Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii adhimu kumpongeza sana na kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake ya dhati kuhakikisha kilimo cha Tanzania kinakua na kuhakikisha kwamba sekta za uzalishaji zinapatiwa fedha ili kuinua uzalishaji nchini katika kupambana na hali ya uchumi wetu, kuingiza fedha za kigeni, kutatua matatizo ya wananchi wetu na hasa wakulima ili waweze kulima kilimo chenye tija na waweze kupata faida ya jasho lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo limedhirika wazi baada ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kukabidhi vitendea kazi kwa Maafisa Ugani wetu pamoja na vifaa mbalimbali ikiwemo vifaa vya kupimia afya ya udongo. Hiyo ni dhamira ya dhati na huo ni mwanzo mzuri wa kuona kwamba sasa tunakwenda kupiga hatua katika sekta hizi ya kilimo na uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo napongeza pia mpango wa Wizara ambao unakwenda kutoa ruzuku kwa wakulima wetu hivi karibuni. Pamoja na na kutoa hizo ruzuku bado naishauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya mbolea vya hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji umeanza kwa kiwanda cha mbolea na vingine vilianza huko nyuma, naishauri Serikali iendelee na uwekezaji kwa wananchi wetu wa hapa ndani pia wawekeze kwenye sekta hii ya viwanda vya mbolea, kwa sababu, mbolea ni silaha kubwa katika kilimo popote duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakapotokea changamoto nyingine zozote duniani kwenye sekta hii ya mbolea basi na sisi tuwe na akiba yetu ya mbolea hapa nchini tuweze kukidhi mahitaji yetu ya wakulima wetu ndani ya nchi, ikiwemo kupanda kwa bei ya mbolea mara kwa mara, kupanda kwa mambo mbengine yatakayojitokeza ya kimazingira na mabadiliko ya tabianchi, lakini na sisi tukiwa na viwanda vyetu vya mbolea hapa nchini, ambavyo vitakwenda kuzalisha mbolea zinazolingana na udogo wa nchi yetu kutokana na mazingira tofauti tofauti ya nchi yetu, itakwenda sana kumkomboa mkulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu, Mheshimiwa Waziri amegusia kuhusu kuzalisha mbolea asili, nami nakubaliana naye katika kuzalisha mbolea asili. Mbolea asili ziende pamoja na viuatilifu asili. Tunavyo viuatilifu vyetu asili na Wizara kupitia vitengo vyake vya utafiti vimeshafanya utafiti kwa baadhi ya viuatilifu, ni vema viuatilifu hivyo vikatangazwa wananchi wakavijua na kuweza kuvitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta hii ya kilimo kumeongezwa fedha kwenye utafiti, huduma za ugani, umwagiliaji, tunaomba katika fedha hizi zilizoingizwa nyingi kwenye bajeti hii ya kilimo, bado tunahitaji fedha zaidi za uwekezaji mkubwa katika kilimo. Fedha hizi zilizoingizwa zilizowekwa kwenye bajeti tunaomba zitoke kwa wakati, kwa sababu zinapotoka mwisho wa mwaka kilimo kinakwenda kwa miongo na bado hatujajiweka sawa kwenye umwagiliaji, hivyo inapokuja fedha miongo ile imeshapita, fedha zile zinakuwa sasa zimekuja mwisho. Tunaomba fedha zije kwa wakati zikafanye kazi kwa wakati kulingana na mazingira ya kilimo kwa Mikoa tofauti, hali ya hewa tofauti na kilimo tofauti katika mazingira tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, niongelee kuhusu utoshelevu wa mafuta. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imejipanga kuhakikisha kuna utoshelevu wa mafuta nchini. Nami naipongeza Wizara kwa mikakati mbalimbali. Tunaomba sote tu-support Wizara ya Kilimo kufuatia watendaji wake, tuunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo ya mafuta, Wizara imewekeza hivi sasa kuliimarisha zao la nazi kwa kutoa miche 2,000. Miche 2,000 ni kidogo mno, kwa sababu kuna baadhi ya maeneo mafuta wanatumia tu kwa sababu hawana la kufanya, lakini matumizi makubwa ni nazi. Kwa hiyo, tukiimarisha hili zao la nazi, litakwenda kupunguza ule upungufu wa mafuta uliopo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna haja ya kujipanga katika mazao ya biashara na mazao ya kukidhi mahitaji yetu ya nchi. Kwenye mazao ya biashara tuangalie soko liko wapi? Mazao gani yana soko? Halafu turudi kwa wakulima, tuhamasishe wakulima wetu walime vipi. Hapo hapo tuimarishe uhifadhi na vifungashio ili mazao yetu yawe na ubora. Vifungashio pia ni sehemu ya kuvutia biashara kwani biashara ipendezayo ndiyo inunuliwayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiacha suala la vifungashio, sasa niipongeze Serikali kwa kuwekeza mtaji mkubwa kwenye Benki ya Kilimo. Benki hii itakwenda kumkomboa mkulima mdogo. Tunaiomba Serikali, kila inapoweza kuongeza mtaji kwenye Benki hii, iendelee na juhudi za kuongeza mtaji ili tuone wakulima wetu wananufaika na kuweza kukidhi mahitaji ya kilimo ikiwemo vitendea kazi ili wavutike na biashara hii ya ukulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubalina na Wizara katika kuuboresha ushirika, ufanyiwe kazi kwa haraka kutatua zile changamoto na pia kutazama udhaifu uliopo kwenye ushirika na kuyaboresha kwa muda huu muafaka ili ushirika uweze kumkomboa mkulima wetu mdogo ambaye anahitaji sana nguvu ya kusaidiwa na Taasisi hii ya Ushirika ambayo ndiyo taasisi tunayoiona kwa sasa inayoweza kumpunguzia matatizo mkulima katika kuhifadhi mazao yake ambayo yanapotea na pia kumtafutia soko la uhakika katika kuuza mazao yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana juhudi zinazofanywa na Wizara kuwekeza Ofisi za Umwagiliaji katika Halmashauri au Wilaya zote za Tanzania. Tunachoomba kwa Mheshimiwa Waziri, hao wahusika wapewe ushirikiano na Wizara na Taasisi zilizopo katika maeneo husika ili waweze kufanya kazi zao kwa uadilifu na kumsaidia mkulima katika sekta hii ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimalizia, niseme kilimo ni biashara, kilimo ni utatuzi mkubwa kwa wananchi wa Tanzania. Naiomba Serikali, kila itakapokuwa na uwezo, basi iwekeze katika sekta hii ya kilimo. Tumpe moyo Mheshimiwa Rais wetu, kwa dhamira yake ya dhati ya kuinua sekta hii na Mheshimiwa Waziri anajipanga vizuri, tunaomba tumpe support kabisa ili tuweze kumkomboa mkulima mdogo aweze kupata tija kwa anachokivuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)