Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya mimi pia kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kusema kwamba ninaunga mkono hoja, ikiwa ni pamoja na haya nitakayokwenda kuyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuchangia mimi nitakwenda kwenye mfumo wa kurasa ili niweze Kwenda haraka. Ninaanza ukurasa wa 13, ambapo kwenye hotuba wameongelea Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi. Napongeza sana hatua hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuna matatizo. Mashirika haya ya Serikali ambayo yanafanya biashara yamekuwa hayafanyi vizuri. Mfano mzuri ni pamoja na kile Kiwanda cha Ngozi ambacho kipo pale Moshi Mjini, ambacho kilitakiwa kiwe kinaajiri angalau watu 3,000; na kwenye mnyororo wake wa faid ampaka watu 10,000. Hata hivyo mpaka sasa kimeajiri watu 250 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili hizi taasisi za kibiashara za Serikali zifanye vizuri ni vizuri namna ya kuwapata viongozi wake isiwe kwa namna ya uteuzi na badala yake tuwe tunawatafuta kutokana na merits, uwezo na competence yao kwenye hizo fields. Kwa kufanya hivyo viwanda hivi vitafanya kazi vizuri. Kwa hiyo kwenye hiki kiwanda kinachoanzishwa, ikiwa ni pamoja na vingine watu wapatikane kwa merits ili waweze kuviendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende ukurasa wa 14 na ukurasa wa 45 ambao umeongelea viwanja vya ndege. Nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Yetu Samia Suluhu Hassan. Moshi Mjini tunarekebisha kiwanja chetu cha ndege ambacho ni muhimu sana kwa Moshi Mjini, Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na nyanja mbalimbali ikiwemo utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilete ombi; kuna nyumba ambazo zilivamia eneo lile; baadhi zina hati na nyingine hazina hati. Niombe, ili kuleta tija zaidi kwenye ule uwanja vile viwanja tutafute namna ya kuvifidia wakati huu ambapo mradi unaendelea ili kiwanja kile kiweze kupanuliwa katika kiwango kinachotakiwa kuwezesha mpaka hizi ndege hizi za bombardier kutua pale na kuleta tija zaidi. Kwa hiyo, kwa sababu ujenzi unaendelea ni rahisi kwa Wizara kuweka fidia pale kwa baadhi ya zile nyumba ili kuweka sura ile inayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendele ukurasa wa 41, na hili linaendana sana na swali ambali nimeliuliza asubuhi kwenye maswali ya nyongeza. Kwenye matumizi bora ya ardhi, pale kwenye ukurasa wa 41, hotuba imeelezea vizuri sana; lakini kuna maeneo ambayo yanahitaji kupewa kipaumbele zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Moshi Mjini ina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 58. Tulishaleta maombi yaliyopita kwenye michakato yote, ya kuongeza eneo eneo mpaka kufikia kilometa za mraba 142, na tulishapata GN No. 219 ya tarehe 15 Julai, 2016. Mchakato ule ulisimama. Nimeshaandika barua nimepeleka kwa Waziri Mkuu, Wizara ya Ardhi na TAMISEMI ili kuomba huo mchakato tu kwanza wa kupanua ile mipaka ukamilike. Tunaomba hivi kwa sababu ninavyoongea hapa sasa hivi Moshi Mjini tumekosa eneo la dampo, tumekwenda kununua eneo Moshi Vijijini ndiko dampo letu liliko. Pia makaburi yetu yanajaa, tutalazimika Kwenda kununua tena maeneo mengine ya makaburi na huduma nyingine za wananchi ilhali tayari kuna mchakato ulishafikia sehemu nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme, kwa pale tulipo sasa, kwa sababu ni padogo sana hata pato letu haliwezi kuongezeka, hata eneo la viwanda haliwezekani kwa sababu viwanja vinakwenda pembezoni. Hata hivyo, zaidi ni kwamba yale maeneo ambayo tuliyaweka kwenye master plan ya kipindi cha nyuma, kwa ajili ya kupanua, tayari yanaendelea kuvamiwa na kujengwa kiholela. Si tu kuvamiwa, watu wanauza na yanajengwa kiholela. Maana yake ni kwamba hata mtakapokuja kuturuhusu kupanuka tutapanuka kuendana na maeneo ambayo hayajapangika vizuri. Kwa hiyo ninaomba sana hili la Moshi Mjini mlichukulie kwa uzito wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende ukurasa wa 51, umeeleza vizuri sana juu ya elimu, na mimi hapa nitagusa Wizara zote mbili, Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI kwa sababu ni suala ambalo linagusa kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Moshi Mjini tuna Shule ya Sekondari ya Mawenzi, ni shule nzuri, ina miundombinu mizuri na ina eneo kubwa. Shule hii ina mchanganyiko. O-Level wako day lakini A-Level wako boarding. Ninaleta ombi, Wizara ionge namna ya kuifanya shule hii iwe na boarding kuanzia O-Level mpaka A-Level. Hii ni kwa sababu kuna eneo kubwa hivyo itakuwa miongoni mwa shule nzuri kama zilivyo Shule ya Moshi na Shule Moshi Tech. Kwa hiyo tunaomba sana watuwekee mabweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini shule mpya tuliyoijenga, shule ya Msandaka ambayo iko pembezoni