Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Katani Ahmadi Katani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tandahimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu. Vile vile nakushukuru wewe kwa kunipa fursa. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitamshukuru kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan hususan kwa sisi wakulima wa korosho kwa kutupa pembejeo bure kwa mara ya pili mfululizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inayofanywa na Waziri wa Kilimo wa sasa, kama bajeti hii ambayo leo anaiomba ya Shilingi bilioni 751 itatoka kutoka Wizara ya Fedha, naamini Taifa hili kwenye kilimo tunakwenda kufanya mapinduzi makubwa sana. Tunajua dhamira yake ya dhati, yeye na Naibu wake pamoja na watendaji wake wa Wizara ya Kilimo, kuanzia Katibu Mkuu Mzee Andrew Masawe; Naibu Katibu Mkuu, Profesa Siza, wanafanya kazi kubwa kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanakwenda kupata tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye korosho, Waziri amefanya jambo kubwa na sina namna zaidi ya kumpongeza. Mwaka huu tarehe 5 Mei, 2022 kwenye Kijiji changu kimoja, Kata yangu moja ya Nanyanga amefanya uzinduzi pale wa upuliziaji wa korosho. Kampuni moja inayoleta dawa; kampuni ya Benz imejitolea kutoa mafunzo kwa wakulima jambo ambalo halikupata kutokea. Hii inaonesha commitment ya Waziri na wazabuni walioleta dawa kuonesha namna gani viuatilifu vyao vina ubora. Wameamua kwenda kutoa mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Wizara kwamba mafunzo yale yasiwe zimamoto, yaende kusambazwa nchi nzima, ikiwezekana kwa wazabuni wote wa dawa, ili kama kuna mkulima atashindwa kupuliza dawa vizuri, tujue kwamba Serikali iliwajibika pamoja na wazabuni waliwajibika. Jambo mlilolifanya ni kubwa na hili lifanyeni sehemu zote zinazolima korosho, mtakuwa mmesaidia wakulima sana, maana watu wanapata elimu ya upuliziaji. Maana yake mnapoleta viuatilifu hivi vina mabadiliko ya majina, wakati mwingine wakulima hawajui kwamba zile dawa ingredients ni sawa, wanadhani labda dawa zina matatizo. Mnapoamua kuleta wazabuni, wakaamua kutoa mafunzo, mnakwenda kuongeza uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Waziri, kama watafanya jambo lile mwaka huu wa 2022, mwaka jana, 2021 waliongeza uzalishaji kwa asilimia 40, mwaka huu wanakwenda kuongeza kwa asilimia 100. Lifanyeni kwa nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kulikuwa na uzinduzi wa ugawaji wa pembejeo, umesimamiwa na Mkuu wetu wa Mkoa wa Mtwara, lakini ukiusoma mwongozo uliotolewa na Bodi ya Korosho, wanaokwenda kusimamia ugawaji, Wenyeviti wa Serikali ya Vijiji hawamo; Madiwani ambao ndio Wenyeviti wa Kamati za Maendeleo ya Kata hawamo. Ushauri wangu kwa Serikali Mheshimiwa Waziri, huwezi kwenda kusambaza pembejeo ukamtoa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji. Yeye ndio anawajua wakulima halisi kuliko hata watu wa Vyama vya Msingi. Watu wa Vyama vya Msingi wakati mwingine kwa sababu ya ukata, wanaweza kuchomekea mkulima ambaye hayupo ilimradi mtu apate chochote maisha yaende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomshirikisha Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, unapomshirikisha Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ambaye ni Mheshimiwa Diwani, maana yake mnakwenda kutengeneza uwiano wa kujua kwamba mazao haya dawa hizi zinakwenda kumfikia nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji ndio anawajua watu wa eneo lile. Mheshimiwa Diwani wa Kata husika ndio anawajua watu wa eneo lile. Leo mnaandaa Kamati za Ugawaji wa Pembejeo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hayumo na Diwani wa Kata hayumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha kesho hapa, atoe tamko kabisa kwa nchi nzima, Wenyeviti wa Serikali ya Vijiji Waheshimiwa Madiwani ni lazima wawepo kwenye ugawaji wa pembejeo na wawepo kwenye mfumo ule. Naomba sana kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ana kazi kubwa sana na namna pekee ya kusaidia mzigo huu, ni lazima akae na Naibu Waziri wake na Naibu Waziri ni Mwanasheria. Sheria za