Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kupata nafasi ya kufungua dimba asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mungu sana kwa ajili ya kutuzawadia zawadi ya uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nishukuru kupata nafasi ya kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, ambayo imewasilishwa mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunampelekea shukrani zetu kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Mvumi, kwa kazi kubwa anazozifanya. Majuzi hapa tulimsikia Mheshimiwa mama Kilango akipiga hesabu ya fedha zilizokwenda jimboni kwake. Kila Mbunge ukimsimamisha hapa atazungumzia pesa zilizokwenda kwenye jimbo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo la Mvumi Mheshimiwa Rais Dkt. Samia majuzi tu ametuteremshia shilingi bilioni tatu na milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha VETA lakini hapo kabla tulishapata pesa kwa ajili ya mradi wa booster, pesa chungu mzima, karibu bilioni sita ukijumlisha, zote zimeingia kwenye Jimbo la Mvumi; haya ni maajabu. Lazima tumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayotufanyia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata miradi ya maji katika Jimbo la Mvumi, karibu ya bilioni mbili inaendelea kujengwa katika Kata ya Mvumi Mission pamoja na Kata ya Handali; hii tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi njema anayotufanyia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo limezungumzwa katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nataka niende kwenye suala la amani na utulivu, amani na utulivu ndio msingi wa kuendesha Tanzania. Lakini Mheshimiwa Rais ameidumisha amani na utulivu kwa kuileta nchi pamoja; amekusanya makundi yote kukaa mezani pamoja ili tuzungumze namna gani tutatoka hapa tulipo kuisogeza nchi pamoja; hongera sana Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hili siyo jambo dogo, hili ni jambo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemuona Rais namna anavyohangaika kutafuta pesa. Waheshimiwa Wabunge ambao tumekaa hapa muda mrefu mtakubaliana nami, sasa hivi mimi ni kipindi cha tatu hapa; bajeti ya mwaka 2021/2022 tulipitisha hapa bajeti Mheshimiwa Rais akaenda kutafuta fedha mpaka zikapita ile bajeti; sijawahi kuona tangu tumekuwa Wabunge humu, wote, akina Mheshimiwa Ole- Sendeka mko hapa. Tumepata pesa zinazovuka bajeti kwa mara ya kwanza. Rais Dkt. Samia anafanya kazi kubwa, tusimkatishe tamaa, lazima tumsaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ninyi Waheshimiwa Mawaziri, Tanzania tumebahatika kupata Rais anayewapa uhuru mkubwa wa kufanya kazi; fanyeni kazi ya kumsaidia Rais. Rais anatafuta pesa, mnataka yeye mwenyewe aingie tena kupiga hesabu; haiwezekani. Lazima muwasimamie watu wetu. Tuwasimamie Makatibu Wakuu, tuwasimamie wahasibu, ili waweze kujibu hoja kabla hazijaletwa hapa Bungeni. Tunachokifanya hatumtendei haki Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Mawaziri, si sawa, hili jambo Mheshimiwa Waziri Mkuu, si sawa. Tunataka Rais afanye kazi ya kutafuta fedha za ujumla lakini haya mambo madogo madogo myamalize ninyi. Tumalize kero za wananchi, tumalize matatizo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vihoja vidogovidogo tunashindwa kuvijibu. Unashindwaje kumaliza tatizo katika Wizara yako wakati unajua kabisa CAG anapokuja anakuja kuhoji watu wako; wasimamie. Hizi hoja nyingine zinajibika kabisa, ndiyo maana unaona Bunge sasa tunatolewa kwenye mstari tunapelekwa sehemu kujadili hoja kabla ya wakati, kitu ambacho siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kupitisha bajeti ya nchi, tunataka kupitisha bajeti ya wananchi wa Tanzania. Hili ni jambo kubwa, lakini kwa sababu kuna baadhi ya Wizara zilizembea kushughulika na hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, ndiyo maana mnaona sasa Bunge linasukumwa pembeni tuanze kujadili kabla ya wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu zinafahamika kwamba ile ripoti ikishapokelewa na Mheshimiwa Spika inakabidhiwa kwa Kamati ya PAC (Hesabu za Serikali), Kamati ya PAC inakwenda kuchakata kwa kuwaita wote. Tunaliita jicho, wataitwa na watu wanaotuhumiwa watatoa majibu, halafu ndio Wabunge tunakuja kuamua. Sasa tukianza kuamua mapema, huo mwezi