzigo wake ndiyo atoe aende nao kwenye soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu hiki kinaenda kuimaliza Kariakoo kabisa. Ninalisema leo hapa na kesho kutwa yatakuja kutokea. Nimeagiza piece 500 za mzigo, siweze kwenda tena bandarini nikaanze kusema jamani mzigo wangu ni huu hapa naomba nilipie. Tuna manpower gani bandari yetu ya kwamba imwage container mfanyabiashara aanze kuchagua mzigo pale ili aweze kulipia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi zote ni bureaucracy za kutengeneza za kuiba, bureaucracy za kupoteza mizigo ya wateja, bureaucracy ya kuhakikisha wafanyabiashara hawakui, bureaucracy ya kuhakikisha Kariakoo inakufa, bureaucracy ya kuhakikisha kwamba watu wanajilimbikizia mali wanatafuta kupitia Soko la Kariakoo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Wizara iangalie hili jambo. Ni jambo ambalo linaenda kuua wafanyabiashara kwa sababu hatuna manpower ya kutosha ya bandari yetu kumwaga mzigo chini ili kila mfanyabiashara aanze kulipia mzigo wake aliouchukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ruhusuni cargo, hizi cargo hawa Watanzania wenzetu wamefungua cargo ziweze ku- facilitate hilo jambo. Kutengeneza hizi bureaucracy ni kuendelea kulifanya Taifa letu liendelee kudidimia. Kwa hiyo, haya mambo matatu if you don’t take care kwenye haya tunaenda kuizamisha Kariakoo. Kariakoo is our brand, Kariakoo ni chanzo chetu, Kariakoo ni eneo letu, TRA inafanya kazi vizuri ya kukusanya mapato lakini watendaji wao wa chini wanaenda kuizamisha Kariakoo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ni suala la maadili na malezi. Kama kuna mambo makubwa mawili kwenye nchi yanayotikisa kwa wakati huu ni suala la maadili na mmomonyoko wa malezi ya watoto wetu. Sisi ni Bunge hapa leo tunazungumza mambo mengi sana ya msingi kwa ajili ya Taifa letu lakini nakuhakikishia miaka 30 ijayo, miaka 40 ijayo kama suala la mapenzi ya jinsia moja hatutaipigia kelele, sisi Wabunge hapa miaka 30 ijayo, miaka 50 ijayo, tunaweza kuja kuwa na viongozi ambao wako kwenye sekta hiyo ya mashoga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo…

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mchangiaji wakati anaifikiria miaka 30 ijayo na siye Wabunge tupo, si tukubaliane tu hapa kwamba tukipima mtu akaonekana anafanya mambo yale anyongwe tumalize kabisa? Tutakuwa tumekomesha kuliko haya ya kusubiri miaka 30. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa unaipokea hiyo taarifa?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anaongea jambo la msingi sana na tuna sheria zetu kwa maana ya kwamba kuna sheria zinazosema ni miaka 30 au kifungo cha maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijidai kama hapa sisi ni vipofu hatuoni kinachoendelea kwamba kwa sababu ni Mbunge ninauwezo wa kum-protect mtoto wangu akawa anaishi mazingira mazuri anasoma shule nzuri. I am telling you, ubunge wetu ni sisi ni kwa sababu ya wananchi walioko kule mtaani ambapo haya wanayashuhudia yanatokea na sisi tuko kimya. Ni vyema kama nchi tukaanza kuchukua hatua immediately. Huu siyo utamaduni wa Kiafrika hata Biblia inakataa, hata Qurani inakataa. Miaka 30 ijayo nusu ya Bunge inaweza ikawa mashoga wamekaa hatuwezi kuwa na Taifa kama hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajenga SGR, tunajenga hizo airport, Mheshimiwa Rais ana-invest fedha nyingi kwenye miradi. Tunakuja ku-invest kwa ajili ya kizazi kipi? Leo nina watoto wangu. Watoto wangu nisipowalinda, watakuja kudondokea kwenye huu mtego.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana lazima tuanze ultimatum kama nchi ya kwamba Taifa letu kwenye suala la malezi ya watoto limebadilika. Lazima tuanze mfumo wa tofauti kuhakikisha kwamba tuna-protect kizazi chetu. Tofauti na hapo kwa sababu ya misaada, kwa sababu tunapewa fedha, kwa sababu ya nini tuwe tayari kuachia damu zetu ziingie kwenye Sodoma na Gomora. Hiyo ni kitu ambacho hakiweze kuruhusiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama makanisa hayatasimama, kama Bunge halitasimama, kama misikiti haitasimama kuna siku misikiti na makanisa na Bunge vitaongozwa na watu ambao wako kwenye upande huo. Niombe tuchukue hatua kali dhidi ya watu hawa. Nimshukuru sana Mkuu wa Wilaya mmoja amefuta taasisi mojawapo. Juzi kuna kesi imetokea kule Mtwara mtu amefungwa. Tuanze Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi kila mmoja kwa nafasi yake alipo tutakuja kupata viongozi wa Jeshi, niliona ile takwimu imetoka jeshini wamepima waliokwenda jeshini wamekuta wengine wako kwenye upande huo. Tutakuja kupata jambo gani? Lazima tushughulike na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe kama Mbunge kwa niaba ya Wananchi wa Makete, sisi Wanamakete suala la ushoga tunasema no, suala la mapenzi ya jinsia moja tunasema no, Biblia na Quran havijatutuma huko, msingi wetu ni kuhakikisha kwamba tunazaliana. Na mnajua kwamba vita yote hii ni kwa sababu Afrika tunazidi kuwa wengi, Wazungu wanajaribu ku-impose taasisi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuamini kwamba adui ameonyesha mlango aliopo na sisi tuonyeshe silaha tulizonazo kuukataa ushoga. Msaada wowote wenye element hizo Serikali tunaomba isiwe sehemu kwa sababu hautakuwa na baraka katika Taifa letu. Hatuwezi kuruhusu kizazi chetu kikapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niende kuunga mkono hoja, niishukuru Serikali kwa ajili ya Jimbo la Makete na miradi ya maendeleo inayokuja. Niseme, tunawakati wa kuilinda Kariakoo lakini pia maadili na malezi kwa watoto wetu lazima tusimamie. Sisi kama Wabunge lazima tuonyeshe upande wetu ni upi nalitetee Taifa letu. (Makofi)