Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Aloyce Andrew Kwezi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi njema anayoifanya katika nchi yetu ya kutuletea maendeleo ya kweli. Nitakuwa sijatenda haki endapo sitampongeza Mheshimwa Waziri Mkuu kwa ripoti yake nzuri sana, ripoti ya Waziri Mkuu na bajeti yake hapa kwa kweli ni ripoti ambayo imekwenda shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kuchangia katika sekta ya Maliasili. Jimbo la Kaliua limepakana na Hifadhi ya Ugalla, Hifadhi ya Kigosi ambazo zote hizi ni National Parks, pia Jimbo linalo ofisi za TAWA na TFS. Nimesimama ili tuweze kujenga hoja na kushauriana mambo mbalimbali kwa ajili ya kuwashauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Mawaziri lilifanya maamuzi katika vijiji 975 katika Jimbo la Kaliua na katika Wilaya ya Kaliua liliachia vijiji na kuvitambua vijiji 29, walipokuja timu ya Mawaziri Nane, mimi ni miongoni mwa mashuhuda ambao nilishiriki mchakato mzima katika Jimbo la Kaliua, Mkuu wangu wa Mkoa Dkt. Batilda Buriani ameshiriki mwanzo mwisho, Mwenyekiti wa Chama wa Mkoa naye alishiriki mwanzo mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ambayo ninaijenga inahusiana na Kata inaitwa Ukumbisiganga. Katika Kata ya Ukumbisiganga kuna vijiji viwili, Kijiji kimoja kinaitwa Kumbikakoko na Kijiji cha pili kinaitwa Usinga, Vijiji hivi kwa sasa kumeibuka mgogoro mkubwa sana lakini mgogoro huu umetokana na tathmini iliyofanywa na wataalam. Baraza la Mheshimiwa Rais ameruhusu na kuvitambua vile vijiji ambavyo vipo pale toka mwaka 1974, walikuja wakatangaza wananchi kaeni, tulieni, Mheshimiwa Rais amesikia kilio chenu lakini bado amewaonea huruma na mimi nikashukuru kama Mbunge wao, bado chama kikashukuru kwa mapenzi mema ya Mheshimiwa Rais wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho kimekuja kutokea hivi sasa ni ile timu ya tathmini imekuja na mapendekezo ambayo ninaweza nikasema kwamba yale mapendekezo sijawahi kuona na nimeona ni kama vile hizi shule kwa kweli saa nyingine hazitusaidii. Hizi shule hazitusaidii kwa sababu gani? Agizo limesema wananchi wakae, wamegewe maeneo lakini badala ya kumegewa maeneo nini kimekuja kufanyika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wananchi kaya 318 kwenye Kijiji cha kwanza kinachoitwa Ukumbikakoko zimependekezwa zitoke Ukumbikakoko ambapo almost ni Kijiji kizima hicho, maana yake ni tofauti ninaona kama vile kijiji kinafutwa sasa, ziondolewe Ukumbikakoko ambayo ndiyo mwisho jirani na Mpanda, kwa hiyo mtu anatoka Makao Makuu, kutoka Makao Makuu ya Kata mpaka ukafike Ukumbikakoko ni kilometa 38. Sasa mapendekezo badala wamegewe yale maeneo ambayo yalikuwa yamependekezwa na hakuna mgogoro wowote, wanasema kaya 318 zitoke pale Ukumbikakoko zivuke Kijiji cha Usinga, zivuke Makao Makuu ya Kata, zivuke Kijiji cha Lumbeyi ziende kuingia kwenye Kata nyingine inaitwa Zuginole kilomita 58 kutoka Kijiji kilipo, halafu zile kaya zinazohamishwa hizo 318 kila kaya iende ikapewe heka tano tano, nilicheka nikasema hii ndiyo shule haijasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwenye vijiji tujiulize Waheshimiwa Wabunge wote tunatoka kwenye vijiji, mimi ukiniuliza katika Kijiji ambacho natoka kwenye eneo la Baba yangu ni zaidi ya heka 1,000 familia nzima tunalima pale, kwa hiyo kaya moja na kaya za kule ninavyowaambia Kaliua kwa Sensa iliyofanyika ina