Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi njiweze kuchangia katika Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema tu kwamba sisi ni sehemu ya Umoja wa Nchi za Afrika ambao katika makubaliano ya Azimio la Malabo tulikubali kwamba, asilimia 10 ya bajeti iweze kutengwa kwa ajili ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kutenga bilioni 751.12 niongezeko la asilimia 255 ikilinganishwa na bajeti iliyopita. Ongezeko la asilimia 255 ni kweli kwamba ni la kupongezwa, linaonesha utashi na azma ya Mheshimiwa Rais ya kuboresha kilimo. Na tunatamani kwamba sisi kama signatories wa Malabo Declaration tufikishe asilimia 10, kwa sababu hii bilioni 751 ni asilimia 1.83 ya bajeti, ni kama tumeanza sasa kuipukuchua. Kwa hiyo tuombe sana kwamba, hebu matokeo yatakayotokana na ongezeko kubwa hili yasababishe Serikali kuona kwamba inafikia kiwango ambacho sisi tumekuwa tukikubaliana na wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi katika Kamati ya Kilimo tunaamini kwamba, kama kilimo kikipewa msukumo mkubwa kama ambavyo tumekubaliana, tunaamini kwanza nchi itajitosheleza kwa chakula na kubakiza ziada kubwa kwa ajili ya kuuzwa nchi za nje. Yaani watu wataamini kwamba, kama kuna dhiki na dhahama mahali fulani basi Tanzania ni mahali pa kukimbilia. Lakini pia uchumi wa wananchi mmoja mmoja na uchumi wa Taifa utakua kwa kiasi kubwa sana na nchi itakuwa inatatua tatizo la ajira kwa vijana. Na inawezekana hata tatizo la machinga ambalo limekuwa ni gumzo katika nchi likaondoka kwa sababu ya kuweka msukumo mkubwa katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna jambo tumejifunza sana kutokana na crisis ya Ukraine na Urusi ni kwamba kama nchi tunapaswa kujitegemea kujitosheleza kwa mazao ya chakula yale ya msingi lakini na mafuta ya kula. Hilo nadhani lisiondoke katika vichwa vyetu, tumejifunza kwamba wakati wa crisis ni muhimu sana uwe unajitosheleza kwa mahitaji yale ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo napenda kutambua na kupongeza jitihada za Serikali na azma ya Mheshimiwa Rais kupitia Wizara ya Kilimo kwamba imeamua kwa dhati kuimarisha utafiti, lakini pia kupima afya ya udongo. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na uongozi wote wa Wizara niwapongeze sana kwa msisitizo wa kusema kwamba watatoa ruzuku katika mbegu bora na kutoa ruzuku katika mbolea. Haya mambo yalipaswa kufanywa zamani, lakini kwa sababu tumekuwa na mwanzo basi tuendelee hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina hoja fulani ninayotaka kuiweka hapa, kwamba historia inakupa namna ya kujifunza kwa ajili ya leo, lakini pia na kwa ajili ya kesho na kwa sababu hii ni historia ya nchi yetu ukiangalia katika kilimo kumekuwa na cycle fulani ambayo nataka kuiweka hapa kama hoja yangu ya msingi. Hoja hiyo ni kwamba, nchi inaanzisha zao fulani inaliita zao la kimkakati na Serikali inatia nguvu, watu wanalima kwa nguvu zote lakini baada ya muda unashaanga tu kwamba zao lililokuwa la mkakati zao hilo linakufa. Halafu Serikali inakuja kulifufua tena na mfano ni zao la mkonge na zao la ngano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwamba baada ya mageuzi haya ambayo tumeyaanzisha sasa, hii cycle ikome, ifikie mahali tunaposema kwamba tunazalisha parachichi, tunazalisha ngano, tunazalisha zao Fulani, basi sisi tuwe kinara ili wakati wa crisis watu wajue kwamba tukienda Tanzania tunapata haya mazao. Kwa hiyo hiyo cycle ya kuanzisha, kufa, kufufua, kuanzisha, haitufanyi tukawa na maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni block farms. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwamba katika hili natambua kabisa kwamba ni jambo la msingi, lakini hebu tuone kwamba vijana tena vijana halisi wanaoonekana ndiyo, waingie hapa pamoja na umuhimu wa kuwepo wawekezaji wakubwa lakini vijana tunajua kwamba watakuwa hawana mitaji, lakini Serikali inapaswa iwape upendeleo ili vijana hawa ndiyo waingie katika block farms kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeondokana na tatizo la ajira za vijana ambao wanamaliza level mbalimbali za elimu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa sababu ya muda ni kwamba kilimo ni ushindani na nchi jirani sisi tunapopanga hapa kwamba tuimarishe kilimo chetu na nchi jirani wanafanya hivyo hivyo na masoko yetu ni hayo hayo. Napendekeza hiki kitengo kisiwe ni Kitengo cha Utafiti lakini Wizara iwe na Kitengo cha Intelijensia kuangalia mwenendo wa masoko ili kwamba kama kunatokea tafrani mahali fulani basi kitengo hiki kinaweza kikatoa information ya namna ya kwenda. Kwa hiyo hiki tuweze kukifanya na tukifanya hivyo naamini kwamba nasi tutaendelea kuwa washindani katika soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hivyo, naomba kuunga hoja mkono ahsante sana. (Makofi)