Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo ina dhamira njema sana tu kwa nchi hii lakini imekuwa yenye dira nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa weledi mkubwa na kazi nzuri anazozifanywa katika majimbo yetu. Mheshimiwa Rais amekuwa kielelezo chema kwa utendaji wake wa kazi ambazo kule vijijini na hasa sisi majimbo ya vijijini tumenufaika sana kwa kiwango kikubwa mno. Vilevile pesa ambazo zimekuwa zikielekezwa chini kabisa kwenye halmashauri zetu ambako zimeenda kwenye afya, maji, elimu, miundombinu na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya dakika hizi chache itoshe tu niseme kwamba kazi nzuri sana sana na wananchi wameona matunda makubwa kabisa. Wameona zahanati zetu, wameona vituo vya afya, wameona hospitali za halmashauri zetu lakini miradi ya maji kule vijijini pamoja na kuchimbwa visima ambavyo wanaendelea navyo. Pia katika elimu tumeona baadhi ya shule mpya kabisa zikijengwa, lakini madarasa yanaongezwa katika shule ambazo zilikuwa na upungufu mkubwa wa madarasa lakini sekondari zetu, kuna kiwango kikubwa sana cha pesa ambacho kimewekezwa kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoendelea kuipongeza Serikali, lakini tunapaswa pia kushauri yale mazuri ambayo tunadhani kwa maono yetu yanaweza kuwa na tija kwa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki ni kipindi cha bajeti. Mwaka 2022 kipindi kama hiki pia tulipitisha bajeti mbalimbali za Serikali yetu. vile vile tunapokuja kwa mwaka mwingine tunatamani kuona matunda na matokeo mazuri, matokeo chanya ya bajeti zile ambazo tulizipitisha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya bajeti ambayo watu walipiga sana makofi na kuisifu ni bajeti ya Kilimo. Serikali iliamua kuongeza kwa makusudi kwa kiasi kikubwa sana bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa zaidi ya asilimia 300 na ni bajeti ambayo tuliamini matokeo yake yatakuwa bora sana. Hata hivyo, tuna mambo ambayo Watanzania watu wanatushangaa sana, tuko mbioni, tuko katika mchakato, karibu tu, yaani hatukamilishi mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo walikuja hapa katika gallery hizi Maafisa Ugani wakiwa wamevalishwa sare nzuri sana na sisi tukashangilia kwamba sasa kilimo chetu kinakwenda kukomboka, tunatoka katika kilimo hiki duni, tunakwenda sasa katika kilimo ambacho kitakuwa na maslahi mapana. Vile vile walipewa pikipiki, Mheshimiwa Rais wetu ndiye aliyewagawia wale watu na sisi tukishuhudia, walipewa vifaa vya kupimia udongo ambavyo naamini dhamira yetu iwe basi ni kwa msimu ule mmoja tuone matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wanagawiwa pikipiki, wanavalishwa magwanda hapa tunaona na tunapiga makofi, wakulima wetu ambao ni wakulima kabisa, wakulima per se walikuwa wanalima na wengine walikuwa wanavuna. Miongoni mwao baada ya muda mfupi walianza kuuza mazao yao kwa mashirika makubwa, Taasisi kama NFRA, Bodi ya Mazao Mchanganyiko lakini na watu binafsi ambao ni wajasiriamali wanaonunua dengu, kunde, choroko walienda kununua kwa wakulima wale ambao siku zote maisha yao ni ya kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuja na mipango ambayo Mawaziri hao vijana wametupa mipango mizuri sana, lakini mashaka yangu, hatuoni manufaa ya mipango hii mizuri. Toka bajeti iliyokwisha mpaka tunaingia katika bajeti nyingine hakuna matokeo ya zile pesa ambazo zilitolewa nyingi kwamba zimesafisha shamba hekari ngapi? Watu mia ngapi wanakwenda kulima? Wamevuna kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango yetu ya bajeti ni ya mwaka mmoja mmoja. Ni mipango tu ndio huwa ya miaka mitano na dira zinakuwa za miaka 25 kwa maana zinagawanywa 25 au 50 tulikuwa tuko pale kwenye maoteo nadhani ya dira ile ambayo baadaye itakuja tuichakate, lakini mipango ya miaka mitano huwa ni mipango ya mambo mengi, lakini Ilani za Uchaguzi nazo huchukua miaka mitano maana yake mpaka uchaguzi mwingine mtakuwa mmetimiza yale malengo yenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo bado hili