Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Bajeti kwa Wizara ya Kilimo ya Kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe na Mheshimwia Anthony Mavunde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia namfahamu Mheshimiwa Hussein Bashe tangu mwaka 2008 akigombea Uenyekiti wa Umoja wa Vijana na baadaye Umakamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana kama Katibu Mkuu wetu Isack alivyosema. Sifa pekee ambayo naweza kuisema ni kwamba ni mtu ambaye ni mgumu kubanduka katika jambo la ukweli analoliamini. Wakulima wa nchi hii wana imani kubwa kwamba kwa sifa hiyo, basi kilimo kimepata tiba ya kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mwenyezi Mungu aijalie nchi yetu iepukane na majanga na Mheshimiwa Rais akusanye mapato ya kutosha ili bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ameiomba aipate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, napenda kushukuru kwamba juzi nilisimama hapa katika Wizara ya Maji kuzungumzia mambo ya wakulima wangu wa Muwa. Napenda kutumia nafasi hii kushukuru Waziri Mheshimiwa Bashe na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, kaka yangu Martine Shigela kwa kutatua changamoto ile. Sasa hivi wananchi wangu wa Kata ya Sanje huko ni shamrashamra kwamba jambo lao limesikika na utatuzi umepatikana, wanaendelea na uvunaji wa miwa na tarehe 19 wanaanza kuingiza miwa katika kiwanda cha Ilovo kwa ajili ya uzalishaji wa sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitagusia kama mambo manne ama matatu kutokana na muda. Mkoa wetu wa Morogoro ni ghala la Taifa. Kwa hiyo, tunamwomba Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe atusaidie sana tafsiri ya ghala la Taifa, kwa kuwa Mkoa wa Morogoro ni Mkoa mzuri sana una ardhi nzuri sana inayofaa kwa kilimo cha kawaida na inafaa kwa kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa yetu ya mkoa, juzi tuliambiwa tuna hekta karibu laki 300 zinazofaa kwa umwagiliaji, lakini nasikitika kidogo kuna miradi imeanzishwa na Serikali na inakwama Morogoro haiendelei, hasa ya umwagiliaji. Nitakutajia baadhi hapa ili Mheshimiwa Waziri unisaidie kuinukuu na wale wanaopulizapuliza usije Kilombero, washindwe, walegee, uje uione hii miradi na uone jinsi fedha za Serikali zimewekwa na miradi haijakamilishwa, wananchi wanapata adha kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Skimu ya Mang’ula Youth, fedha za Serikali zimeenda pale, mradi haujakamilika. Tuna Mark Magombela, tuna mradi wa Kisawasawa, Serikali ilipeleka fedha lakini haijapeleka fedha za kumalizia. Wakulima hawana pa kuhifadhi mazao yao kama Msalise na Mkula. Maeneo mengine wameomba Shilingi milioni 280 kumalizia na maeneo mengine wameomba Shilingi milioni 150 kumalizia, lakini fedha hazijaenda. Kwa mfano, Mkula wawekezaji wamejenga maghala makubwa kabisa, na mwekezaji kafunga hajamaliziwa fedha yake na wakulima wanashindwa kuhifadhi mpunga wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama tunasema Mkoa wa Morogoro ni ghala la Taifa na tunaweza kuzalisha; unajua karibu 50% ya hitaji la mchele tu la ndani ya nchi yetu, Mkoa wa Morogoro peke yake unaweza. Sasa kama miradi hii haitafanyiwa kazi, kwa vyovyote vile ni wazi kwamba hatutaweza kuwa ghala la Taifa kikwelikweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kibaoni pale karibu na Ifakara Mjini kuna hekta karibu 10,000 Lungongole ambazo zinafaa kwa kilimo, lakini bado upembuzi yakinifu unasuasua kutokana na ufinyu wa fedha. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri utusaidie ili tuweze kutafsirika kama Mkoa wa Morogoro ni ghala la Taifa. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Waziri pamoja na sifa tunazosema kwako na msimamo wako, katika muda atakaokujalia Mwenyezi Mungu kuongoza Wizara ya Kilimo, itakuwa ni aibu kubwa sana ukiacha nchi hii inaagiza sukari kutoka nje. Itakuwa aibu kubwa kweli kweli! Sisi Morogoro hasa Kilombero kama wakulima wa muwa, nami nimekuwa nikipiga kelele kila siku kuhusu wakulima wa muwa na mambo ya ushirika; nitasema baadaye kuhusu ushirika. Sukari, sukari, sukari, ni aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kuzungumza habari ya importation of sugar, najua ni vita kubwa hii ya uingizaji wa sukari. Kwa msimamo wako tunajua uta-control, isiue kilimo chetu cha ndani cha miwa. Maana yake sisi tulienda Kilombero na Waziri aliyepita akaona miwa karibu 200,000 inabaki. Yaani nchi hii tunaingiza sukari na juzi nimemwona Rais Museven