Novemba wakati PAC wamechakata tutatoa uamuzi gani tena? Tutakuwa tunajikanyaga wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, kwa hiyo, tusifanye jambo kwa mihemko. Tuna Spika mzuri, mwanasheria, anatuongoza vizuri, kwa hiyo, nina uhakika kabisa Bunge hili litaamua sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema; Mheshimiwa Rais ametoa uwazi mkubwa. Unajua hata hii ripoti yenyewe kama Rais angekuwa hataki itoke, ingetoka? Ni Rais ndio anataka, Rais ameweka mambo kwa uwazi, hataki kificho, anataka sisi tumsaidie wapi panavuja, wapi tuzibe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutapata wapi Rais kama huyu ambaye anaiongezea bajeti Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; utampata wapi? Ili aweze kukagua kila kona. Rais anataka nchi yetu tuwe wawazi ili tuweze kujua wapi kuna tatizo tusughulike nalo; wapi kuna shida tushughulike nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Mawaziri, tusimamie kwenye Wizara zetu. Mnafanya kazi vizuri, msinyongee, hakuna Waziri ametajwa mahali popote katika hii ripoti. Wasiwasi wenu uko wapi? Chapeni kazi za maendeleo ya wananchi. Tusimamie barabara, tusimamie maji, tusimamie maendeleo kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia kwenye kada ya afya, juzi Mheshimiwa Rais amefanya kufuru hapa; ameleta magari ya kuchimba visima vya maji karibu nchi nzima. Kwa hiyo, sasa hivi maana yake kila jimbo likipangiwa ratibu vitatobolewa visima virefu vya maji na kuondoa matatizo yote ya maji; hii ni kazi inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeona madarasa yalivyojengwa nchi nzima, kila jimbo limeguswa. Zamani kabla ya Mheshimiwa Samia, wananchi wetu tulichangishana mpaka wengine wangefungwa; uongo kweli? Kuna watu wangekimbia kwenye majimbo. Lakini Mheshimiwa Samia akasema hapana, tutatafuta fedha tuwapunguzie mzigo wananchi ili watu waweze kusoma shule, na sasa hivi tuna tatizo la kupeleka wanafunzi, siyo tena madawati. Madawati yapo, madarasa yapo, ila sasa watoto hawataki kwenda shule. Tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana tunapomuunga mkono Mheshimiwa Rais tumuunge kwa vitendo. Mawaziri fanyeni kazi sisi Wabunge tupo. Ukifika wakati wa kujadili Taarifa ya CAG tutaijadili kwa nguvu zote. Lakini kwa sasa tupitishe bajeti ya Serikali ambayo iko mbele yetu. (Makofi)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Ole-Sendeka.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutumia nafasi hii kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Mbunge, rafiki yangu Lusinde. Kusema kwamba jambo hili liendelee kusubiri mpaka wakati mwingine kwa maana ya kufuata ratiba mpaka Novemba ilihali mnaujua upepo uliopo nje, Watanzania wamekerwa na hatua hii ya ufisadi uliokithiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo chochote cha kuchelewesha uchukuaji wa hatua dhidi ya wahusika wa ufisadi huu wa matrilioni, mabilioni ya fedha, na bila Bunge lako kuchukua hatua ya kuunda Kamati teule au kufanya maamuzi kwa ripoti iliyokamilika ni kuchelewesha kutoa haki kwa Watanzania na huko ni kufifisha jitihada za kumuunga mkono Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya ya kukusanya fedha na kwamba hata hasira yake Bunge hili litakuwa halijamtendea haki Samia wala Watanzania kama hamtachukua hatua sasa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei kwa sababu anachangia kwenye hotuba yangu. Nilichosema ni kwamba tufuate taratibu, taratibu ni taratibu. Tumejipangia taratibu na sheria zimepangwa. Jamani eh, kuku anatotoa baada ya siku 21. Sasa Mheshimiwa Mzee Ole- Sendeka anataka atotoe kesho, yaani mayai atage leo, atotoe kesho; itawezekana jamani? Wabunge tusijidanganye, tusifikiri kwamba hapo ndiyo tunamsaidia Rais, kumsaidia Rais kwa kuvunja sheria, kwa kuvunja Bunge, kwa kuvunja kanuni itakuwa siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi maafisa masuhuli wote wako pale, wamekuja kuleta bajeti. Utawaitaje? PAC itawaitaje kwenda kushughulikia mambo yao? Kwa hiyo, ninashauri sisi wakati tunajadili hukatazwi kuligusa kaka, lakini lazima lifuate ratiba ya Kibunge. Na likifuata ratiba ya Kibunge ndiyo litakuwa na majibu sahihi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakushukuru sana; ahsante sana. naunga mkono hoja. (Makofi)