kidogo, nayo Halmashauri tumetenga zaidi ya milioni 150 kwa ajili ya mabweni. Tunaomba Wizara sasa nayo iangalie ili tuongeze shule hizi za mabweni katika manispaa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye ukurasa wa 61 na 62, kumeongelewa masuala ya kazi, wafanyakazi na mifuko ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vya Serikali vilibinafsishwa. Kiwanda cha magunia, Kiwanda cha Moshi Leather, kiwanda cha utilization; wafanyakazi waliokuwa wanafanya kazi kwenye hivi viwanda wakati vikiwa vya Serikali hawajawahi kulipwa mafao yao na wanaendelea kudai. Wanasumbuka kuja ofisini kwangu kwa makundi kila siku, na wengine mpaka wameshaaga dunia wakiendelea kudai. Naomba Serikali ifanye mpango, iangalie namna ya kutafuta fedha ili kuwalipa waliokuwa watumishi wa mashirika ya umma yaliyobinafsishwa ambao wanatangatanga, hawapewi hatima yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 62 ni kuhusu mifuko ya jamii, nako kumekuwa kuna usumbufu mkubwa usio wa lazima. Baadhi ya watu wanapokuwa wamemaliza muda wao wa utumishi, wengine ni watumishi wa Serikali, kama walimu, unakuta amestaafu kabla hajapandishwa daraja. Anapokwenda kutafuta daraja lililokuwa haki yake anazungushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, wastaafu hawa ambao wameshaitumikia Serikali wanapopata huu usumbufu kwa kweli wanatupa picha mbaya sana kw ahata hawa wanaotumika sasa hivi kuona kwamba unaweza ukatumikia kwa moyo lakini mwishowe ukaja ukapata mateso.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 65 ni kuhusu uwezeshaji wa wananchi kiuchumi; nilishaliongea mara nyingi na ninashukuru sana Mheshimiwa Rais ameona twende kwa njia hiyo. Hii mikopo ambayo hairejeshwi ni kwa sababu ya watu tuliowapa kazi hiyo, Maafisa Maendeleo ya Jamii hawana utaalam wa ku-assess mradi, kukopesha na kwenda kuchukua mkopo huo. Ninaungana moja kwa moja na wazo la Mheshimiwa Rais kwamba tutafute benki ambazo tutawapa hizi kazi na sisi tuendelee kuwa wasimamiaji wakuu na kusiwe na interest wala collateral kama ilivyo, ni jambo linalowezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 69 na 73, kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na mapambano dhidi ya dawa za kulevya; kwa bahati mbaya hapa nitatumia lugha ambayo si rafiki sana. Kwa hii rushwa tunayoona, kwa haya mazingira tunayoyasikia kutokana na taarifa ya CAG suala ya rushwa tuchukue njia waliyoichukua China, tutoe adhabu kali zaidi, miaka 30, 40, 50, hata ikibidi adhabu za kunyongwa, kwani tunachoogopa ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku tulikuwa na mjadala kuhusiana na adhabu ile ya kubaka. Mtu akibakwa afanywe nini miaka 30, mmoja wa watu waliokuwa wameshiriki ile washa akasema hapana ni kubwa mno tukamwambia basi wewe umejiandaa kubaka. Kama wewe unaona adhabu hiyo ni kubwa umejiandaa kufanya hilo tukio. Hili suala la rushwa, suala la madawa ya kulevya tupitishe sheria hapa itakayoweka adhabu kali, miaka 30, 40 na ikibidi kunyongwa kwa wale wanaoshiriki ili tukomeshe, kwa sababu tunapoona aibu kusema hivyo maana yake hawa wanaokosa hizo haki nao wanateseka na wengine wanakufa kwenye mahospitali na kwenye maeneo yetu ya haki. Kwa hiyo, mimi nimeona nichukue njia hiyo ngumu kuishauri Serikali tufikirie suala hilo kwa njia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 83, kuna ukatili dhidi ya watoto. Nashukuru sana kwa sababu maazimisho ya Dawati la Jinsia Kitaifa yalikuja kuzinduliwa Moshi Mjini na taarifa iliyosomwa na Waziri wa Kisekta Dkt. Gwajima, ilionesha katika asilimia 100 ya watoto wanaofanyiwa ukatili, asilimia 60 wanafanyiwa nyumbani na kwa sababu nyumbani wanafanyiwa na ndugu na kama ni ndugu maana yake kesi haziendi mahali. Sasa tuna kitu cha kufanya, ni lazima tutafute namna bora hata ikibidi tuwe na namba maalum ya watoto kuweza kuifikia, wakifanyiwa ukatili waweze kutoa taarifa na inapoonekana ni ndugu, sisi Serikali tuichukue sisi na sio ndugu, maana ndugu wanaombana msamaha, wanamaliza wakati mtoto anakuwa ameshaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwe na njia ya kuhakikisha tunawalinda hawa watoto. Haya madhara ambayo tunayaongelea ya hii tabia inayokuja pengine wengine wanalazimika kwenda kwa sababu walishafanyiwa ukatili, wakaona ile ndio njia. Kwa hiyo nashauri sana kwenye ukatili huu wa Watoto, tuwe na namba maalum ambayo watoto wanaweza kuipiga lakini tuwe na uwezekano wa kubadilisha sheria nazo ziwe kali na hata ikibidi tunaweza tukafanya vitu ambavyo kimsingi vitaonekana sio vizuri. Kwa mfano, hakuna sababu ya ndugu ambao wameshafikia umri wa mature kuendelea kukaa na kulala chumba kimoja na watoto wetu, tunaamini kwamba ni ndugu hawatawadhuru lakini taarifa ndio hiyo imetoka asilimia 60 wame…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)