anazindua Kiwanda cha Sukari kitakachozalisha tani 5,000 kwa siku, yaani cha kawaida tu. Sisi tuna-import sugar wakati tuna ardhi ya kutosha, tuna kila kitu cha kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, achana na ardhi, miwa imeshalimwa tani 200,000 kiwanda hakina uwezo. Waziri akaenda akatoa statement pale wawekezaji wa Ilovo wakakubali kufanya expansion ya kiwanda. Mpaka sasa hivi imeishia kwenye ku-clean layer tu, wanasema tunaogopa. Importation of sugar; kwamba kuna mashaka kwamba sukari itaingizwa bila utaratibu. Tutawekezaje hapo 500 billion? Mheshimiwa Waziri tuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kile na upanuzi huo usipofanyika, na hata nimemwona Balozi Mpungu amezungumza kwenye vyombo vya habari akielezea mashaka yake katika uwekezaji ule. Miwa tani 200,000 itaendelea kubaki; na mpaka Magereza walikuwa wanaendelea kulima miwa, na matokeo yake ni kwamba wananchi malalamiko yao yataendelea, na nchi yetu itazidi kuingiza sukari kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua uingizaji wa sukari na vibali hivi vina faida yake, lakini ni wazi kwamba nchi hii hatutakiwi kuingiza sukari kutoka nje. Sisi tunatakiwa kuzalisha sukari kuuza nje. Nimeona hata wawekezaji wa Kagera wale, wakina Nasoro wa Kagera wanahangaika na maeneo tu, wapewe maeneo waweze kulima miwa wazalishe sukari. Wapeni maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wilaya ya Kilombero upande wa Mlimba kule Mofu kuna hekta 10,000 za Bodi ya Sukari zinamilikiwa. Unatafuta mwekezaji mdogo azalishe sukari. Kwa hiyo, katika uongozi wako legacy mojawapo ni kuhakikisha utamu wa nchi hii kwa wananchi katika chai unazalishwa na unatosheleza wenyewe humu humu ndani na unakuwa wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu; ukiwa Naibu Waziri wakulima wangu wameshasafiri na mabasi hapa mara tatu au mara nne ukawapokea wakilalamikia makato ya kodi ya 2% na ulitoa statement kwamba hela yenu mtarudishiwa. Mpaka sasa hivi hawajarudishiwa. Wakulima wa Kilombero wanauza sukari, hawauzi miwa. Ndiyo mkataba wa kiwanda na wakulima. Wakulima, unalima muwa wako, kiwanda kinavuna, kinaenda kinachakata, kinauza, kikishauza, kikishatoa gharama zote, ndiyo mkulima analipwa na kodi imekatwa. Mkaja kuanzisha 2% ya kwenye mazao, wamekatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alitoa statement kwamba ile pesa itarudishwa, haijarudishwa. Sasa huko mbele tukiwa na nia ya kushika Shilingi tutakuwa tunakukosea adabu, lakini ukweli ni kwamba unajua mwenyewe wanakaa mwezi, wanapanda basi, wanakuja kufuatilia two percent yao. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa ahadi zenu hizo mhakikishe kwamba fedha zao mnazirudisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Doctor hapa mtaalamu wa ushirika, fanya mabadiliko katika ushirika; na hii hafumbifumbi macho, mimi mwaka 2021 nimefuatilia matatizo ya ushirika. Nimeenda pale kusaini kitabu kwa Mrajisi Taifa hapa mara 11, watu wanaingilia hapa wanatokea hapa. Fanya mabadiliko katika ushirika, lete modal. Yupo Mheshimiwa Dkt. Cherehani hapa, ukikaa naye, unajua ana utalaamu wa ushirika, anaweza kukusaidia mawazo. Watu wanalalamika sana kwenye ushirika, na taarifa ya Waziri Mkuu hapa Bungeni inatosha kukupa picha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu anasema vyama 6,013 vilivyokaguliwa, vyama 357 pekee ndiyo hati zake zinaridhisha. Kuna watu wa Ushirika tuna Mrajisi tuna nani, na Morogoro wana matatizo makubwa, mimi siumi maneno na mwaka jana iliundwa tume mpaka leo taarifa inafichwafichwa, siumi maneno kama Mkoa wa Morogoro Ghala la Taifa Ushirika hawajatimiza wajibu wao na vyama hivyo katika vyama 6,013 na sisi tumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawahami, watu hawarekebishwi, watu hawabadilishwi kama mikoa mingine tunavyoona. Ukisema wanasema Mbunge una ajenda binafsi, haiwezekani Waziri ukaja hapa ukatuambia Waziri Mkuu katoa taarifa kasema vyama 6,013 Waziri Mkuu wa nchi hii, vyama 357 pekee ndiyo vina hati ya kurizisha, Waziri ukileta statement yako hapa lazima utujibu taarifa hiyo wa Waziri Mkuu wewe unaishughulikia kwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kengele imepigwa, nakushukuru naomba kusisitiza kuunga mkono bajeti lakini kusisitiza kwenye ruzuku ya mbolea, chonde chonde wakulima wangu wa mpunga, wakulima wangu wa miwa wanataka ruzuku katika mbolea. Mwaka huu jasho limewatoka kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)