Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mambo makubwa kabisa ambayo anaifanyia nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru pia kwa hotuba nzuri ya Waziri Mkuu kila mtu humu ndani anafahamu namna ambavyo Waziri Mkuu ni mwema, muungwana ambaye ni rahisi kabisa kufikika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nichangie kwenye maeneo mawili muhimu, Eneo la kwanza ni eneo la maji, moja ya maeneo ambayo yamekuwa na shida kubwa ya maji kwenye nchi yetu hii ni Wilaya ya Chemba ni kwa sababu ya hali ya kijiografia ni maeneo machache sana ambayo ukichimba maji unapata.

Mheshimiwa Spika, nataka nimshukuru Waziri wa Maji baada ya kuelewa changamoto hizi yapo mambo makubwa sasa Chemba yanafanyika naomba nitaje miradi michache tu ambayo sasa inaendelea. Ninafahamu watanzania wote wanafahamu moja ya changamoto kubwa ya wananchi ni maji. Na hasa maeneo ya vijijni kama kwetu, kwenye eneo langu la chemba kuna miradi mingi inaendelea moja ya miradi hiyo ambayo kwa dhati kabisa namshukuru Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa Kelema ambao una milioni 500, Mradi wa Babayo ambao unaendelea una milioni 500, Mradi wa Kubungo unaendelea unazaidi ya milioni 335, Mradi wa Chandama milioni 550, mradi wa machija una milioni 700 na mradi wa visima 11 vya awali milioni 550. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya yanaenda kupunguza kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa maji. Naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais lakini pia namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji. Mara kadhaa kule ambako nimeenda kutoa ushauri ni namna gani tutatue chamgamoto ya Chemba kwa sababu ni maalum ameweza kunielewa na kunisikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika. Pamoja na miradi hiyo lakini pia tuna miradi mikubwa ya mabwawa nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu jana katika hotuba yake alielea kwa kina namna gani wanaenda kutekeleza mradi wa Bwawa la Farukwa. Kwenye bajeti iliyopita tulitengewa milioni 283 nishukuru watu wako site na kazi inaendelea.

Mheshimiwa Spika, kwenye mradi huo kuna jambo la kufanya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ukisoma vizuri andiko la mradi ule linaeleza linaenda kuhudumia watu milioni 2.5 wa Dodoma mjini haliongelei kokote Habari ya Chemba. Mheshimiwa Waziri Mkuu tumefika kwenye eneo la mradi ukatuahidi na sisi tutapata maji naomba wataalamu wetu waanze kufikiria ni namna gani na sisi tuaenda kupata maji kwenye mradi ule.

Mheshimiwa Spika, nishukuru sana namna ambavyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Waziri wa Maji ambaye mara kadhaa umefika kwenye mradi huo. Lakini pia niwashukuru kumekuwa na miradi ya mabwawa midogomidogo. Tumechimba mabwawa manne kwenye mwaka huu wa fedha lakini pia tuna mradi mkubwa wa bwawa la bilioni tatu pale Chidoka. Kandarasi ilitangazwa tukaenda kumtambulisha mkandarasi lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu mpaka leo yule mkandarasi hajawahi kufika sijui nini kinaendelea.