watu 668,000, badala tufikirie kwamba tutawasaidia hawa sasa hii ni allocation mbovu. Eneo lipo pale wazi badala waongeze lile eneo ambalo lipo jirani pale wanakwenda sasa wanavuka vijiji vinne mpaka wanakwenda kuwa-dump kwenye Kata nyingine, sasa unajiuliza kwa kweli hapa si ndiyo tunafuta, sasa kuna Kijiji pale? Hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha pili kinaitwa Usinga. Kile Kijiji cha Usinga kina kaya 937 zilizopendekezwa kuondolewa kwenye kile Kijiji, hebu pigeni mahesabu ndugu zangu kaya 937 zitoke kwenye eneo lake sasa zinakwenda wapi? Zenyewe zinakwenda kilometa 42 kutoka zilipo, hizi kaya 937 ambazo Rais huku amesema ameona huruma kwa wananchi, wakalishwa na kiapo, Mbunge wao pia nikabebwa na Mawaziri kama Nane walikuwepo pale wakati wanatoa kila kitu, mwaka mmoja umeisha ni mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie Serikali na kuwashauri, kwanza watambue yale maeneo tumeyatunza, mimi nimezaliwa Ukumbikakoko iko pale, Usinga ipo pale, lakini Mheshimiwa Rais kwa sababu anatupenda tunavyoongea kuna miradi ya maendeleo inaendelea pale. Upo mradi wa maji milioni 440 unaendelea, Stesheni ipo pale, pia jirani zetu wa Mpanda ninavyoongea almost ni mita 500 naianza Mpanda kuna kijiji pale, lakini unakuja kuona maelekezo ndiyo maana nikasema utaalam mwingine! Kwa kweli nimeshamuelewa sasa hivi Dkt. Musukuma namuita Daktari kabisa, kwa sababu sasa ile informal education ndiyo naiona umuhimu wake, mmenielewa ndugu zangu? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama mtu umeenda shule unasema kwamba haya vijiji vyote vinaondoka, huku miradi Rais analeta pale inaendelea, zahanati zipo, shule zipo, stesheni zipo na sasa mmeanza kukarabati reli ya kutoka Kaliua kwenda Mpanda tayari wanajenga tena kulekule sasa hii ni nini? The same Government huku tuna-argue hiki hapa, huku mna-argue kitu kingine hiki hapa! Kiongozi mmoja naye anakuja anatamka kwamba msipeleke miradi ya maendeleo huku Rais ana miradi pale inaendelea, madarasa yanaendelea pale hivi ni kitu gani hiki? Miezi michache tu nyuma wametoka pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwa kweli kwenye suala la Ukumbikakoko na Usinga ni suala ambalo mimi binafsi limeniuma sana, kwa sababu sikutarajia! Huku tamko ni hili hapa, agizo ni hili hapa lakini kinachokuja kutekelezwa ni tofauti kabisa na kile ambacho kiliamuliwa huko. Sasa maana yake nini? Tena wakanitania Viongozi wangu kule kwamba sasa nenda kawahamasishe kule nikawaambia siwezi kwenda kula matapishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waliniambia pale Mheshimiwa Mbunge kazi imefanyika wakanipamba kweli kweli nikabebwa juu, sasa agizo bado lipo pale hiki kilichotokea ni kitu gani cha kubadilisha? Shida ni nini? Kama maendeleo yote haya yapo. Hivi kuna kaya ambayo hamuifahamu kabisa kwenye Kijiji kuna kaya ambayo ina heka 300, heka
400 mpaka unafikia eti heka tano tano au ndiyo zile Mheshimiwa Mbunge mmoja alisema humu kwamba tunapokuwa na zile garden zetu tunafikiri ni mashamba, tunawa- frustrate watu, umefanya maamuzi “A” leo unakuja kuyakataa maamuzi yako au unashauri vinginevyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ipitie upya ile timu ya tathmini kama walikwenda pale tena na wahusika wakubwa ni TFS wa kule fuatilieni mtusaidie kufanya maamuzi sahihi, na hili nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu ulikuwa