Ushirika ziko ovyo. Mwaka 2021 Waziri amekamata watu na pembejeo Tunduma. Matokeo yake kwa sababu tuna sheria ambazo haziwasaidii, wale watu ni wahujumu uchumi kama wahujumu uchumi wengine. Pembejeo za bure zinapotolewa na Mheshimiwa Rais, dhamira yake ni kumsaidia mkulima. Anapopatikana mtumishi mmoja, anakwenda kuiba pembejeo, unakwenda kuikamata Tunduma, unamfungia ofisini kwako mpaka saa 7.00 usiku, haitakusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iletwe sheria hapa mahususi kabisa tutakayokwenda kuipitisha Wabunge, mtu anayekwenda kuhujumu pembejeo za mkulima, huyu awe ni mhujumu uchumi kama mhujumu uchumi mwingine. Hata ikiwa ni mifuko miwili, tutawasaidia wakulima na tutakomesha huu wizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashawishi Wabunge wenzangu, tumekaa hapa, Maafisa Ugani wetu wote wanasimamiwa na TAMISEMI, lakini ndio Maafisa Kilimo tuliokuwa nao vijiji vyote na kata zote. Naomba Wabunge wenzangu tuone namna ya kuisaidia Wizara, Maafisa Ugani wote warudi Wizara ya Kilimo, wasimamiwe na Wizara ya Kilimo. Hii itatusaidia sana. Mtakapotoa maelekezo yataenda moja kwa moja kuliko contradiction ambayo sasa tunaipata. Wako TAMISEMI, mnatoa maelekezo wakati mwingine watu wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu hawajui wawajibike kwa nani. Kumbe ni watu walipaswa kwenda Wizara ya Kilimo. (Makofi)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Kuchauka.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji. Ni kweli jambo analolizungumza kuhusu Maafisa Kilimo, kwani wao sasa hivi ndio Watendaji wa Kata. Yaani kwenye Mtendaji wa Kata, Mtendaji wa Kijiji akiondoka, nafasi inazibwa na Afisa Ugani kwa sababu ndio wanaoonekana wako lose, hawana kazi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Katani unapokea taarifa?

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa kwa mikono miwili kabisa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye suala la utafiti. Mimi nikupongeze Waziri, nimeona mmeongeza kutoka shilingi bilioni 7.35 mpaka shilingi bilioni 11.65. Kwenye jambo hili kwenye korosho tunakuta mnaweka fedha ambazo zinakwenda kwenye utafiti. Sasa kama huku mmeongeza fedha zinakwenda kwenye utafiti, tunataka kwenye mjengeko wa bei sasa tusione makato yanayokwenda kwenye utafiti tena, maana hapa tunashawishi Wabunge wenzetu tupitishe bajeti hii.

Mheshimwia Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Mwijage, hii ni bajeti ya Taifa. Unapozungumza kilimo ambacho kinakwenda kuwanufaisha Watanzania zaidi ya asilimia 65 ni eneo ambalo angekuwepo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Mchemba hapa, ningemwomba sana kaka yangu, katika Wizara ambazo bajeti zake alipaswa fedha zake apeleke zote, basi Wizara ya kwanza ingekuwa Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana huko aliko, wasaidizi wake kama wapo, namwomba sana Waziri wa Fedha, namwomba sana Waziri wa Fedha, namwomba sana Waziri wa Fedha, Wizara hii ya Kilimo bajeti hii iliyopangwa ipelekwe yote tumpime Mheshimiwa Bashe kwa fedha ambazo mtakuwa mmempa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wamezungumza wenzetu vizuri sana, kwa namna ulivyoichakata bajeti hii ya kilimo, kama mtapata fedha na ikasimamiwa vizuri, ndiyo kitakuwa kipimo sahihi, lakini kama tutapeleka fedha asilimia 46, asilimia 50, hatutampima Mheshimiwa Bashe wala Mheshimiwa Mavunde pale. Maana watakuwa na utetezi kwamba tuliomba Shilingi bilioni 751, tumepata Shilingi bilioni 300 na ngapi. Tumpeni Shilingi bilioni 751, tunaporudi mwakani hapa tuwe na kitu cha kumwuliza kwamba uliomba shilingi bilioni 751, umepewa, kilimo kimefika wapi? Uzuri wake wewe una makisio. Kila mahali ulipokwenda umeweka matarajio yako, umeweka maoteo yako. Maoteo yako hayatakwenda kutimia kama hizi fedha ambazo umeomba hazitakuja kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumwomba tena Waziri wa Fedha, kwenye jambo hili tujitahidi na Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha fedha za Wizara ya Kilimo zisipungue japo shilingi ili tupime utekelezaji mzuri wa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)