Mheshimiwa Spika, ninaomba sana hebu yule mkandarasi afike kwa sababu tulimchezea ngoma siku ile tunafungua ule mradi sasa akipotea moja kwa moja nauliza sasa zile ngoma tulicheza mbona sasa hivi hayumo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru sana kwa kweli Wizara ya Maji lakini pamoja na shukrani hizo yapo maeneo naomba wanisaidie tumefanya survey wenyewe kwenye vijiji tisa kwa ajili ya kupata maji. Na nafahamu kuna hizi mashine za Uviko zimekuja Dodoma kwa sababu tume survey wenyewe kwa gharama zetu kwenye vijiji vya Chang,ombe, Magandi Jinjo, Jangalo, Songoro, Piho, Tandala, Dinai, Takwa tunaomba zile mashine zikaanzie eneo la Chemba kwa sababu ndio eneo ambalo lina asilimia ndogo zaidi ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndani ya miaka miwili hii ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tumepunguza upungufu wa maji kwa asilimia kubwa sana watu ambao wanafikafika Chemba wanafahamu kwamba miaka miwili iliyopita upatikanaji wa maji ulikuwa ni asilimia 23 sasa hivi tume jump mpaka asilimia 36, haya ni mageuzi makubwa sana lakini miradi hii ikikamilika, miradi hii ambayo sasa hivi inaendela tunaenda kupanda mpaka kwenye asilimia 54. Kwa hiyo, nisipomshukuru Mheshimiwa Rais kwa fedha nyingi ambazo zinapatikana nitakuwa siyo muungwana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba nitoe shukrani kwenye eneo la barabara miaka miwili iliyopita bajeti ya barabara ya Chemba ilikuwa ni milioni 700 tu lakini mtandao mzima wa barabara ulikuwa ni kilomita 736 unaweza ukafikiria ni namna gani unaweza kutengeneza unamtandao kilometa 700 halafu unapata bajeti ya milioni 700. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sasa tumeongezewa zaidi tunapata bilioni 2.3 angalau maeneo mengi ya vijijini yanaweza kupitika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaombi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. kwa barabara ambayo inatoka Kontoro, Sanzawa, hadi Ntendo lakini pia inavuka eneo la Mto Bibu kwa hiyo bajeti ya bilioni 2.3 hakuna namna ambavyo tunaweza kujenga imeshafanyiwa kila kitu na inahitaji zaidi ya bilioni tatu yenyewe peke yake. Wakati Mheshimiwa Rais amekuja Chemba Dkt. Samia Suluhu Hassan nililisema hilo na tukaahidiwa sasa tuwasiliane na Wizara husika ili kazi ile ikafanyike nikuombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu hebu tusaidie katika hilo maana fedha zinazokuja kwa ajili ya barabara hatuna uwezo wa kutumia maana tulitumia fedha hizo bilioni 2.3 maana yake sasa tutumie fedha zote kwenye barabara moja wakati barabara nyingine zitakuwa zina hali mbaya.

Mheshimiwa Spika, tuna barabara kubwa ambayo imetangazwa kandarasi, barabara ya kutoka Kibarashi, Handeni hadi Singida. Barabara hii zaidi ya kilomita 100 ipo kwenye jimbo langu na ambaye nina uhakika barabara hii ikijengwa Maisha ya watu wa Chemba itakuwa rahisi sana. Lakini barabara hiyo ina viunganishi vya barabara ambavyo kujenga peke yake itakuwa changamoto nyingine.

Mheshimiwa Spika, ninomba kuna kiunganishi cha kutoka Goima Mondo hadi Bichwa kuunganisha na barabara kuu ya Arusha chenye kilomita kati ya 24 na 28 nacho naomba kiangaliwe namna ya kujengwa lakini si hiyo tu kuna barabara ya kutoka Malamaya kiunganishwe na hiyo barabara eneo la Donsee kilometa kati ya 28 na 26 nazo hizo barabara zinatakiwa zitafutiwe fedha ili ziweze kujengwa kwa hiyo kufanya hivyo tutakuwa tumepata package nzima ya barabara yote ambayo hii sasa tunaongelea ya kutoka Kibarashi hadi Singida kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba pia kuishukuru Serikali kwa sababu yapo mambo mengi yamefanywa kwenye Afya. Miaka miwili iliyopita Chemba haikuwa na Hospitali ya Wilaya kulikuwa na ujenzi umeanza lakini tumepata fedha zote na hospitali imekamilika zipo changamoto za Watumishi, sasa hivi pale, ipo changamoto ya Gari ya Ambulance. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ikikupendeza kwa sasa hivi hospitali inahudumia watu wengi sana inahudumia watu zaidi ya laki tatu. Kama kuna uwezekano wa kupata gari sehemu yoyote kwa sababu kwa saizi hali iliyopo inabidi tukachukue gari la Kituo cha Afya Mbijo ili lije lifanye kazi kwenye Hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, tatizo hilo limekuwa ni tatizo la muda mrefu na nimewahi kuliuliza kwenye swali la nyongeza lakini nikaahidiwa mpaka sasa hivi hatujapata gari hilo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya nakushukuru sana, kwa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)