linanitatiza. Kilimo cha Tanzania asilimia kubwa ni cha mvua. Sasa kama tulitoa pesa nyingi na bado tuko katika dhamira ya kutegemea kilimo cha mvua maana yake tuwe na mipango ya mwaka mmoja mmoja, lakini kama ni kilimo cha umwagiliaji, basi tungekuja hapa kwamba tumeshachimba angalau mabwawa 20 katika halmashauri 20 au majimbo 20, lakini tuko katika mchakato, tuko mbioni, ndio mipango yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona wanachukua vijana, dhamira njema sana, lakini vijana watatu katika halmashauri au wanne au watano wale waliopendelewa, wana impact gani katika kilimo cha nchi hii ambacho tunategemea tuka- achieve nini? Tunaenda kupata kitu gani kwa vijana watatu katika Halmashauri ya Itigi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao wakulima ambao siku zote wanalima. Kwa nini tusiwapelekee pembejeo za kutosha zile pesa tukaingiza kwenye ruzuku za trekta, wale wale wanaolima kama ni kuwasafishia mashamba, tukawasafishia wale wale vijana ambao siku zote wanalima, kuliko kuwachukua vijana na Kuwafungia Bihawana kwa miezi minne wanajifunza nini wakati Maafisa Ugani tunao? Hao waliowaleta hapa kazi yao nini? Unamfundisha mkulima kwa miezi minne na huyo Afisa ugani anafanya kazi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana wetu walimaliza Vyuo vya Kilimo SUA na vyuo vingine, kwa nini tusichukue watu wenye weledi wa kutosha kama kweli tuna dhamira ya kuajiri watu waajiriwe na kilimo? Kwa nini wale waliosoma kilimo tusiwape hiyo nafasi? Tukachukua mtu ambaye alikuwa amekaa nyumbani ambaye hajawahi kulima na kwa sababu unataka kumfundisha ili kwa sababu ana shida ya ajira, atakuja kusoma hilo somo ambalo unamfundiha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano mmoja ambao ume-fail hapa hapa Dodoma, shamba lile ambalo Mheshimiwa Rais alipita pale Chinangali lilikuwa Shamba la Ushirika wa Wakulima wa Zabibu waliwezeshwa na Halmashauri ya wilaya ya Chamwino, Benki ya CRDB iliwakopesha Dola Milioni moja kama Bilioni 1.6 wakati ule, lakini baada ya kulipa mkopo hakuna kilichoendelea, kwa sababu dhamira yao ilikuwa sio kilimo, ilikuwa ni fursa. Wangekuwa ni wakulima wangeendelea kulima kwa sababu walipewa mashamba bure na kwa sababu ilikuwa ni fursa ya ajira, walipomaliza kulipa ule mkopo na yule Meneja aliyekuwa anawasimamia, aliposema sasa nawaachieni basi lile shamba limekufa, leo tunalichukua katika utaratibu mwingine. Mfano huu ndio huu ambao tunakwenda kuuendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali tukawezeshe wakulima ambao kila siku wanalima. Tusilenge zao moja, kama mkulima wa parachichi ajengewe uwezo kwenye zao lake, kama mkulima wa mpunga ajengewe uwezo kwenye shamba la mpunga, kama mkulima wa mahindi tumwekee uwekezaji wa kutosha katika kilimo cha mahindi ili tupate matokeo mazuri kwa muda mfupi. Vile vile mipango hii ya muda mrefu ya mchakato na tuko mbioni iendelee kwa sababu ndio mipango yetu mingi. Kwa nini tusiwe na matokeo ya haraka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wakulima ambao waliuzia NFRA chakula, chakula kikaanza hadi kupelekwa nchi jirani na sisi tumesema tutakuwa hub ya chakula nchi hii. Kwa nini tusiwasaidie hawa wakulima wa Meatu, wakulima kule Iramba, wakulima wa kule Madaba, wakulima wa kule Itigi, pale alipo ardhi itengwe, kama ni hekari mia tano mia tano kila halmashauri halafu zikasimamiwa au kila jimbo. Hivi kweli ukimwezesha Mbunge kupitia halmashauri yake ile pesa atakula wakati anatengeneza kula zake? Inawezekana wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Rais hapa alileta shilingi bilioni moja za barabara kule Vijijini kwetu tulinufaika sana na mpaka leo watu wanasifia haya yanayootokea, kwa nini sasa na ninyi wa kilimo msiishushe kule chini? Hela hizi zikaenda kwa watu ambao moja kwa moja ni wakulima na wakafanye kazi za kilimo ili kilimo kiwe na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nimeona umewasha microphone, naunga mkono hoja hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)