pale, hivi vijiji navitaja ulikuwa kwetu unatutumikia Baba tena mtiifu, mwadilifu naendeleza kazi yako, hebu tuoneeni huruma vijiji vya Kumbikakoko unavijua, mpaka sasa hivi tunavyoongea ndicho kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hilo lifanyiwe kazi tena haraka ili kuondoa frustration kwa sababu wengine wanaanza kusema usipeleke hela, usipeleke hela kwa kigezo gani? Huku miradi ya umeme inaendelea kule maana yake nini? Tunashindwa kuwa na kauli moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya ambayo yalikuwa yanagusa vijiji viwili ningependa nichangie jambo jingine. Kule kuna kuna barabara inapita ya kutokea Mpanda – Kaliua – Uliankuru - Ushetu mpaka Kahama iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na tayari wemeshafanya detail design kule na kwenye bajeti wamependekeza kujenga daraja la Ugalla, sasa mnajenga kwa ajili ya nani? Hizo Stesheni ambazo mnaboresha kwa ajili ya nani? Kama mnapendekeza wananchi huku kwamba kuna moja, mbili, tatu hakuna madhara tumetunza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo hifadhi mnaziona tumetunza, tumehangaika sisi na ndiyo maana maeneo yote tunapokaa hatuna hata mgogoro na mtu lakini kwa vijiji hivi nimeona kama maamuzi yanayofanywa, maamuzi yalifanywa sahihi na Rais wetu anayetupenda na timu yake yote ya Mawaziri huko chini huku kuna shida kinachotokea ni kingine, halafu agizo liko hivi kwamba Wilaya na Mikoa ishughulikie kuhamisha, wanahamisha wanawalipa nini? Hizo nyumba zao? Nikasema sasa hiki, yaani mimi nilichanganyikiwa! Kwa hiyo naomba tufikirie maamuzi sahihi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Kaliua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchabgia pia kwenye mradi mwingine, mimi nachangia kwenye barabara. Tunae Mkandarasi anaendelea kutoka Kazilambwa kwenda Chaya kilometa 36 ameshapita Usinge ile bypass ya Usinge shida bado nini, kwa sababu tayari mainjinia wetu wa Mkoa kila kitu wameshawasilisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini bypass ya Usinge ile kilometa Saba mliyoahidi Waziri wa Ujenzi kwa nini hamuanzi kuijenga mpaka muda mkandarasi uishe tuingie kwenye gharama na hoja zisizokuwa na msingi tuanze kuleta wakandarasi wengine, mobilization ya material na mambo mengine yaendelee. Mradi wa ufadhili hela ipo shida nini? Mimi kwa kweli napata wakati mgumu tunakuwa na kigugumizi kufanya maamuzi kwa sababu gani? Mkandarasi yupo na mambo yanaenda kwa nini tunakwama? Kwa hiyo, naomba ile bypass ya Usinge barabara ya kilometa saba ianze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningependa kulichangia. Tabora ni wakulima wa tumbaku na tumbaku inayozalishwa karibu Tanzania ni kilo milioni 44, kilo milioni 22 inatoka katika Wilaya ya Kaliua, kuanzia tarehe 20 tunakwenda kwenye masoko, sasa kule kwenye masoko nawaomba wale Wateuzi wa Serikali huwa wanafanya tathmini wakishatoka bei inayokuja wananchi wanakuja kupunjwa, haifuatwi ile bei ya wateuzi wa Serikali iliyofanyiwa tathmini, kwa hiyo masoko tarehe 20 niombe tuende vizuri, wananchi wauze tumbaku yao vizuri na mtuongeze mteuzi, mteuzi ni mmoja tu kwa Majimbo yote siyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya kuyasema haya ninaomba Serikali iyafanyie kazi kwa umakini ili tuondoe taharuki ambayo inajitokeza kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja naunga mkono Bajeti, ahsante sana. (Makofi)